Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu wazidi kufurushwa Darfur- WFP

Binti wa miaka 7 akimpa maji ya kunywa bibi yake kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Darfur nchini Sudan
© UNICEF/Shehzad Noorani
Binti wa miaka 7 akimpa maji ya kunywa bibi yake kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Darfur nchini Sudan

Maelfu wazidi kufurushwa Darfur- WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP linaimarisha msaada kwa watu waliofurushwa makwao baada ya mapigano ya kikabila magharibi na kusini mwa Darfur nchini Sudan kusababisha watu 100,000 kukimbia ili kusaka usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa WFP Tomson Phiri, amesema takriban wakimbizi 70,000 wamekusanyika katika vituo 70 kwenye mji wa Geneina magharibi mwa Darfur na shirika hilo limeanza kusambaza mgao wa chakula kwa watu ndani mwa Geneina na kufikia watu 40,000 katika vituo 30 kati ya vituo 71. 

Bwana Phiri amesema “msaada unajumuisha mtama, nafaka na chumvi  kwa ajili ya kupika mlo pamoja na biskuti zenye virutubisho ambazo zinapatiwa watoto kwa ajili ya lishe ya papo hapo na watu wazima wasio na maji ya kupika. Mgao wa chakula unaendelea ili kuwafikia waathirika ndani ya mji ambapo usambazaji nje ya mji utaanza baada ya kukamilika kwa kazi ya utambui wa wakimbizi.”

Ameongeza kuwa shirika hilo lina hofu kubwa  “juu  ya ghasia zinazoendelea. Novemba na Januari ni wakati wakulima wanaanza msimu wa upanzi wakati wa majira ya baridi na ni msimu mkuu wa mavuno ya mtama na ulezi. Hivyo vurugu zozote za shughuli zao za kujipatia kipato zinaweza kuwa na athari za muda mrefu.”

Bwana Phiri amesema iwapo wakulima watashindwa kupanda au kuvuna mazao katika msimu wa sasa itakuwa vigumu kufanya hivyo wakati mwingine.

Halikadhalika amesema iwapo mifugo haitaweza kuswagwa kwenda kwenye malisho au kunywa maji, mifugo hiyo itakufa na wanaoathirika zaidi ni familia maskini ambaoz hali ya kupata chakula itazidi kuwa mbaya.