Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaingiwa hofu kufuatia Urusi kusitisha ushiriki wake kwenye makubaliano ya usafirishaji nafaka Bahari Nyeusi

Meli ya kwanza ya kibiashara ikiwa na nafaka kupitia mpango wa usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi
© UNOCHA/Levent Kulu
Meli ya kwanza ya kibiashara ikiwa na nafaka kupitia mpango wa usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi

UN yaingiwa hofu kufuatia Urusi kusitisha ushiriki wake kwenye makubaliano ya usafirishaji nafaka Bahari Nyeusi

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya uamuzi wa Urusi kusitisha ushiriki wake kwenye makubaliano ya usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi, au kwa kiingereza, Black Sea Grain Initiative, makubaliano ambayo yalianzishwa tarehe 22 mwezi Julai mwaka huu ili kuwezesha Ukraine kuanza kuuza tena nje ya nchi hiyo vyakula na mbolea.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric amesema kupitia taarifa aliyoitoa jumapili jijini New York, Marekani kuwa, Katibu Mkuu ameamua kuchelewesha kwa siku moja safari yake ya kwenda kushiriki mkutano wa viongozi wa nchi za kiarabu huko Algiers, Algeria ili kujadili suala hilo la Urusi kujiondoa kwenye mpango huo.

Kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tarehe 24 mwezi Februari mwaka 2022, shehena kubwa za nafaka zilisalia kwenye mabohari nchini Ukraine, meli zikishindwa kupata njia salama ya kupita kuelekea au kutoka bandari za Ukraine huku njia za barabara zikiwa hazitoshelezi kukidhi mahitaji ya usafirishaji.

Hali hiyo ilisababisha ongezeko kubwa la bei za vyakula duniani kote kutokana na Urusi na Ukraine kuwa wasafirishaji wakubwa wa nafaka kama vile ngano.

Ikijumuishwa pia na ongeezko la gharama ya nishati, nchi zinazoaendelea zilikuwa hatarini kushindwa kulipa madeni na ongezeko la watu walio hatarini kukumbwa na baa la njaa.

Mpango huo wa usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi ulikuwa ufikie ukomo wiki ya tatu ya mwezi ujao wa novemba lakini kulikuweko na fursa ya kuongeza muda iwapo pande zote ikiwemo Urusi na Ukraine zingekubali.

Mamilioni waliokolewa kutoka kwenye umaskini

Bila shaka makubaliano hayo yalisaidia kushusha bei za vyakula na kuwezesha mamilioni ya tani za ujazo za nafaka kusafirishwa kwa usalama kutoka bandari za Ukraine.

Hadi mwezi uliopita wa Septemba, Rebecca Grynspan Mkuu wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara, UNCTAD na pia mratibu wa mpango huo alitangaza kuwa bei zimeshuka kwa miezi mitano mfululizo na kwamba kipimo cha bei ya vyakula kimepungua kwa takribani asilimia 14 kutoka kiwango cha juu zaidi mwezi Machi.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifam Mpango huo kwa njia moja au nyingine umeepusha watu milioni 100 kutumbukia kwenye ufukara.

Kulikoni Urusi kujitoa kwenye mpango wa Bahari Nyeusi?

Uamuzi wa Urusi kujitoa kwenye mpango huo ulitangazwa Jumamosi, ikidai kuweko kwa shambulio kwenye meli katika bandari ya Ukraine ya Sevastopol kwenye rasi ya Crimea, eneo ambalo Urusi ilijitwalia mwaka 2014.

Hatua hiyo yaripotiwa ilishangaza wafanyabiashara na kuongeza hofu ya ongezeko la bei za vyakula.

Mchumi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP, Arif Husain, ameripotiwa kuionya Urusi ya kwamba uamuzi wake unatishia kuleta hatari kubwa kwa nchi nyingi na kwamba ipatie suluhu suala hilo mapema iwezekanavyo.

Bwana Dujarric amesema Katibu Mkuu anaendelea kufanya mawasiliano ya kina yenye lengo la kumaliza sitisho hilo la Urusi kushiriki kwenye mpango huo.

Mawasiliano hayo yanalenga pia kurejesha utekelezaji kamilifu wa Mpango huo wa usafirishaji nafaka na mbolea kupitia Bahari Nyeusi kutoka Ukraine pamoja na kuondoa vikwazo vyovyote vilivyosalia vya kusafirisha vyakula na mbolea kutoka Urusi.