Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF inasaidia kukabiliana na utapiamlo kwa watoto nchini Sudan

Mama akipokea fedha kama sehemu ya msaada wa kuwezesha mama na mtoto kuwa na fedha za kujikimu, ikiwa ni mpango wa UNICEF nchini Sudan.
© UNICEF/Florin Bos
Mama akipokea fedha kama sehemu ya msaada wa kuwezesha mama na mtoto kuwa na fedha za kujikimu, ikiwa ni mpango wa UNICEF nchini Sudan.

UNICEF inasaidia kukabiliana na utapiamlo kwa watoto nchini Sudan

Msaada wa Kibinadamu

Takriban watoto milioni 3 wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini Sudan, wanakabiliwa na utapiamlo, ambapo kati yao 650,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali sana.  Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linafanya kila juhudi ili kuwasaidia watoto hawa kama anavyosimulia

Takriban wananchi milioni 12 nchini Sudan wanakabiliwa na uhaba wa chakula hali ambayo imeathiri zaidi afya za wanawake na watoto kwani familia nyingi hazina uwezo wa kupata chakula na hata pale wanapopata kinakosa virutubisho muhimu na hali hii imeongeza tatizo la watoto wenye utapiamlo nchini humo.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF kwa kushirikiana na wadau wake wanafanya kazi ya kuhakikisha wanazuia watoto kupata utapiamlo, wanagundua watoto wenye utapiamlo na kuwatibu kama anavyoeleza Afafa Mohammed Briema Afisa lishe wa UNICEF katika jimbo la Darfur Kaskazini.

“Tunatembelea kituo cha kufundisha kuhusu lishe huko kwenye jamii ambapo huko wakina mama hupokea ushauri nasaha na elimu kuhusu namna bora za kuwalisha Watoto na usafi wakati wa unyonyeshaji. Pia tunawafanyia uchunguzi wa utapiamlo watoto wao, kazi inayofanywa na maafisa lishe pamoja na vikundi vya akina mama waliopatiwa mafunzo ili waweze kuwatambua wale wenye utapiamlo mkali na kuwapa ushauri wa kwenda kwenye vituo husika kwa ajili ya msaada zaidi.”

Afisa lishe Briema anasema watoto walio na afya njema wanaendelea kupewa ushauri,  na wale wenye matatizo ya kiafya wanasajiliwa katika programu za uangalizi, lakini wenye utapiamlo mkali wanapelekwa katika vituo vya afya maalum kwa ajili ya wenye utapiamlo.

“Wakiwa hapa Watoto hupatiwa matibabu ya maradhi yanayowasibu na kupatiwa maziwa ya matibabu kw ajili ya utapiamlo na mara baada ya afya zao kuimarika wanapokea chakula cha matibabu ambacho kipo tayari kwa matumizi na wanaruhusiwa kwenda nyumbani ambapo huko wataendelea na matibabu katika programu za nje kwa Watoto waliokuwa wamelazwa.”

Ili kuendelea kuhakikisha Watoto nchini Sudan wanakuwa hai na wenye afya bora, UNICEF imetoa ombi kwa wadau, ombi la kuunganisha nguvu ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo kwa kuwapatia taarifa wakina mama na watoa huduma za afya jinsi ya kuwapatia Watoto lishe bora ili wasipate utapiamlo.