Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau waanza kupatia wakimbizi DRC misaada; Walinda amani washambuliwa

Watoto wa familia za wakimbizi wa ndani wakipika katika kambi iliyoko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Watoto wa familia za wakimbizi wa ndani wakipika katika kambi iliyoko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

UN na wadau waanza kupatia wakimbizi DRC misaada; Walinda amani washambuliwa

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Umoja wa Mataifa na wahudumu wa kibinadamu wameanza kusambaza misaada kwa maelfu ya wakimbizi waliofurushwa makwao kufuatia mapigano yaliyodumu kwa takribni wiki mbili sasa kati ya jeshi la serikali, FARDC na waasi wa M23 kwenye jimbo la Kivu Kaskazini karibu na mpaka wa DRC na nchi za Uganda na Rwanda.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani wakati wa mkutano wake wa kila siku na wana tasnia hao, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema idadi kubwa ya wakimbizi hao wanatoka eneo la Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini na sasa wanaishi kwenye makazi ya muda katika shule, hospitali, kanisani na maeneo mengine, ijapokuwa idadi kubwa wanaishi na familia wenyeji zilizowapokea.

50,000 wanahitaji chakula

“Licha ya vikwazo lukuki, wahudumu wa kibinadamu wameanza kusaidia wakimbizi wa ndani kwenye eneo la Nyiragongo, wakiwapatia maji na huduma za afya. Washirika wetu pia wanasambaza chakula kwa watu 50,000,” amesema Bwana Dujarric.

Amefafanua kuwa zaidi ya watoto 180,000 wasio na wazazi au walezi wamebainika na sasa wanasaidiwa na wahudumu wa ulinzi wa mtoto, ilhali wengine 2,000 wamepatiwa usaidizi wa kisaikolojia.

Misaada zaidi yahitajika

“Mahitaji bado ni makubwa kuzidi kilichoko, hasa eneo la kusini la kanda ya afya ya Kayna kwenye eneo la Lubero ambalo tayari linahifadhi wakimbizi 50,000,” amefafanua msemaji huyo akiongeza kuwa mahitaij ya haraka zaidi kwa walionasa katikati ya uwanja wa mapigano ni maji, huduma za kujisafi, pamoja na vifaa muhimu vya majumbani, malazi, chakula, huduma za afya na ulinzi.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO unaendelea kupatia raia ulinzi kwa mujibu wa mamlaka yake, na unafanya kazi bega kwa bega na jeshi la serikali kukabiliana na waasi wa M23,  kundi lenye Watutsi wengi lililoundwa zamani kupigana dhidi ya wanamgambo wa kihutu miaka 10 iliyopita na sasa limeimarika tena pamoja na makundi mengine ya waasi ambayo yanashikilia maeneo kadhaa ya mashariki mwa DR Congo.

Walinda amani wamejipanga maeneo kadhaa

Msemaji huyo wa UN amesema katika kuimarisha ulinzi wa raia, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamejipanga kule kunakowezekana katika maeneo kadhaa yenye uhasama.

Kufuatia mashauriano na wadau wa kitaifa, MONUSCO imeondoa walinda amani wake kutoka kituo chake cha Rumangabo jimboni Kivu Kaskazini, eneo ambalo wanajeshi wa serikali hivi sasa hawako tena.

Katika ukurasa wake wa Twitter, MONUSCO imesema imechukua hatua hiyo ya kimbinu za medani ili kujiandaa kwa hatua zijazo pamoja na wadau wake wa kitaifa ili kusonga mbele na kudhibiti waasi wa M23, ambao jumamosi iliyopita walitwaa kitongoji cha Kiwanja jimboni Kivu Kaskazini.

Katika tukio hilo walinda amani wanne wa UN walijeruhiwa wakati wa operesheni za ulinzi.

Walinda amani washambuliwa

Bwana Dujarric ameripoti pia msafara wa walinda amani ulifurumushiwa mawe na kundi lenye uhasama katika kituo kimoja cha ukaguzi wa kijeshi karibu na kambi ya wakimbizi wa ndani, kilometa 8 kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma.

“Walinda amani wawili wamejeruhiwa, na angalau gari moja la MONUSCO limeteketezwa kwa moto. WAlinda amani walifyatua risasi hewani ili kutoa onyo na msafara upite kwa amani,” alisema Bwana Dujarric.

“Wenzetu wanatueleza kuwa ghasia na uharibifu wa vifaa unakwmaisha uwezo wa MONUSCO kutekeleza jukumu lake la kulinda rai ana kusaidia usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa jamii zilizo hatarini,” amesema Bwana Dujarric.