Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alaani mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya na Somalia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
TASS/ UN DPI
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alaani mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya na Somalia.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo jijini New York amelaani vikali shambulizi lililotekelezwa jana katika kaunti ya Wajir nchini Kenya ambapo takribani askari polisi nane wameuawa na wengine kujeruhiwa wakati gari lao lilipolipuliwa kwa kilipuzi kilichoundwa kienyeji. 

Shambulizi hilo linakuja baada ya utekwaji wa maafisa polisi watatu wa Kenya katika kaunti hiyo hiyo ya Wajir, Ijumaa, tukio ambalo Al Shabaab wanadai kuhusika.

Aidha Katibu Mkuu Guterres aamelaani mauaji ya takribani watu nane na wengine kujeruhiwa katika shambulizi la bomu kwenye gari katika kizuizi cha barabarani mjini Mogadishu, Somalia, shambuliji jingine ambalo Al Shabaab wamedai kuhusika.

Guterres ameeleza kusikitishwa kwake na akatuma salamu za rambirambi kwa familia za wale waliouawa, serikali zote mbili na kwa watu wa Kenya na Somalia. Amewatakia kupona haraka wale waliojeruhiwa.

Katibu Mkuu Guterres pia ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa uko pamoja na serikali ya Kenya na Somalia katika juhudi za kupambana na ugaidi pamoja na vurugu za itikadi kali.