Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muongozo mpya kuhusu haki za waomba hifadhi watolewa: UN

Wasaka hifadhi wapumzika katika kituo cha mapokeszi cha Debrecen.(Picha:UNHCR/Béla Szandelszky)

Muongozo mpya kuhusu haki za waomba hifadhi watolewa: UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya utesaji (CAT) leo imetoa muongozo mpya kuhusu haki za waomba hifadhi.

Muongozo huo una lengo la kuzisaidia serikali kuepuka ukiukaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuwasaidia wasaka hifadhi kukwepa mateso au manyanyaso.

Kwa mujibu wa CAT muongozo huo uutwao “Maoni ya jumla” unalenga serikali mbalimbali katika utekelezaji wa kifungu nambari 3 cha mkataba dhidi ya utesaji.

Kifungu hiki kinahusika na masuala yasiyo ya kukatazwa, kupiga marufuku kufukuza mtu, kumrudisha au kumuhamishia kwenye nchi nyingine ambako anaweza kuteswa.

Kupitia muongozo huo unaozitaka serikali kutimiza wajibu wao wa kimataifa, kamati hiyo itakuwa ndio kiongozi wa kuzishauri serikali cha kufanya na maoni ya jumla ndiyo yatakayotathimini endapo msaka hifadhi yuko katika hatari ya kuteswa au kunyanyaswa katika nchi yake, endapo atarejeshwa.

Kwa mujibu wa Jens Modving mwenyekiti wa kamati hiyo, muongozo huo pia unatoa orodha ya masuala muhimu na vyanzo vya hatari ambavyo serikali zinapaswa kuvitilia maanani na pia itawasaidia watu walio katika hatari wakirejeshwa kuwasilisha madai yao kwa serikali.

Orodha hiyo mbali ya masuala mengine inaziomba serikali kuzingatia kwamba waathirika wa utesaji na makundi mengine yasiyojiweza mara nyingi hukabiliwa na matatizo ya msongo wa mawazo aina ya (PTSD) ambao husababisha athari nyingine kadhaa ikiwemo watu kujitenga, kutojieleza vyama na hata kuwa na fikra mbaya za kutaka kujiua.