Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa na umasikini ni sumu ya maendeleo Afrika lazima tuvitokomeze:FAO/AfDB

Wafugaji wakipeleka mifugo kwenye malisho
FAO/Giulio Napolitano
Wafugaji wakipeleka mifugo kwenye malisho

Njaa na umasikini ni sumu ya maendeleo Afrika lazima tuvitokomeze:FAO/AfDB

Ukuaji wa Kiuchumi

Benki ya maendeleo ya Afrika AfDB na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO zimekubaliana kuendeleza juhudi za pamoja  za kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo barani Afrika ili kukomesha njaa, na utapia mlo kwa lengo la  kupanua wigo  wa ustawi na maendeleo barani humo.

Makubaliano hayo yamefanyika mjini Roma Italia ambapo AfDB na FAO zimeazimia kuongeza dau la ufadhili hadi kufikia dola milioni 100 katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kufanikisha shughuli zao za pamoja.

Ushirika huo mpya, una lengo la kuongeza ubora wa uwekezaji na faida zake katika uhakika wa chakula, lishe, ulinzi wa jamii, kilimo , misitu, uvuvi pamoja na maendeleo ya vijijini.

Baada ya kutia saini muafaka huo, Rais wa AfDB, Akinwumi Adisa amesema

Makubaliano haya na FAO  yataisaidia FAO kuanzisha miradi  ya maendeleo ambayo kama benki tunaweza  kusaidia kuifadhili , kupitia vituo vya uwekezaji vya FAO tunaweza kusaidia sekta binafsi za kimaendeleo  ambazo kama Benki  ya Afrika tunaweza kuzisadia.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jose Graziano da Silva, amesema kuwa , FAO na Benki ya maendeleo ya Afrika zinapanua wigo wa ushirika kuweza kusaidia mataifa ya Afrika  kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu SDG’s, na kufadhili kilimo pamoja na sekta binafsi ambazo  ndio ufunguo wa kuwatoa mamilioni ya watu katika njaa na umasikini uliokithiri barani Afrika  lakini pia kuhakikisha kunakuwepo chakula cha kutosha.

 

Oumou,mmoja wa wanofaidika na mpango wa FAO akifunga mbuzi wake aliowapata  kutoka mpango wa ufugaji wa FAO nchini Mali
FAO/Sonia Nguyen
Oumou,mmoja wa wanofaidika na mpango wa FAO akifunga mbuzi wake aliowapata kutoka mpango wa ufugaji wa FAO nchini Mali

 

Ushirika baina ya AfDB na FAo ulianza mwaka 1968 na tangu hapo FAO umetoa msaada wa kiufundi katika kuanzisha miradi 161 ya sekta ya kilimo inayofadhiliwa na AfDB yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3.7.

Muafaka huu mpya utafaidisha nchi kadhaa ikiwemo Tanzania, Equatorial Guinea, Côte d'Ivoire, Morocco and Cape Verde.

Mkakati wa benki hiyo wa “lisha Afrika” uliozinduliwa mwaka 2015 unalenga kuwekeza dola bilioni 25 katika kilimo barani Afrika  kwa kipindi cha zaidi ya miaka10 ili kuboresha será za kilimo, soko,miundo mbinu na taasisi ili kuhakikisha nyenzo muhimu ikiwepo teknolojia bora inawekwa kwa wakulima kuweza kuitumia.