Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake 100 nchini Somalia waahidi kutokeketa binti zao

Wasichana wakimsikiliza muelimishaji rika wa mtandao wa Y-Peer kuhusu madhara ya ukeketaj iau FGM huko shuleni kwao Garoe jimboni Puntland, Somalia.
© UNFPA Somalia/Tobin Jones
Wasichana wakimsikiliza muelimishaji rika wa mtandao wa Y-Peer kuhusu madhara ya ukeketaj iau FGM huko shuleni kwao Garoe jimboni Puntland, Somalia.

Wanawake 100 nchini Somalia waahidi kutokeketa binti zao

Afya

Pindi Halima, * alipokuwa na umri wa miaka 8, alikeketwa na mama yake kwa kutumia kiwembe. Mama yake alikuwa ni mkunga wa jadi. 

“Kitendo hicho kilikuwa cha maumivu makali, na hakutumia hata nusu kaputi au dawa ya kufubaza maumivu. Nilivuja damu kwa siku kadhaa,” anakumbuka Halima katika Makala ya shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA.

Anaendelea kusema, “nililala kitandani kwa zaidi ya miezi mitatu huku nikiwa na tatizo la kutoa haja ndogo.”

Alipofikia umri wa ubarubaru kutoa hedhi ilikuwa ni shida kubwa. Hali ilikuwa mbaya zaidi alipoolewa ambapo hata tendo la kujamiiana na mume wake lilikuwa la uchungu. Na baada ya kubeba ujauzito, kujifungua ndio ilikuwa hali ngumu zaidi ambapo uchungu ulidumu kwa siku kadhaa.

Licha ya machungu yake aliyopitia, Halima alikubali binti yake wa kwanza naye akeketwe. “Binti yangu alikeketwa kwa njia ile inayoitwa sunna ambapo ni sehemu kidogo tu ya sehemu yake ya siri ilikatwa na alipata machungu niliyopitia,” anasema Halima.

Lakini kwa kuwa haikuwa ukeketaji kamilifu wenye machungu zaidi unaohusisha kushona kabisa sehemu ya siri ya mwanamke, watu waliwadhihaki wakisema binti yake hakuwa msafi.

Halima, mwenye umri wa miaka 50 na mama wa watoto watano wa  kike na watano wa kiume, sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani  nje kidogo ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Eneo hilo ni makazi ya kaya 280 zilizokimbia kijiij cha Danunay kilichoko takribain kilometa 250 kutoka Mogadishu, na sababu ya kukimbia ni mashambulizi.

Halima katika jamii yake ana ushawishi mkubwa na mwanajamii ambaye ushawishi wake umewezesha kubeba jukumu la kuhamasisha jamii kuondokana na mila potofu ya ukeketaji ambayo  yeye na binti yake wamepitia.

Takwimu za ukeketaji Somali zinasemaje?

Takwimu za utafiti wa hali ya afya na jamii nchini Somalia mwaka 2020 zinaonesha kuwa asilimia 99 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 nchini Somalia wamekeketwa na wengi wao walifanyiwa hivyo wakiwa na umri wa kati ya miaka 5 hadi 9.

Utafiti huo pia unaripoti kuwa asilimia 72 ya wanawake wanaamini kuwa ukeketaji ni sharti la dini ya kiislamu ijapokuwa baadhi ya viongozi wa dini hiyo wanasema dini ya kiislamu inalaani kitendo hicho.

Sitaki tena binti zangu wengine na wasichana wengine wapitie machungu ambayo mimi nimepitia- Halima

Mwaka 2020 UNFPA ilipatia wanawake na wasichana 52,225 wa kisomali huduma za ulinzi na tiba dhidi ya FGM, ingawa hakuna sheria ya kuharamisha ukeketaji au FGM, mwaka jana jimbo la Puntland lilipitisha sheria ya kutokomeza ukeketaji.

Mwelekeo mpya

Kama sehemu ya harakati za UNFPA na taasisi ya IFRAH, kampeni ya Mpendwa Binti ilizinduliwa na Halima pamoja na wanawake wengine wenye ushawishi kambini wakapata mafunzo kuhusu madhara ya ukeketaji na katika moja ya warsha akaelezea uzoefu wake.

“Wakati wote wa mafunzo, kumbukumbu za madhara ya jinsi ukeketaji umeathiri maisha yangu zilikuwa zinanijia,” amesema Halima.

Miaka mitatu iliyopita, binti mdogo alifariki kambini kutokana na kuketwa. Sasa Halima anachagiza jamii ili janga hilo lisirudie tena. Na taasisi ilisambaza kwa kaya 100 redio kutoka UNFPA ili wanafamilia waweze kusikia ujumbe wa kuhamasisha. 

“Imekuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu kufanya kazi kuokoa wasichana dhidi ya machungu yasiyo ya lazima yatokanayo na FGM, “ anasema manusura wa kitendo hicho Ifrah Ahmed, muasisi wa taasisi ya Ifrah huku akiongeza kuwa Halima ni mfano wa jinsi ambavyo wanaweza kubadili mustakabali wa wasichana wa Somalia.

Kampeni hiyo ilianzishwa mwaka jana inachagiza sauti za wanawake na wanaume ili kutokomeza ukeketaji nchini Somalia.

Mtaalamu wa masuala ya ukatili dhidi ya wanawake huko UNFPA nchini Somalia, Nkiru I. Igbokwe, anasema kampeni inalenga jamii za vijijini na mijini ambazo zinachukua hatua za kipekee ndani ya maeneo yao kutokomeza FGM.

Kutokana na ushawishi wa Halima, takribani akina mama 100 akiwemo mama mzazi wa Halima na wakunga wengine wa jadi wameahidi kutokeketa tena hivyo kuepusha wasichana 200 dhidi ya kitendo hicho.

Halima anaahidi “sitaki binti zangu wengine na wasichana wengine kupitia machungu niliyopitia.”

*Halima si jina lake halisi na limetumika kuhifadhi utambulisho wake.