Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti yabainisha vitendo dhalili na mateso Malawi, Uganda na Somalia

Waandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mateso wakihutubia waandishi wa habari..
UN Photo/Rick Bajornas
Waandishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mateso wakihutubia waandishi wa habari..

Ripoti yabainisha vitendo dhalili na mateso Malawi, Uganda na Somalia

Haki za binadamu

Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utesaji, CAT imetoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa haki za binadamu katika mataifa 6 yakiwemo Malawi, Somalia na Uganda kwa mujibu wa Mkataba wa kimataifa dhidi ya utesaji na ukatili na vitendo vingine dhalili na adhabu kwa binadamu. 

Ripoti hiyo imetolewa leo huko Geneva, Uswisi na jopo la wajumbe wa kamati hiyo yenye wajumbe 10, kamati ambayo jukumu lake ni kuchunugza ripoti za utesaji kwa lengo la kukomesha na kuzuia uhalifu huo. 

Malawi: Mlundikano wa wafungwa ni zaidi ya 200% 

Mathalani kuhusu Malawi, ripoti inamulika mlundikano kupindukia kwa wafungwa magerezani ambako mlundikano umezidi asilimia 200 ya uwezo, huku mazingira yakiwa ni mabaya. 

Kamati imeitaka Malawi ihakikishe mazingira ya magerezani yanazingatia viwango vya Umoja wa Mataifa na ichukue hatua muhimu za kisheria kupunguza mlundikano magerezani kwa kutumia mbinu mbadala za kusweka watu korokoroni. 

Kamati pia imeishutumu Malawi kwa kushindwa kuzuia kitendo cha kutesa wafungwa ili wakiri makosa, kitendo kilichomo kwenye sheria na taratibu za utoaji ushahidi. 

Malawi badilisha sheria husika na hakikisha ushahidi uliopatikana kwa njia hiyo unafutwa. Serikali pia iandae mwongozo wa mafunzo kwa maafisa wa polisi kuhusu mbinu za kuhoji bila kutesa,” imesema ripoti hiyo. 

Somalia: Usalama wa Taifa na utesaji watuhumiwa 

Kwa upande wa Somalia, kamati imesikitishwa na ripoti kuhusu mateso na vitendo dhalili ikiwemo ukatili wa kijinsia vinavyofanywa na Ofisi ya Usalama wa TAifa, jeshi la Somalia na vikundi vingine vya kiserikali na visivyo vya kiserikali. 

Halikadhalika kamati imegundua pia vitendo vya kunyonga watu hadharani nchini Somalia vinaibua hoja nzito kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Mateso. 

Imetaka Somalia ianzishe ainisho sahihi kuhusu mateso kwa mujibu wa Mkataba huo na ianzishe haraka taasisi ya kitaifa kuhusu haki za binadamu na ihakikishe kuwa madai yoyote ya mateso na vitendo dhalili vinachunguzwa bila kuegemea upande wowote. 

Uganda: Maeneo yasiyotambulika ya ushikiliaji watuhumiwa  

Kamati pia imetoa matokeo ya uchunguzi wake nchini Uganda ikimulika ripoti za vikosi vya usalama nchini humo kutumia nguvu kupita kiasi na vurugu kwa minajili ya kukabili ugonjwa wa coronavirus">COVID-19. 

Kamati imesihi Uganda kuchunguza kwa kina na bila upendeleo wowote madai ya kufanyika kwa vitendo hivyo haraka iwezekanavyo na uchunguzi huo ufanywe na chombo huru. 

Kamati bado inasalia na wasiwasi wake kuhusu ripoti ya kuweko kwa ‘nyumba salama’ au maeneo yasiyotambulika rasmi ya kushikilia watu nchini Uganda. 

Imetaka serikali kufunga nyumba hizo na itoe taarifa kuhusu maeneo yote yanayotumika kushikilia watuhumiwa. 

Ripoti kamili unaweza kupata hapa.