Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wasikitishwa sana na kuibuka tena kwa mapigano DRC

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Morocco ambao walijeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya jeshi la serikali la DRC, FARDC na waasi wa M23 huko Kiwanja, Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini wakisafirishwa kwa matibabu zaidi.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Morocco ambao walijeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya jeshi la serikali la DRC, FARDC na waasi wa M23 huko Kiwanja, Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini wakisafirishwa kwa matibabu zaidi.

Umoja wa Mataifa wasikitishwa sana na kuibuka tena kwa mapigano DRC

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesikitishwa sana na kuibuka tena kwa mapigano tangu tarehe 20 Oktoba,2022 kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, FARDC na kundi la wapiganaji waasi la M23 ambayo yamesababisha vifo vya raia, kusababisha watu kuyakimbia makazi yao na kujeruhiwa kwa walinda amani wanne wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Katibu Mkuu Stephen Dujarric kutoka New York Marekani hapo jana jumapili Oktoba 30, katibu Mkuu amefanya mazungumzo na wakuu wa nchi mbalimbali zinazohusika katika kutafuta suluhu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC.”

“Katibu Mkuu Guterres amezungumza na Rais wa Angola, João Lourenço, Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Kenya, William Ruto na Rais wa Senegal, Macky Sall, katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika, AU. Katibu Mkuu alitoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja na akasisitiza kuwa Umoja wa Mataifa una unga mkono upatanishi unaoongozwa na Rais wa Angola, João Lourenço, na mchakato wa Nairobi chini ya unaoongozwa na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta.”

Dujarric ameongeza kuwa “Katibu Mkuu anahimiza kikundi cha M23 na makundi mengine yenye silaha kusitisha mara moja uhasama na kushusha silaha bila masharti.

MONUSCO ipo tayari kujibu mashambulizi kwa uchokozi mpya utakaofanywa na M23

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO tarehe 29 mwezi huu wa Oktoba, walinda amani wake wanne kutoka Morocco wamejeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya jeshi la serikali FARDC na waasi wa M23 kutoka katika eneo la Kiwanja, Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini.

Taarifa ya MONUSCO imeelezea mashambulizi hayo yanayowalenga walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita na kwamba haitabakisha juhudi zozote kuwashtaki waliohusika mbele ya mahakama za kitaifa na/au kimataifa.

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umelaani vikali vitendo vya uhasama vinavyofanywa na M23 na madhara makubwa wanayosababisha kwa raia na kutoa wito kwa kundi hili la waasi kusitisha mara moja uhasama wote na kuonya kuwa upo tayari kujibu mashambulizii kwa nguvu katika tukio la uchokozi jipya litakalotelekezwa katika kambi zake.

MONUSCO pia imeeleza itaendelea kuwa na mshikamano na wakazi wa mji wa Rutshuru huko jimboni Kivu Kaskazini ambako kumeharibiwa na matukio haya ya kutisha ya mapigano na imethibitisha azma yake ya kuwalinda raia wa Kongo na kuwaunga mkono katika kutafuta amani na usalama.

Mapigano yafurusha maelfu makwao, wengine wakimbilia Uganda

Mchana wa leo jumatatu, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaeleza waandishi wa habari jijini New York, Marekan ikuwa mapigano ya takribani siku 11 sasa kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali ya DRC, yamesababisha watu 50,000 wakiwemo wanawake, wanaume na watoto kukimbia makazi yao.

Amesema miongoni mwao hao 12,000 wamevuka mpaka na kuingia nchini Uganda ili kusaka usalama zaidi.

Bwana Dujarric amesema huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, kumefanyika maandamano jana na leo karibu na mpaka na Rwanda, maandamano ambayo yaliitishwa na wanachama wa mashirika ya kiraia.