Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nalaani vikali shambulio la kigaidi Moghadishu:Guterres

Mwanamke akipita pembeni ya gari la wagonjwa ndani ya hospitali ya Benadir mjini Mogadishu, Somalia.
UN /Ilyas Ahmed
Mwanamke akipita pembeni ya gari la wagonjwa ndani ya hospitali ya Benadir mjini Mogadishu, Somalia.

Nalaani vikali shambulio la kigaidi Moghadishu:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea Alhamisi mjini Moghadishu nchini Somalia na kukatili maisha ya watu wengi.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia na jamaa wa walioathirika na shambulio hilo huku akiwatakia ahuweni ya haraka majeruhi. Pia amepongeza wahudumu wa huduma za dharura wa Somalia kwa kujitahidi kuokoa maisha ya watu na kufikisha huduma kwa wakati muafaka.

Kwa mujibu wa duru za habari vikosi vya usalama vya Somalia vimekuwa katika mapambano makali na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha ambao waliteka jengo moja na kujificha ndani mjini Mogadishu, saa kadhaa baada ya shambulio hilo la kujitoa muhanga lililotekelezwa kwenye gari katika eneo la mtaa wa pilikapilika nyingi na kusababisha vifo vya watu takriban 20 na kujeruhi wengine wengi.

Shambuli hilo lilitokea siku ya Alhamisi limetekelezwa na watu wanaoshukiwa kuwa ni wanamgambo wa Al-Shabab katika eneo lililosheheni hoteli, maduka na migahawa. Vikosi vya usalama vya Somalia baadaye viliwazingira watu hao waliokuwa na silaha na majibizano ya silaha yakaendelea usiku kucha mjini Mogadishu.

Duru hizo zinasema hatimaye leo vikosi hivyo vya usalama vimefanikiwa kuwauwa watu wote watatu waliokuwa na silaha wakishikilia jengo moja la mtaa huo.

Katibu Mkuu amesema anaamini kwamba shambulio hilo halitowakatisha tamaa Wasomali ya kuendelea kusaka amani na mustakabali bora.

Amerejelea wito wake kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia na kushikamana na serikali na watu wa Somalia.