Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 8 ambaye anaishi kwenye kituo cha kutunza watoto waliokimbia ndoa za lazima na ukeketaji, FGM

Fahamu ukweli kuhusu ukeketaji(FGM)

© UNICEF/Henry Bongyereirwe
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 8 ambaye anaishi kwenye kituo cha kutunza watoto waliokimbia ndoa za lazima na ukeketaji, FGM

Fahamu ukweli kuhusu ukeketaji(FGM)

Haki za binadamu

Mambo muhimu 
• Ukeketaji unahusisha uondoaji wa sehemu au sehemu yote ya siri ya nje ya mwanamke au kuweka jeraha lingine kwa viungo vya uzazi vya mwanamke kwa sababu zisizo za kimatibabu. 

  • Kitendo hiki hakina faida za kiafya kwa wasichana na wanawake. 
  • Ukeketaji unaweza kusababisha kutokwa na damu nyingi na matatizo ya kukojoa, na baadaye uvimbe, maambukizo, pamoja na matatizo wakati wa kujifungua na kuongezeka kwa hatari ya vifo vya watoto wachanga. 
  • Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 walio hai leo wamefanyiwa ukeketaji katika nchi 30 za Afrika, Mashariki ya Kati na Asia ambako ukeketaji unafanyika kwa kiwango cha juu. 
  • Ukeketaji mara nyingi hufanywa kwa wasichana wadogo wa umri wa kati ya uchanga na miaka 15. 
  • Ukeketaji ni ukiukaji wa haki za binadamu za wasichana na wanawake. 
  • Kuna ushahidi unaopendekeza kuwa kuna ushiriki mkubwa wa watoa huduma za afya katika vitendo hivyo. Hii inajulikana kama matibabu. 
  • Shirika la afya duniani (WHO) linapinga aina zote za ukeketaji, na linapinga watoa huduma za afya kufanya ukeketaji. 
  • Matibabu ya matatizo ya kiafya yatokanayo na ukeketaji katika nchi 27 zenye maambukizi makubwa yanakadiriwa kugharimu dola za Kimarekani bilioni 1.4 kwa mwaka na inakadiriwa kuongezeka hadi dola bilioni 2.3 ifikapo mwaka 2047 ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa. 
Wasichana wakimsikiliza muelimishaji rika wa mtandao wa Y-Peer kuhusu madhara ya ukeketaj iau FGM huko shuleni kwao Garoe jimboni Puntland, Somalia.
© UNFPA Somalia/Tobin Jones
Wasichana wakimsikiliza muelimishaji rika wa mtandao wa Y-Peer kuhusu madhara ya ukeketaj iau FGM huko shuleni kwao Garoe jimboni Puntland, Somalia.

Nani anafanya ukeketaji? 

Ukeketaji unajumuisha taratibu zote zinazohusisha uondoaji wa sehemu au jumla yote ya sehemu ya siri ya nje ya mwanamke.  
Zoezi hilo mara nyingi hufanywa na waganga wa jadi na wanaokeketa wanajulikana kama mangariba.  
Ukeketaji unatambulika kimataifa kama ukiukaji wa haki za binadamu za wasichana na wanawake.  
Inaonyesha ukosefu wa usawa uliokita mizizi kati ya jinsia, na unajumuisha aina ya ubaguzi dhidi ya wasichana na wanawake.  

Karibu kila mara hufanywa kwa watoto na ni ukiukaji wa haki za watoto. Kitendo hicho pia kinakiuka haki za mtu za afya, usalama na uadilifu wa kimwili, haki ya kuwa huru kutokana na mateso na ukatili, unyama au udhalilishaji, na haki ya kuishi, katika mazingira ambayo ukeketaji huo unasababisha kifo. 

Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.
UNICEF/Holt
Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.


Aina za ukeketaji (FGM)

Ukeketaji umegawanywa katika aina 4 kuu: 
Aina ya 1: Huu ni uondoaji wa sehemu au kinembe chote (sehemu ya nje na inayoonekana ya kisimi, ambayo ni sehemu nyeti ya sehemu ya siri ya mwanamke), na/au mkunjo wa ngozi unaozunguka sehemu ya siri ya mwanamke.  
Aina ya 2: Huu ni uondoaji wa sehemu au kisimi chote na labia ndogo (mikunjo ya ndani ya uke), pamoja na au bila kuondolewa kwa labia kubwa (mikunjo ya nje ya ngozi ya uke). 
Aina ya 3: Pia inajulikana kama infibulation, huku ni kupunguza kwa mwanya wa sehemu ya uke kupitia utengenezaji wa muhuri wa kufunika sehemu hiyo. Muhuri huundwa kwa kukata na kuweka upya labia ndogo, au labia kubwa, wakati mwingine kwa kushona, na au bila kuondolewa kwa kisimi/kinembe. 
Aina ya 4: Hii inajumuisha taratibu zingine zote zenye madhara kwa sehemu ya siri ya mwanamke kwa madhumuni yasiyo ya matibabu, kama kutoboa, kuvuta, kuchanja, kukwarua na kuchoma sehemu za siri. 

Hauna faida zozote za kiafya, bali kusababisha madhila 

Ukeketaji hauna faida zozote za kiafya, na unadhalilisha wasichana na wanawake kwa njia nyingi. Unaharibu uke wa mwanamke na huingilia utendakazi wa asili wa miili ya wasichana na wanawake. Ingawa aina zote za ukeketaji huhusishwa na ongezeko la hatari ya matatizo ya kiafya, hatari ni kubwa zaidi kutokana na aina kali zaidi za ukeketaji. 

Athari hizo ni pamoja na 
• maumivu makali 
• kutokwa na damu nyingi (kuvuja damu nyingi) 
• uvimbe wa tishu za viungo vya uzazi 
• homa kali 
• maambukizi ya magonjwa kama pepopunda 
• matatizo ya mkojo 
• matatizo ya uponyaji wa jeraha 
• Kupata mshtuko 
• Na hata kifo. 
 

Msichana barubaru aliyeokolewa kutokana na kitendo cha ukeketaji akiwa darasani nchini Uganda.
UNICEF/Henry Bongyereirwe
Msichana barubaru aliyeokolewa kutokana na kitendo cha ukeketaji akiwa darasani nchini Uganda.

Na matatizo ya muda mrefu ni pamoja na 

  • Matatizo wakati wa haja ndogo (kukojoa kwa uchungu au maumivu makali, maambukizi ya magonjwa ya njia ya mkojo); 
  • Magonjwa ya sehemu za siri kama (kutokwa usaha, kuwasha, magonjwa yatokanayo na bakteria na maambukizi mengine); 
  • Matatizo ya hedhi (hedhi inayoambatana namaumivu makubwa na ugumu wa kupitisha damu ya hedhi, nk) 
  • Kuwa na jeraha la maisha 
  • Matatizo ya kushiriki ngono (maumivu wakati wa kujamiiana, kutofurahia tendo la kujamiiana na kutoridhika au kufika kileleni) 
  • Hatari ya kuongezeka kwa matatizo wakati wa kujifungua (kujifungua kwa shida, kutokwa na damu nyingi, kuhitaji upasuaji, kujifungua mtoto mfu na vifo vya watoto wachanga 
  • Kuhitaji kufanyiwa upasuaji baadaye: kwa mfano, kuziba au kupunguza uwazi wa uke (sababu ya aina ya 3 ya ukeketaji)
  • Matatizo ya kisaikolojia (Msongo wa mawazo, wasiwasi, Kupata kiwewe baada kujifungua na kutojiamini. 
Mwanamke akiongoza kundi moja huko Mali la kuhamasisha wanawake na wasichana kuhusu aina zote za ukatili ikiwemo ndoa katika umri mdogo na ukeketaji kwa lengo la kuleta mabadiliko ya tabia na kuacha tabia hizo.
© UNICEF/Harandane Dicko
Mwanamke akiongoza kundi moja huko Mali la kuhamasisha wanawake na wasichana kuhusu aina zote za ukatili ikiwemo ndoa katika umri mdogo na ukeketaji kwa lengo la kuleta mabadiliko ya tabia na kuacha tabia hizo.

 
Nani yuko hatarini? 

Ukeketaji mara nyingi hufanyika kwa wasichana wadogo kati ya umri wa utoto na ujana, na mara kwa mara kwa wanawake watu wazima.  
Kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO takwimu zilizopo kutoka nchi 30 ambako ukeketaji unafanyika katika maeneo ya Magharibi, Mashariki na Kaskazini Mashariki mwa Afrika, na baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati na Asia, zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 walio hai leo wamefanyiwa vitendo hivyo, huku zaidi ya wasichana milioni 3 wakikadiriwa kuwa katika hatari ya kukeketwa kila mwaka.  
Kwa hivyo ukeketaji ni changamoto na suala la kimataifa.

Sababu za kitamaduni na kijamii za kufanya ukeketaji

WHO inasema sababu zinazofanya ukeketaji ufanywe hutofautiana kutoka eneo moja hadi jingine na vile vile baada ya muda, na ni pamoja na mchanganyiko wa mambo ya kitamaduni katika familia na jamii. 

  • Pale ambapo ukeketaji ni utaratibu wa kijamii (kaida ya kijamii), shinikizo la kijamii la kufuata kile ambacho wengine wanafanya na wamekuwa wakifanya, pamoja na haja ya kukubalika kijamii na hofu ya kukataliwa na jamii, ni motisha kubwa ya kuendeleza mila hiyo. 
  • Ukeketaji mara nyingi huchukuliwa kuwa sehemu muhimu ya kulea msichana, na njia ya kumtayarisha kwa utu uzima na ndoa. 
Wasichana wengi wako hatarini ya ukeketaji na ndoa za utotoni hususan wakati wa janga la COVID-19.
UNFPA
Wasichana wengi wako hatarini ya ukeketaji na ndoa za utotoni hususan wakati wa janga la COVID-19.


 Ukeketaji mara nyingi huchochewa na imani kuhusu kile kinachochukuliwa kuwa tabia ya kujamiiana inayokubalika. Inalenga kuhakikisha ubikira kabla ya ndoa na uaminifu wa ndoa. 

  • Pale ambapo inaaminika kuwa ukeketaji huongeza fursa za ndoa, kuna uwezekano mkubwa wa kufanywa vitendo hivyo. 
  • Ukeketaji unahusishwa na maadili ya kitamaduni ya uke na adabu, ambayo ni pamoja na dhana kwamba wasichana ni safi na warembo baada ya kuondolewa kwa sehemu za mwili zinazochukuliwa kuwa najisi, zisizo za kike au za kiume. 
  • Baadhi ya watu wanaamini kwamba vitendo hivyo vinaungwa mkono na dini, ingawa hakuna maandiko ya kidini yanayoeleza jambo hilo. 
  • Viongozi wa kidini huchukua misimamo tofauti kuhusiana na ukeketaji: wengine wanauendeleza, wengine wanaona kuwa hauhusiani na dini, na wengine wanachangia kuutokomeza. 
  • Miundo ya ndani ya mamlaka kama vile viongozi wa jamii, viongozi wa kidini, magariba, na hata baadhi ya wahudumu wa afya wanaweza kuchangia kudumisha desturi hiyo. Vile vile, wanapoelimishwa, wanaweza kuwa watetezi wazuri wa kuachana na ukeketaji. 
  • Katika jamii nyingi, ambapo ukeketaji unafanywa, inachukuliwa kuwa ni mila ya kitamaduni, ambayo mara nyingi hutumiwa kama hoja ya kuendeleza ukatili huo. 
Ngariba nchini Uganda ambaye sasa anaunga mkono juhudi za kutokomeza ukeketaji.
UNICEF/Nakibuuka
Ngariba nchini Uganda ambaye sasa anaunga mkono juhudi za kutokomeza ukeketaji.

Gharama kubwa kwa nchi 

WHO imefanya utafiti wa gharama za kiuchumi za kutibu matatizo ya kiafya yatokanayo na ukeketaji na imegundua kuwa gharama za sasa kwa nchi 27 ambako takwimu zilipatikana ni kubaini kuwa jumla ya dola za Kimarekani bilioni 1.4 zimetumika katika kipindi cha mwaka mmoja (2018).  
Kiasi hiki kinatarajiwa kupanda hadi bilioni 2.3 katika miaka 30 ijayo kufikia  (2047) ikiwa vitendo vya ukeketaji vitaendelea na hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 68% la gharama za kutokuchukua hatua.  
Hata hivyo, ikiwa nchi zitaachana na ukeketaji, gharama hizi zingepungua kwa asilimia 60% katika kipindi cha miaka 30 ijayo. 

Mwanamke akiwa ameshikilia kisu kilichotumika kwenye ukeketaji.
UNICEF/Catherine Ntabadde
Mwanamke akiwa ameshikilia kisu kilichotumika kwenye ukeketaji.

 

Hatua Muhimu

Kwa kuzingatia kazi ya miongo iliyopita, mwaka wa 1997, WHO ilitoa tamko la pamoja dhidi ya mila ya ukeketaji kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA). 
Tangu 1997, juhudi kubwa zimefanywa kukabiliana na ukeketaji, kupitia utafiti, kufanya kazi ndani ya jamii, na mabadiliko katika sera za umma. 
Mwaka huu wa 2022, WHO itazindua mwongozo wa mafunzo juu ya mawasiliano yanayomhusu mtu binafsi (PCC), mbinu ya ushauri ambayo inawahimiza watoa huduma za afya kupinga mitazamo yao inayohusiana na ukeketaji na kujenga ujuzi wao wa mawasiliano ili kutoa ushauri nasaha wa kuzuia ukeketaji.