Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa 73 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO waanza Gaborone, Botswana

Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.
UNICEF/Christine Nesbitt
Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.

Mkutano wa 73 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO waanza Gaborone, Botswana

Afya

Mkutano wa Sabini na tatu wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) umeanza hii leo katika mji mkuu wa Botswana, Gaborone huku tukio hilo likishuhudia pia Maabara ya Kitaifa ya Marejeleo ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ya Botswana ikipewa hadhi ya kuwa Kituo Kishiriki cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) cha kufuatilia Ubora. 

Mkutano huu utakaoendelea hadi tarehe Mosi ya mwezi ujao Septemba unawakutanisha Mawaziri wa afya wa Afrika na wawakilishi wa serikali pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya kutoka kote barani Afrika ili kujadili na kukubaliana kuhusu hatua muhimu za kushughulikia changamoto za afya za kanda ya Afrika, kuendeleza na kukuza afya bora na ustawi wa watu. 

Na kuhusu Maabara ya Kitaifa ya Botswana kuwa Kituo Kishiriki cha Ubora cha WHO, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus  akizungumza asubuhi ya leo ya Botswana baada ya yeye na Rais Dkt Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi wa Botswana kutia saini makubaliano amesema,"WHO inajivunia kuhesabu maabara hii kama Kituo cha Kushirikiana na inatarajia kufanya kazi pamoja kwa karibu zaidi katika kutoa msaada na huduma zinazohitajika kwa watu wanaoishi na VVU." 

Kwa upande wake Rais Masisi wa Botswana amesema kuteuliwa kwa maabara hii kama Kituo Kishiriki cha Ubora cha WHO kunaipa nchi ya Botswana imani kwamba wako kwenye njia sahihi ya kufikia lengo la WHO la mwaka 2030 la kudhibiti Virusi Vya Ukimwi (VVU).  

Wengine walioko nchini Botswana kuhudhuria Mkutano huo unaofanyika kwa njia ya ana kwa ana na mtandaoni ni Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti ambaye kabla ya kuhitimishwa kwa mkutano huu, anatarajiwa kutoa taarifa kuhusu hali ya afya barani Afrika.