Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika katika COP27: Guterres ataka taasisi za kifedha zibadili miundo ya biashara

Mradi wa UNEP wa kusaidia serikali ya Zambia kuboresha huduma za maji na kukabiliana na  athari za ukame
UNEP/ Georgina Smith
Mradi wa UNEP wa kusaidia serikali ya Zambia kuboresha huduma za maji na kukabiliana na athari za ukame

Afrika katika COP27: Guterres ataka taasisi za kifedha zibadili miundo ya biashara

Tabianchi na mazingira

Hii leo huko kwenye mji wa pwani wa Sharm el- Sheikh nchini Misri kunakofanyika mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27, kumefanyika mjadala wa viongozi juu ya kuchagiza harakati za kuwezesha bara la Afrika kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres “tunahitaji kuwekeza kwa kina kwenye miradi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi iwapo tunataka kuepuka kutumia fedha nyingi zaidi katika kukabili madhara ya majanga.”

Ameongeza kuwa suala hilo ni dhahiri ya kwamba tunahitaji kugawana vema ufadhili kwenye uwekezaji wa kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa benki ya kimataifa za maendeleo zina uwezo mkubwa wa kuhamasisha na kuchangisha fedha kutoka sekta binafsi ambazo kwa sasa hazijaelekezwa kwenye miradi ya hatua kwa tabianchi.

Amefafanua “hii ina maana kubadili mifumo na miundo ya biashara, kukubali kukabiliana na hatari zaidi na kuwa mstari wa mbele kama taasisi za kifedha zenye ushirika katika kubeba hatari inayoweza kutokea.”

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, alihutubia pia mkutano huo ambapo amesisitiza kuwa Afrika ina mchango mdogo mno katika kusababisha madhara ya tabianchi lakini “watu wetu, hasa vijana ndio wanaathirika zaidi na madhara hayo.”

Ametoa wito kwa uungaji mkono na usaidizi katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Akinwumi Adesina, amesema “tunahitaji uugwaji mkono katika Programu ya Afrika ya Kukabili mabadiliko ya tabianchi. Tunahitaji msaada wenu wa kufadhili hatua kwa tabianchi kupitia mfuko wa Maendeleo wa Afrika.”