Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marynsia Mangu: Kijana aliyedhamiria kujenga utamaduni wa watoto kusoma vitabu

Marynsia Mangu - Mwanzilishi wa taasisi ya Mikono yenye mafanikio
UN News/ Assumpta Massoi
Marynsia Mangu - Mwanzilishi wa taasisi ya Mikono yenye mafanikio

Marynsia Mangu: Kijana aliyedhamiria kujenga utamaduni wa watoto kusoma vitabu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Lengo namba nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa linazungumzia Elimu na linataka jamii kuhakikisha kuna elimu bora, jumishi na inayolingana na kukuza fursa za kujifunza maishani kwa wote.

Namna moja wapo ya kujifunza ni kusoma vitabu ambavyo vina maarifa lukuki vilivyoandikwa na watu mbalimbali duniani.

Msichana Marynsia Mangu ni mmoja ya watu wanaopenda kusoma vitabu ambayo anasema alianza tangu utotoni na baba yake ndio alimfundisha tabia hiyo. Kwakutambua umuhimu na maarifa yanayopatikana kwenye vitabu alikuwa akiwashawishi marafiki zake kusoma vitabu hivyo.

Lakini baada ya jitihada zake za kuwashawishi marafiki zake kusoma vitabu kushindwa kuzaa matunda akaamua kufuata usemi wa Kiswahili usemao Samaki mkunje angali mbichi na kuanzisha shirika la success Hands au kwa lugha ya Kiswahili Mikono yenye Mafanikio nchini Tanzania ambalo jukumu lake ni kuwajengea watoto tabia yakupenda kusoma vitabu tangu wangali tumboni mwa mama zao.

“Mimi nililelewa na baba na alikuwa anapenda nisome vitabu sasa nilivyoshindwa kuwashawishi marafiki zangu watu wazima wasome vitabu nikaamua kuanzisha shirika hili ili niwasaidie watoto kujenga tabia hiyo. Lengo ni hili lilifanikiwa kwa kuwawezesha zaidi ya watoto 60,000 ambao walikuwa wanakutana kila jumapili na wanasoma vitabu.”

Leah Mushi (Kushoto) akifanya mahojiano na Marynsia Mangu wa Mwanzilishi wa Taasisi ya Mikono yenye Mafanikio
UN News/ Assumpta Massoi
Leah Mushi (Kushoto) akifanya mahojiano na Marynsia Mangu wa Mwanzilishi wa Taasisi ya Mikono yenye Mafanikio

COVID-19 yambadilisha

Hali ya watoto kukutana na kusoma kila jumapili ilishindikana kuendelea baada ya dunia kukumbwa na janga la COVID-19

“Baada ya CORONA hatukuweza kukutana na watoto hawa na ndio akili zetu zikaanga kuchangamka tukaona namna bora ya kuwasaidia watoto ni kujenga maeneo kwa ajili ya watoto kujifunza ambazo zitasaidia si kusoma vitabu tu katika maktaba bali pia kuwa na sehemu za michezo kwa watoto.”

Taasisi yake pia inalenga watoto walio tumboni kuanzia miezi mitano.

“Tutakuwa na maeneo ambapo wazazi watakuja watakaa na kuanza kuwasomea watoto wao walio tumboni, hii inasaidia watoto hata wakizaliwa kuendelea kusomewa vitabu mpaka hapo wakiwa wakubwa wanatapoweza kusoma wenyewe.”

Mwanzilishi huyu wa taasisi ya Mikono yenye Mafanikio anasema kwa miaka mitano ya kwanza watafanya kazi na kujenga maeneo hayo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dododoma na Mbeya huku lengo la muda mrefu ni kufikia nchi nzima ya Tanzania. Hata hivyo kwa sasa wanasubiri serikali iwapatie maeneo ya kuweza kujenga vituo hivyo.

Wazazi na walengo wa watoto nao waeleza

Miongoni mwa wanufaika wa watoto wao kusoma vitabu ni Linda Lucas ambaye anasema “Programu hii ya kujengea watoto kusoma vitabu imemsaidia sana mtoto wangu na imembadilisha, mara ya kwanza alikuwa anapenda kucheza na simu lakini kwa sasa anapenda kusoma vitabu. Pia hata ameongeza kujiamini.”

Mwingine ni Stella Godfrey mkazi wa Arusha ambaye anasema mdogo wake anayemlea baada ya kuanza kuhudhuria kila jumapili amebadilika. “Ameimarisha sana kwenye matokeo yake ya darasani na kila siku amezidi kuwa bora hii imekuja sababu ya kusoma vitabu.”

Marynsia Mangu ametoa ushauri kwa wazazi na walezi kuendelea kuwajengea watoto taratibu tabia ya kupenda kusoma vitabu ili waweze kutimiza lengo namba 4 la SDGs na wazidi kupata maarifa zaidi.