Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama DRC bado ni tete; Bi. Keita alijulisha Baraza la Usalama

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Morocco ambao walijeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya jeshi la serikali la DRC, FARDC na waasi wa M23 huko Kiwanja, Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini wakisafirishwa kwa matibabu zaidi.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Morocco ambao walijeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya jeshi la serikali la DRC, FARDC na waasi wa M23 huko Kiwanja, Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini wakisafirishwa kwa matibabu zaidi.

Hali ya usalama DRC bado ni tete; Bi. Keita alijulisha Baraza la Usalama

Amani na Usalama

Suala la usalama linasalia kuwa changamoto kubwa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC licha ya harakati zake za kujilinda, Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, Bintou Keita amesema hayo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

“Katika kipinid cha wiki kadhaa zilizopita, hali ya usalama mashariki mwa DRC imezorota kwa kiasi kikubwa,” amesema Bi. Keita ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UNn nchini humo, akiongeza kuwa tangu mwezi Oktoba mwaka huu, waasi wa kikundi cha M23 wamerejesha uhasama na wameendelea kupanua wigo wao kwenye jimbo la Kivu Kaskazini. 

Kuimarisha usaidizi 

Kwa kuzingatia changamoto hiyo, amesema MONUSCO inaendelea kutoa msaada wa vifaa, ufundi kwa jeshi la serikali, FARDC pamoja na polisi wa kitaifa wakati huu wanakabiliana na M23 na makundi mengine ya waasi. 

Mathalani doria za kina zinafanyika kwenye mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma pamoja na viunga vyake ili kulinda raia na kufurumusha M23 ili wasiendelee kusonga kuingia mjini. 

Halikadhalika, MONUSCO imeongeza mitandao ya kutoa tahadhari katika maeneo yaliyo hatarini zaidi. 

Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
MONUSCO/Sylvain Liechti
Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Uhalifu wa kikatili 

Mkuu huyo wa MONUSCO ameelezea kuhusu madai ya vitendo vya kutisha vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na wapiganaji wa M23 kwenye maeneo ya Kishishe na Bambo kwenye mji wa Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini ambapo takribani wanaume 102, wanawake 17 na watoto 12 waliuawa kwa kupigwa risasi au mapanga. 

Na wakati huo huo, M23 wamebaka wanawake wapatao 22, wameharibu shule nne na wametwaa shule mbili. 

“Natoa wito kwa Baraza hili la Usalama lilaani vitendo hivi kwa kauli kali na nataka kuachiwa haraka kwa manusura ambao wanazuiwa na M23 kuondoka kwenye maeneo hayo,” amesema Bi. Keita. 

Ameongeza kuwa wale wahusika wa vitendo hivyo na ukatili mwingine dhidi ya raia lazima wafikishwe mahakamani ya kitaifa au kimataifa,” amesema “Those responsible for these and other atrocities against the civilian population must be prosecuted nationally or internationally”.  

Uhalifu unaathiri operesheni za UN  

Kudorosa kwa usalama pia kunahatarisha operesheni za MONUSCO. 

Bi. Keita amerejelea tukio la shambulio kwenye kituo cha ujumbe huo cha MInembwe jimboni Kivu Kaskazini, tukio ambalo lilisababisha kifo cha mlinda amani mmoja. 

“Nalaani shambulio hili, na watekelezaji wake lazima wafunguliwe mashataka,” amesema Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC. 

Mwanamke mkimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, akiwa kambini Kanyaruchinya baada ya kukimbia makazi  yake kutokanana mapigano kati ya jeshi la serikali, FARDC na waasi wa M23
UN
Mwanamke mkimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, akiwa kambini Kanyaruchinya baada ya kukimbia makazi yake kutokanana mapigano kati ya jeshi la serikali, FARDC na waasi wa M23

Janga la kibinadamu linaloendelea 

Bi. Keita amesema uwepo wa vikundi vilivyojihami nchini DRC umefanya taifa hilo kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani barani Afrika. 

Takribani watu wengine 370,000 wamefurushwa makwao katika awamu ya hivi karibuni zaidi ya  mashambulizi kutoka M23 na mapigano ya kikabilia kwenye majimbo ya magharibi yamechochea ukimbizi wa watu zaidi ya 50,000 wengi wao wanawake na watoto. 

“Katika mazingira haya yatarini, licha ya vikwazo vyote vilivyoko, wahudumu wa kibinadamu wanaendelea kutoa misaada ya muhimu ya kuokoa maisha,” amesema Bi. Keita akisihi wadau waendelee kusaidia ombi la kufanikisha operesheni za kibinadamu halikadhalika hatua kwa ajili ya jimbo la Kivu Kaskazini. 

Mchakato wa kidiplomasia  

Afisa mwandamizi huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa pia kuhusu michakato ya amani ya kikanda kwa ajiil ya DRC ikiwemo mpango wa Luanda na ule wa Nairobi. 

“Tangu mwezi Aprili mwaka 2022, MONUSCO imepatia msaada wa kiufundi, vifaa na kisiasa, sekretarieti ya pamoja ya DRC na Kenya ili kufanya mashauriano kati ya serikali ya DRC na vikundi vilivyojihami. 

Kujiimarisha kidijitali 

Mapema akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Mwakilishi huyo Maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amesema wamechukua hatua kuimarisha uwepo wao kwenye majukwaa ya mtandaoni ili kukabiliana na kauli za chuki na za uhasama sambamba na taarifa potofu na za uongo dhidi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO. 

Bi. Keita amesema wamechukua hatua hiyo kwa kuwa kauli hizo za chuki na taarifa potofu na za uongo zimekuwa na madhara makubwa ikiwemo mauaji ya walinda amani pamoja na raia.