Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MINUSCA kanda ya magharibi nchini CAR atembelea kambi ya TANBAT 6

Luteni Kanali Amin Stevin Mshana (katikati), Mkuu wa TANZBATT 6 akiwasili Berbérati, Mambéré-Kadéï, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
TANZBATT 6/Kapteni Mwijage Inyoma
Luteni Kanali Amin Stevin Mshana (katikati), Mkuu wa TANZBATT 6 akiwasili Berbérati, Mambéré-Kadéï, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Mkuu wa MINUSCA kanda ya magharibi nchini CAR atembelea kambi ya TANBAT 6

Amani na Usalama

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, MINUSCA Kanda ya magharibi Brigedia Jenerali Zarrar Haider ametembelea kikosi cha 6 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, TANBAT 6 kilichoweka kambi Berberati, Mambéré-Kadéï.

Brigedia Jenerali Zarrar Haider ametua katika kambi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa akitokea katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui na moja kwa moja akakutana na maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na askari walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa kikosi hiki cha sita kutoka Tanzania.

Amewakumbusha walinzi wa amani kuendeleza kazi nzuri wanayoendelea nayo ya ulinzi wa amani ikiwemo kuendeleza ushirikiano na taasisi za dini, afya na wadau wengine wa ulinzi wa amani ndani ya MINUSCA.

Aidha amewakumbusha kujua wajibu wao ikiwemo kufahamu ni wakati gani watatumia nguvu na kuwa makini sana na mabomu ya ardhini wanapokuwa katika majukumu ya ya ulinzi wa amani lakini pia kuendelea na kuwa makini na ugonjwa wa COVID -19 na malaria ili watekeleze majukumu yao ya ulinzi wa amani.

Kwa upande wa TANBAT 6, akitoa shukrani kwa niaba ya kikosi hicho, Mkuu wa kikundi hicho Luteni Kanali Amini Stephen Mshana kuendeleza yote aliyoahidi. 

« Umesisitiza kuhusu ushirikiano na wadau wakiwemo makao makuu, viongozi wa serikali na wenzetu vikosi vya ulinzi vinavyotuzunguka. Mkuu tunafanya hivyo na tutaendelea kushirikiana nao. Tunatambua kwamba MINUSCA ni jumuishi na ulinzi wa wananchi ni jukumu la pamoja kwa hiyo hakuna namna TANBAT 6 itatimiza jukumu lake bila ushirikiano. Nami kama kamanda wa kikosi nitalilisisitiza katika kila hali »