Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha kwa moyo mkunjufu tangazo la Urusi kurejea katika makubaliano ya Bahari Nyeusi

Mjini Istanbul, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaangalia meli ya WFP SSI Invincible 2, ikielekea Ukraine kuchukua shehena kubwa zaidi ya nafaka ambayo bado inasafirishwa nje ya nchi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.
UN Photo/Mark Garten
Mjini Istanbul, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaangalia meli ya WFP SSI Invincible 2, ikielekea Ukraine kuchukua shehena kubwa zaidi ya nafaka ambayo bado inasafirishwa nje ya nchi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

UN yakaribisha kwa moyo mkunjufu tangazo la Urusi kurejea katika makubaliano ya Bahari Nyeusi

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha kwa moyo mkunjufu tangazo la Urusi la kurejea kwenye ushiriki wa makubaliano ya kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi au Black Sea Grain Initiative, ikiwa ni siku nne tangu itangaze kusitisha ushiriki wake.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu imo kwenye taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric.

Guterres ashukuru waliofanikisha hatua hii

Bwana Guterres amesema hatua hiyo ya Urusi, itafanikisha usafirishaji salama wa nafaka, vyakula na mbolea kutoka Ukraine kwenye nchi zingine.

“Ninatoa shukrani kwa juhudi za kidiplomasia za Uturuki, na shukrani sana kwa Mratibu wa Umoja wa Mataifa Amir Abdulla, na timu yake kwa kazi yao waliyofanya ya kuhakikisha njia hii ya usambazaji wa chakula inasalia wazi,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika Katibu Mkuu amesema anaendelea kuwasiliana na washiriki wote wa makubaliano hayo yaliyoanza kazi mwezi Julai mwaka huu ili yaweze kutiwa tena saini kwa kuwa ukomo wake unafikia tarehe 18 mwezi huu wa Novemba.

“Nimejizatiti kuendelea kuondoka vikwazo vyote vilivyosalia kwenye usafirishaji nje ya nchi wa vyakula na mbolea kutoka Urusi,” amesema Katibu Mkuu Guterres.

Tweet URL

Yaliyojiri baada ya Urusi kusitisha ushiriki wake

Punde tu baada ya Urusi kutangaza kusitisha ushiriki wake kwenye mpango huo wa usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi kwa madai ya mashambulizi kwenye bandari iliyoko eneo ambalo ilijitwalia, bei za vyakula zilipanda.

Katibu Mkuu alitoa taarifa kusihi Urusi irejee, huku pia akisogeza mbele kwa siku moja kuanza kwa ziara yake huko Algeria alikokuwa anakwenda kushiriki mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa nchi za kiarabu.

Mapema leo, Mratibu wa UN kwenye mpango huo, Amiri Abdullah naye kupitia mtandao wake wa Twitter alitangaza uamuzi huo wa Urusi wa kurejea kwenye makubaliano.

Urusi na Ukraine zinazalisha kiwango kikubwa cha nafaka itumikayo duniani

Kwa mujibu wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, mpango wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi umesaidia sana kupunguza bei za vyakula ambazo zilipanda kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu lukuki ikiwemo kitendo cha Urusi kuvamia Ukraine.

MKurugenzi wa WFP Pembe ya Afrika Michael Dunford akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani alikiri kuwa bei za vyakula zilishuka punde tu baada ya meli ya kwanza Brave Commander kuondoka bandari ya Ukraine mwezi Agosti mwaka huu wa 2022 ikiwa tani 23,000 za ujazo wa ngano.

"Urusi ilipotangaza kusitisha ushiriki wake, bei tuliona zimepanda," amesema Bwana Dunford akiongeza, "najua kwamba ukanda huo ni mzalishaji mkubwa wa mbolea na kiasi kikubwa kinapelekwa kwenye pembe ya Afrika. Kupungua kwa bei ya mbolea kunamaanisha kuongezeka kwa mazao kwa wakulima na hatimaye kuongeza uhakika wa chakula. Hivyo sababu zote zinahitaji kutiliwa maanani na wafanya maamuzi. Kwa hakina hatutaki kuona kwamba baada ya majadiliano mengi mradi huo unaruhusiwa kuteleza” 

Urusi na Ukraine zinachangia takribani asilimia 30 ya ngano na shayiri yote inayotumika duniani.