Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Mashambulizi ya M23 huko Kivu Kaskazini yaua raia 131 – Ripoti

Clémence Ndabohweje, mwenye umri wa miaka 49, akisafisha vyombo nje ya makazi yake kwenye kambi ya wakimbizi ya ndani ya Kanyaruchinya huko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kufuatia mashambulizi ya M23. Anaishi hapa yeye na watoto wake 6 na waj…
UNICEF/Arlette Bashizi
Clémence Ndabohweje, mwenye umri wa miaka 49, akisafisha vyombo nje ya makazi yake kwenye kambi ya wakimbizi ya ndani ya Kanyaruchinya huko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kufuatia mashambulizi ya M23. Anaishi hapa yeye na watoto wake 6 na wajukuu watatu.

DRC: Mashambulizi ya M23 huko Kivu Kaskazini yaua raia 131 – Ripoti

Amani na Usalama

Ripoti ya uchunguzi wa awali uliofanywa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu imethitibisha kuwa takribain raia 131 waliuawa wakati waasi wa M23 waliposhambulia vijiji viwili kwenye mji wa Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini humo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa Habari jijini New York, Marekani siku ya Alhamisi amesema M23 walifanya mashambulio hayo tarehe 29 na 30 mwezi uliopita wa Novemba kwenye vijiji vya Kishishe na Bambo kwa kile walichoeleza kuwa ni mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya raia.

Miongoni mwa watu hao 131 waliouawa, 102 ni wanaume, 17 ni wanawake ilhali 12 ni Watoto.

Wanawake na wasichana walibakwa

“Watendaji hao waliofanya uchunguzi wa awali wanasema kuwa watu hao waliuawa kwa risasi na visu. Halikadhalika watu wengine 8 walijeruhiwa kwa kupigwa risasi, wengine 60 walitekwa na takribani wanawake 22 na wasichana watano walibakwa,” amesema Bwana Dujarric.

Solange, mtoto mwenye umri wa miaka 11 (aliyevalia nguo ya rangi ya chungwa) alitenganishwa na famili yake alipokimbia mapigano. Sasa anaishi na familia enyeji lakini mchana anakuweko kwenye  kituo cha  malezi cha  UPDEDO kinachosaidiwa na UNICEF. Anapat…
UNICEF/Arlette Bashizi
Solange, mtoto mwenye umri wa miaka 11 (aliyevalia nguo ya rangi ya chungwa) alitenganishwa na famili yake alipokimbia mapigano. Sasa anaishi na familia enyeji lakini mchana anakuweko kwenye kituo cha malezi cha UPDEDO kinachosaidiwa na UNICEF. Anapatia stadi za kufuma vikapu.

MONUSCO imelaani vikali ukatili huo dhidi ya rai ana imetoa wito wa kutaka eneo hilo liweze kufikika sambamba na manusura wapatiwe msaada wa dharura wa kibinadamu.

Halikadhalika Bwana Dujarric amenukuu MONUSCO ikikaribisha uamuzi wa mamlaka za DRC wa kuanzisha mchakato wa kisheria dhidi ya watekelezaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu nchini humo.

“Ujumbe huo unasalia tayari kuchangia katika juhudi hizo na kutoa wito kwa kukoma mara moja kwa ghasia na ukatili dhidi ya raia,” amesema Bwana Dujarric.

UN na kauli dhidi ya mashambulizi yanayofanywa na M23

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres kupitia taarifa mbalimbali amekuwa akilaani vurugu hizo akitaka sitisho la mapigano na mchakato wa mazungumzo upatiwa nafasi huku akipongeza wale wote wanaosimama kidete, ikiwemo harakati za kikanda na zile za Rais wa Angola.

Tarehe 22 mwezi uliopita wa Novemba, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walitoa taarifa ya kulaani vikali kurejea upya kwa mashambulizi yanayofanywa na waasi wa kikundi cha M23 huko jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kitendo cha waasi hao kuendelea kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa jimbo hilo, Goma na maeneo mengine.

Walitaka sitisho la mara moja la mashambulizi hayo, waasi hao wajisalimishe huku wakiunga mkono mchakato wa Nairobi unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC