Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii zipatiwe uwezo ili zifanikishe kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030- UNAIDS

Grace Amodu, alitambua kuwa ana VVU alipokuwa na umri wa miaka 7. Sasa ana watoto wawili na wote hawana maambukizi ya VVU kutokana na huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, PMTCT.
UNAIDS Nigeria
Grace Amodu, alitambua kuwa ana VVU alipokuwa na umri wa miaka 7. Sasa ana watoto wawili na wote hawana maambukizi ya VVU kutokana na huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, PMTCT.

Jamii zipatiwe uwezo ili zifanikishe kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030- UNAIDS

Afya

Kuelekea siku ya Ukimwi duniani tarehe 1 mwezi ujao wa Desemba, UNAIDS ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la kukabili Ukimwi linasihi serikali kote duniani kutumia ipasavyo nguvu ya jamii mashinani ili hatimaye kutokomeza ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2030. 

Ripoti mpya ya UNAIDS iliyotolewa leo ikipatiwa jina Achia Jamii Ziongoze, inaonesha kuwa Ukimwi unaweza kuwa sio tena tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030 iwapo tu jamii zilizo kwenye mstari wa mbele wa kutokomeza ugonjwa huo zitapata msaada ambao zinahitaji kutoka serikalini na kwa wahisani. 

Jamii ziko tayari kuongoza, mamlaka zinaweka vikwazo 

“Jamii duniani kote zimeonesha ziko tayari, na zina utashi na uwezo wa kuonesha njia. Lakini zinataka vikwazo vya kutekelea kazi hiyo viondolewe, na zinahitaji rasilimali sahihi,” amesema Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS kupitia taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo Geneva, USwisi na London, Uingereza. 

Amesema mara nyingi wapitisha maamuzi na watunga sera huchukulia jamii kama matatizo ya kudhibitiwa, badala ya kutambuliwa na kuchukuliwa kama viongozi wanaohitaji kupatiwa msaada. 

“Jamii si vizuizi bali ni zinaangazia njia ya kutokomeza Ukimwi’” amesema Bi. Byanyima. 

Ripoti hiyo imezinduliwa London, nchini Uingereza wakati wa tukio la Siku ya Ukimwi lililoandaliw ana shirika la kiraia la STOPAIDS, na ripoti hiyo inaonesha ni kwa jinsi gani jamii zimekuwa kichocheo cha maendeleo yaliyopatikana sasa katika kutokomeza Ukimwi. 

Mifano ya uchechemuzi kutoka kwenye jamii 

Kuna uchechemuzi wa jamii kuanzia mitaani hadi vyumba vya mahakama, hadi Bungeni na hatua hizo kwa mujibu wa UNAIDS zimesaidia kuleta mabadiliko makubwa ya kisera. 

Kampeni za jamii zimesaidia kufungua upatikanaji wa dawa za bei nafuu za kupunguza makali ya Ukimwi kwani kampuni zimelegeza masharti ya hataza. 

Kwa kufanya hivyo gharama ya bei ya dawa imepungua kutoka dola 25,000 kwa mtu mmoja kwa mwaka mwaka 1995 hadi chini yad ola 70 kwa mwaka leo hii. 

Ripoti inaonesha kuwa kuwekeza kwenye miradi ya kijamii ya kukabili Virusi Vya  Ukimwi, VVU inaleta manufaa yenye mabadiliko makubwa chanya. 

Mathalani nchini Nigeria, kampeni za kijamii zimeongeza ufikiaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU kwa asilimia 64 na kuongeza maradufu uwezo wa kinga dhidi ya VVU. 

Azimio la kisiasa 2021 

Azimio la kisiasa la mwaka 2021 kuhusu kutokomeza Ukimwi , lililopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa lilitambua nafasi muhimu ya jamii katika utoaji wa huduma za kupambana na VVU, hasa kwa watu walio hatarini kuambukizwa UKIMWI. 

Kila dakika, mtu mmoja anakufa kutokana na Ukimwi. Kila wiki wasichana na wanawake vijana wanaambukizwa VVU, na kati ya watu milioni 39 wanaoishi na VVU, milioni 9.2 hawana uwezo wa kufikia matibabu ya kuokoa maisha yao. 

UNAIDS inasema kuna njia ya kumaliza UKIMWI na UKIMWI unaweza kutokomeza ifikapo mwaka 2030 pale tu jamii zitakaposhika hatamu ya vita dhidi ya ugonjwa huo. 

Soma ripoti nzima hapa