Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban nusu ya watoto wenye UKIMWI hawapati matibabu

Mama na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, wote wana VVU, wanatembelea kliniki ya afya huko Mubende, Uganda.
© UNICEF/Karin Schermbrucke
Mama na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, wote wana VVU, wanatembelea kliniki ya afya huko Mubende, Uganda.

Takriban nusu ya watoto wenye UKIMWI hawapati matibabu

Afya

Wakati zaidi ya robo tatu ya watu wazima wote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI VVU wanapata aina fulani ya matibabu, idadi ya watoto wanaofanya hivyo, inafikia asilimia 52 pekee. 

Katika kukabiliana na tofauti hii ya kushangaza, mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa kwakushirikiana na wadau wengine wameunda ubia wa kimataifa ili kuzuia maambukizi mapya ya VVU na kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 watoto wote walio na VVU wanawezakupata matibabu ya kuokoa maisha. 

Taarifa iliyotolewa leo katika miji ya Montreal Canada, Geneva Uswisi na New York, Marekani imeyataja mashirika hayo kuwa ni lile linashughulika na masuala ya UKIWMI UNAIDS,linaloshughulika na watoto UNICEF na lile la afya ulimwenguni WHO ambao kwa pamoja wanashirikiana na mashirika mengine ya kimataifa, asasi za kiraia na serikali.

Ubia huo umetangazwa katika Mkutano wa kihistoria wa Kimataifa wa UKIMWI, ambao unafikia tamati huko Montréal, Canada, hii leo na kutaja nchi 12 zilizojiunga na muungano huo katika awamu ya kwanza kuwa ni Angola, Cameroon, Côte d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Msumbiji, Nigeria, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

“Hakuna mtoto anayepaswa kuzaliwa na VVU au kukua na VVU, na hakuna mtoto aliye na VVU anayepaswa kutopata matibabu” amesema DkT. Tedros Adhanom Gheberyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO na kuongeza kuwa “Ni ukweli kwamba nusu tu ya watoto wenye VVU wanapokea dawa za kurefusha maisha, hii ni kashfa na doa katika dhamiri zetu za pamoja. Ubia wa Kimataifa wa Kutokomeza UKIMWI kwa Watoto ni fursa ya kufanya upya ahadi yetu kwa watoto na familia zao kuungana, kuzungumza na kutenda kwa nia na mshikamano na akina mama wote, watoto na vijana”

Wazazi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, vvu wakiwa katika kliniki yao ya kuwapatia usaidizi wilayani Kamuli nchini Uganda.
© UNICEF/Jimmy Adriko
Wazazi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, vvu wakiwa katika kliniki yao ya kuwapatia usaidizi wilayani Kamuli nchini Uganda.

Nguzo nne zakuchukua hatua

Kwa pamoja, wadau katika muungano wamebainisha nguzo nne za hatua ya pamoja ambazo ni 
1.    Kuziba pengo la matibabu kati ya wasichana wanaonyonyesha na wanawake wanaoishi na VVU na kuongeza kuhamasisha watu kuwa na muendelezo wa matibabu.
2.    Kuzuia na kugundua maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa wasichana na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.
3.    Kukuza ufukiwaji wa upimaji, matibabu yaliyoboreshwa, na utunzaji wa kina kwa watoto wachanga, watoto na vijana walio katika hatari ya kuambukizwa na wanaoishi na VVU.
4.    Kushughulikia usawa wa kijinsia, na vikwazo vya kijamii na kimuundo vinavyozuia upatikanaji wa huduma.

Mafanikio yanayowezekana kufikiwa na ubia huu yatategemea hali inayowaunganisha. 
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima anasema kuwa, "kwa kuleta pamoja dawa mpya zilizoboreshwa, utashi mpya wa kisiasa, na harakati zenye dhamira ya dhati kuilenga jamii, tunaweza kuwa kizazi kinachomaliza UKIMWI kwa watoto. Tunaweza kushinda hili  lakini tunaweza tu kushinda pamoja.”

Ni kwa ushirikiano katika ngazi zote za jamii, ndipo suluhu kamili zinaweza kuundwa ili kuzuia maambukizi zaidi ya VVU, ilisema mkuu huyo wa UNAIDS.

Kwa kuleta suluhu zenye kuzingatia kutoa majawabu yanayoendana na wananchi wa mashinani huku tukihamasisha kujitolea na upatikajai wa rasilimali duniani kote, muungano huu unalenga kuchochea uvumbuzi na kuboresha ubora wa kiufundi unaohitajika kutatua suala hili muhimu.

Daktari akipima mtoto kama ana VVU nchini Ukraine.(Maktaba)
© World Bank/Yuri Mechitov
Daktari akipima mtoto kama ana VVU nchini Ukraine.(Maktaba)

Mfano bora kutoka Lesotho 

Akihutubia mkutano huo, Limpho Nteko kutoka nchini Lesotho alisimulia safari yake toka alipopata taarifa za kushangaza kuwa na maambukizi ya VVU hadi kuanzisha mpango unaoongozw ana wakina mama uitwao mama kwa mama “Mothers2mothers” ili kukabiliana na maambukizi ya VVU wakati wa ujauzito. Akiwa mjamzito alipogundulika, Nteko alisisitiza umuhimu wa uongozi katika ngazi ya jamii katika mapambano dhidi ya VVU.

“Ili kufanikiwa, tunahitaji kizazi chenye afya na maarifa cha vijana ambao wanajisikia huru kuzungumza kuhusu VVU, na kupata huduma na usaidizi wanaohitaji kujikinga wao na watoto wao dhidi ya VVU”, aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano huko Canada.

Aliongeza kuwa “Mothers2mothers imefanikisha kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa wateja wetu waliojiandikisha kwa miaka minane mfululizo hii inaonyesha kile kinachowezekana tunapowaruhusu wanawake na jamii kuunda suluhu zinazolingana na hali halisi yao.”

Netko alitoa msisitizo kuhusu uongozi wa jamii kuungwa mkono na kupatiwa rasilimali kutoka kwenye  muungano wa kimataifa.

Mkutano wa Afrika 

Katika mkutano huo, Waziri wa Afya wa Nigeria Dkt. Osagie Ehanire, aliahidi “kubadilisha maisha ya watoto walioachwa” kwa kuweka mifumo inayohitajika ili kuhakikisha kuwa huduma za afya zinakidhi mahitaji ya watoto wanaoishi na VVU.

Nchi ya Nigeria itakuwa mwenyeji wa uzinduzi wa kisiasa wa muungano huo barani Afrika katika mkutano wa Mawaziri mnamo Oktoba mwaka huu 2022.