Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wengi wauawa na mashambulizi ya Al Shabaab, Somalia- Kamishna Mkuu Türk

Magari  yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.
UN /Stuart Price
Magari yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.

Raia wengi wauawa na mashambulizi ya Al Shabaab, Somalia- Kamishna Mkuu Türk

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk amezieleza pande zote zilizo kwenye mzozo nchini Somalia lazima zitekeleze wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kuhakikisha kuwa raia wanalindwa.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu, OHCHR, jijini Geneva Uswisi imeeleza kuwa Kamishna Turk amesema ujumbe wake unalenga pande zote wale wenye silaha na wanashiriki kwenye mapigano, Serikali katika vita dhidi ya Al-Shabaab, pamoja na vikosi vya kimataifa.

"Ninatoa wito kwa Serikali ya Somalia kuchukua hatua zote zinazohitajika na kwakushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuimarisha ulinzi wa raia, kulingana na kanuni na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu," amesema Kamishna Mkuu.

Mauaji na majeruhi

Kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kumekuwa na ongezeko kubwa la vifo vya raia nchini Somalia, kutokana na mashambulizi mengi yanayotekelezwa na kundi la Al-Shabaab. Mashambulizi haya yanazidisha hali mbaya ya haki za binadamu na uhitaji wa kibinadamu unaowakabili wananchi wa Somalia.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, takriban raia 613 wameuawa na 948 kujeruhiwa tangu mwaka huu uanze (2022). Hii ni idadi kubwa zaidi tangu 2017 na zaidi ya asilimia 30 ikilinganishwa na takwimu za mwaka jana.

Vifaa vya kulipuka IEDs zilisababisha vifo vya watu 315 huku watu 686 wakijeruhiwa na asilimia 94 ya vifo na majeruhi hao waliohusishwa nai Al-Shabaab. Majeruhi wengine wamesababishwa na vikosi vya usalama vya Serikali, wanamgambo wa koo na wahusika wengine wasiojulikana.

Kwa ripoti hizi za vifo na majeruhi Türk amesema “Nina wasiwasi mkubwa kwamba Wasomali zaidi wanaendelea kupoteza maisha kila siku.”

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Somalia, majeruhi wengine wametokana na milipuko ya mabomu ya kujitoa muhanga ya Al-Shabaab ambayo ilitokea tarehe 29 Oktoba,2022 karibu na Wizara ya Elimu katika mji mkuu wa Mogadishu, na kusababisha takriban watu 121 kuuawa na 333 kujeruhiwa.

Wengi wa waliopoteza maisha walikuwa raia. Shambulizi la awali la Al-Shabaab lilitekelezwa kwenye Hoteli ya Hayat mjini Mogadishu mnamo tarehe 21 Agosti liliua takriban raia 22 na kujeruhi 30.

Al-shabaab waharibu miundombinu

Mbali na kuwalenga raia kimakusudi, taarifa za hivi punde zilizokusanywa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu zinaonesha kuwa katika miezi ya hivi karibuni Al-Shabaab wameharibu visima vingi na kutia sumu nyingine katika eneo la Hiraan, wakati ambapo Wasomali wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na ukame katika maeneo mengi ya nchi.

Al-Shabaab pia waliharibu sehemu ya ukingo wa mto wa Shabelle, nyumba, daraja, walikata antena za mawasiliano ya simu na shule 11.

Türk amesema kuwa “uharibifu kama huo wa kuchukiza ni wa kulaumiwa, hasa kutokana na hali ngumu ya kibinadamu, kwakuzingatia nchi hiyo inakabiliwa na mfululizo kwa misimu mitano ya mvua kushindwa kunyesha na watu wengi kuhama makazi yao nchini humo.”

Ameongeza kuwa “Kuwalenga raia kimakusudi na kuharibu miundombinu, kama hivyo, vitu muhimu kwa raia ni uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa. Lazima waache mara moja.”

Kamishna Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamuamesisitiza haja muhimu ya uwajibikaji kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu ambazo ni muhimu ili kuzuia kuendelea kuchochea mzunguko wa vurugu nchini Somalia.