Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamhuri ya Afrika ya Kati yahitaji msaada wa kibinadamu-UN

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ursula Mueller akiwa ziarani CAR
OCHA
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ursula Mueller akiwa ziarani CAR

Jamhuri ya Afrika ya Kati yahitaji msaada wa kibinadamu-UN

Msaada wa Kibinadamu

Jamhuri ya Afrika ya Kati  CAR inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu. Ghasia zinasambaa taifa zima kwa haraka na raia wa kawaida wanaendelea kutaabika na hali ya kutokuwa na usalama nchini humo.

Hayo yametamkwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA-, Ursulla Mueller, wakati akikamilisha ziara yake ya siku nne nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo pia ameiomba jamii ya kimataifa kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa hali hii ya kusikitisha  inakuja  wakati  ufadhili wa misaada ya kibinadamu nchini CAR ikiwa  unapungua kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Idadi ya wakimbizi wa ndani  imeongezeka mara dufu, hadi mwaka jana na kufika 694,000. Mashirika yanayotoa misaada ya kibanadamu yanakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi na yanapata shida kutimiza mahitaji yanayozidi kuongezeka.

Mkuu huyo, katika ziara yake hiyo,  amesisitiza  umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa raia wa kawaida na usalama kwa ujumla na pia kuhimiza kuwa uimarishaji wa usalama ni chachu kwa utoaji misaada kwa watu walio katika hali tete sambamba na malengo ya kibinadamu.