Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kuzuia na matibabu ya VVU kwa watoto, vijana, na wanawake wajawazito zimepungua:UNICEF

Kituo kimoja cha afya nchini Uganda kinapatia elimu wanawake ili waweze kujifungua bila kuambukiza watoto wao VVU
© UNICEF
Kituo kimoja cha afya nchini Uganda kinapatia elimu wanawake ili waweze kujifungua bila kuambukiza watoto wao VVU

Juhudi za kuzuia na matibabu ya VVU kwa watoto, vijana, na wanawake wajawazito zimepungua:UNICEF

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limeonya kuwa maendeleo ya kuzuia na matibabu ya VVU kwa Watoto, vijana barubaru na wanawake wajawazito yamepungua sana katika miaka kadhaa iliyopita na kupungua huko kusiko na kifani kumekuja wakati kuna pengo linaloongezeka  katika upande wa matibabu miongoni mwa watoto na watu wazima.  

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani imesema “Takriban watoto na vijana 110,000  wa umri wa miaka 0-19 walikufa kutokana na sababu zinazohusiana na Ukimwi mwaka 2021” Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya UNICEF   inayotoa taswira mpya ya kimataifa kuhusu watoto, VVU na ukimwi. Wakati huo huo, shirika hilo limesema wengine 310,000 walipata maambukizi mapya na kufanya jumla ya vijana wanaoishi na VVU kufikia milioni 2.7. 

Kuelekea siku ya ukimwi duniani UNICEF inaonya kwamba “maendeleo katika kuzuia na matibabu ya VVU kwa watoto, vijana, na wanawake wajawazito yamekaribia kudumaa kabisa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, huku kanda nyingi bado haijafikia huduma za kabla ya janga la COVID-19 huku pengo la matibabu likiongezeka baina ya watoto na watu wazima.” 

Hali inayoshuhudiwa si ya kawaida 

Kwa mujibu wa Anurita Bains mkuu msaidizi wa UNICEF kuhusu masuiala ya  VVU na UKIMWI "Ingawa watoto kwa muda mrefu wamesalia nyuma ya watu wazima katika hatua za kupambana na ukiwmi, Hali ya kudumaa kwa hatua iliyoonekana katika miaka mitatu iliyopita si jambo la kawaida, na kuweka maisha ya vijana wengi katika hatari ya magonjwa na vifo. Watoto wanaathirika vibaya kwa sababu kwa pamoja tunashindwa kuwapata na kuwapima na kuwapatia matibabu ya kuokoa maisha. Kila siku inayopita bila maendeleo, zaidi ya watoto na vijana 300 hupoteza vita yvao dhidi ya ukiwmi.” 

Licha ya kuchangia asilimia 7 pekee ya watu wote wanaoishi na VVU, watoto na vijana walijumuisha asilimia 17 ya vifo vyote vilivyohusiana na ukwimi na asilimia 21 ya maambukizo mapya ya VVU mwaka 2021.  

Bila kushughulikia vichochezi vya ukosefu wa usawa, UNICEF inaonya kwamba “kukomesha ukimwi miongoni mwa watoto na vijana itaendelea kuwa ndoto ya mbali.” 

Bado kuna matumaini katika vita dhidi ya VVU 

Hata hivyo ripoti hiyo ya UNICEF inaonyesha kuwa mwelekeo wa muda mrefu unabaki kuwa mzuri.  

Maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto wadogo  wa umri wa miaka 0-14 yalipungua kwa asilimia 52 kati ya mwaka 2010 hadi 2021, na maambukizi mapya kati ya vijana barubaru wa umri wa miaka 15-19 pia yalipungua kwa asilimia 40.  

Vile vile, matibabu ya kurefusha maisha ya ART miongoni mwa wanawake wajawazito wanaoishi na VVU iliongezeka kutoka asilimia 46 hadi asilimia 81 katika muongo mmoja uliopita. 

Mama na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, wote wana VVU, wanatembelea kliniki ya afya huko Mubende, Uganda.
© UNICEF/Karin Schermbrucke
Mama na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, wote wana VVU, wanatembelea kliniki ya afya huko Mubende, Uganda.

Wakati jumla ya idadi ya watoto wanaoishi na VVU inapungua, UNICEF imesema pengo la matibabu kati ya watoto na watu wazima linaendelea kukua.  

Katika nchi zinazopewa kipaumbele na UNICEF katika masuala ya ukimwi, huduma ya ART kwa watoto ilifikia asilimia 56 mwaka 2020 lakini ilishuka hadi asilimia 54 mwaka 2021.  

Kupungua huku ripoti inasema kunatokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na janga la COVID-19 na majanga mengine ya kimataifa, ambayo yameongeza unyanyapaa na umaskini, lakini pia ni taswira ya utashi wa kisiasa unaofifia na hatua za kukabiliana na ukimwi kwa watoto.  

Ulimwenguni kote , asilimia ndogo ya watoto wanaoishi na VVU walipata matibabu ambayo ni asilimia 52%, ambayo imeongezeka kidogo  sana katika miaka michache iliyopita. 

Watu wazima wanapata huduma zaidi kuliko watoto 

Wakati huo huo, ripoti imesema huduma miongoni mwa watu wazima wote wanaoishi na VVU ni asilimia 76% ambayo ni asilimia 20 zaidi ya huduma wanayopatiwa watoto.  

“Pengo lilikuwa kubwa zaidi kati ya watoto na wajawazito wanaoishi na VVU  ambalo ni asilimia 81%. Inashangaza kwamba, asilimia ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 0-4 wanaoishi na VVU na wasiotumia ART imekuwa ikiongezeka katika kipindi cha miaka saba iliyopita, na kupanda hadi asilimia 72 mwaka 2021, kama ilivyokuwa mwaka 2012.” Imeongeza ripoti hiyo. 

Pia imesema maeneo mengi ikiwemo Asia na Pasifiki, Caribbea, Mashariki na Kusini mwa Afrika, Amerika ya Kusini, Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini,  na Afrika Magharibi na Kati pia yalikumbwa na kupungua kwa huduma za matibabu kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha mwaka 2020, na upande wa Asia na Pasifiki, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini huduma zilizidi kupungua mwaka wa 2021.  

Kwa Afrika Magharibi na Kati, maambukizi ya mama kw amtoto yameshamiri

Kwa upande wa Afrika Magharibi na Kati, ripoti imesema inaendelea kuona mzigo mkubwa zaidi wa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, hakuna kanda yoyote kati ya zilizotajwa ambayo imerejea kwa viwango vya huduma za matibabu kama vilivyofikiwa mwaka wa 2019.  

Usumbufu huu UNICEF imesema huweka maisha ya watoto wachanga katika hatari kubwa.  

Mwaka 2021, zaidi ya maambukizo mapya 75,000 ya watoto yalitokea kwa sababu wajawazito hawakugunduliwa kuwa wameambukizwa na kuanza matibabu mapema. 

Bains amesema “Kwa dhamira mpya ya utashi wa kisiasa ya kufikia walio hatarini zaidi, ushirikiano wa kimkakati na rasilimali ili kuongeza programu, tunaweza kukomesha ukiwmi kwa watoto, vijana barubaru na wanawake wajawazito,"