Vijana wa Afrika wachoshwa na porojo za tabianchi, wataka hatua zichukuliwe
Vijana wa Afrika wachoshwa na porojo za tabianchi, wataka hatua zichukuliwe
Ule usemi wa vijana ni taifa la kesho, umeonekana kuwa kesho haitaweza kufika na ndio maana vijana kutoka kila pembe ya dunia wamefunga safari kwenda kuhudhuria mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27 unaofanyika huko nchini Misri.
Vijana hao wake kwa waume wamefanya mambo mbalimbali ikiwemo kushiriki katika mikutano ya wakuu wa nchi na serikali, kufanya maandano nje ya kumbi za kimutano na pia kuendesha mikutano wenyewe kueleza kile wanachotaka kifanyike na tena kwakuwashirikisha ili dunia kukabiliana na changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi.
Katika kila eneo la viunga vya Pwani ya Sham el Shekhe kunakofanyika mkutano wa COP27 vijana bila kuchoka walieleza hisia zao kwa njia tofauti kuanzia kwenye muziki, ngoma, mavazi ya rangi nzuri za kupendeza na michoro ya ukutani yenye ujumbe kwa viongozi wa dunia mpaka kushiriki katika mazungumzo na wanachokisema ni kimoja tu, wanataka hatua zichukuliwe na zichukuliwe sasa.
Afrika Mashariki
Kutoka nchini Uganda mwanaharakati kijana wa tabianchi patience Nabuklau anasema “Ujumbe wangu kwa kiongozi wa dunia ni kuacha kuwekeza kwenye nishati chafu barani Afrika. Afrika sio jalala. Afrika si mahali pa uchimbaji wa mafuta ya kisukuku. Afrika pekee inachangia chini ya asilimia 3 ya hewa chafu duniani, lakini tunateseka zaidi kutokana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Tunahitaji hatua na tena zichukuliwe sasa hivi.”
Afrika Magharibi
Mawazo haya yanaungwa mkono na Margaret Impraim, kutoka Ghana “Niko hapa kujifunza juu ya kile kinachoendelea na kusaidia watu kuelewa hitaji la ushirikiano kama mtu binafsi na kama shirika ili pamoja tujue namna ya kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinatakiwa kuchukuliwa na kila mmoja wetu, na kama Mghana, najua kitu ambacho ni muhimu ni sote tunapaswa kuja pamoja ili kuhakikisha kwamba jukumu letu ni kuhakikisha tunatokomeza mabadiliko ya tabianchi nchini mwangu na hasa katika kuhakikisha kwamba sote tunaunganisha nguvu zetu na kuhakikisha kwamba hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi niza kweli nchini Ghana.”
Kaskazini mwa Afrika
Saad Uakkas, kutoka kutoka Morocco naye anahitimisha kwakusema mazungumzo ya fidia kwa waliaothirika na tabianchi yafanyike haraka ili kusaidia jamii zinazoteseka. “Kama Kijana wa Morocco na mwanaharakati wa tabianchi wa Afrika, nina furaha sana kwamba COP inafanyika barani Afrika. Na ndio maana ni muhimu sana kuharakisha mazungumzo ili kupitisha ufadhili wa tabianchi kufidia hasara na uharibifu na kusaidia jamii na kuunga mkono bora letu ili kusaidia wale walio katika mazingira magumu.”
Maeneo mengi ni vijana walionekana wakiimba huku wakiwa wameshika mabango na kufanya maandamano kuwa hawataki tena Bla Bla Bla wanataka kufidia ya hasara na uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Bila shaka ujumbe wenu na uwepo wenu nchini Misri utaleta tofauti, hongera vijana wote.