Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa Bahari Nyeusi wawezesha zaidi ya tani milioni 30 za nafaka kusafirisha - UN

Timu ya pamoja ya kiraia ya ukaguzi inayojumuisha maafisa kutoka Shirikisho la Urusi, Uturuki, Ukraine na Umoja wa Mataifa ilitembelea meli ya kibiashara ya Razoni mnamo tarehe 3 Agosti 2022.
© UNOCHA/Levent Kulu
Timu ya pamoja ya kiraia ya ukaguzi inayojumuisha maafisa kutoka Shirikisho la Urusi, Uturuki, Ukraine na Umoja wa Mataifa ilitembelea meli ya kibiashara ya Razoni mnamo tarehe 3 Agosti 2022.

Mpango wa Bahari Nyeusi wawezesha zaidi ya tani milioni 30 za nafaka kusafirisha - UN

Msaada wa Kibinadamu

Makubaliano yaliyoratibiwa na  Umoja wa Mataifa ya kusafirisha nafaka, chakula na mbolea kutoka Ukraine kupitia Bahari Nyeusi kwa lengo la kukabiliana na ongezeko la uhaba wa chakula lililochochewa na vita nchini Ukraine, yamewezesha usafirishaji salama wa zaidi ya tani za ujazo milioni 30 tangu yaanze kutekelezwa mwezi Julai mwaka jana. 

Huo  ndio  ujumbe wa Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, Martin Griffiths, ujumbe aliotoa kwenye mkutano uliofanyika Alhamisi huko Istanbul, Uturuki kujadili mustakabali wa makubaliano hayo, mkutano uliohusisha pia maafisa waandamizi wa pande zilizotia saini mpango huo ambazo ni Urusi na Ukraine, pamoja na Umoja wa Mataifa na Uturuki ambazo ziliratibu makubaliano hayo. 

Muhimu kwa uhakika wa chakula duniani 

Nyaraka kwa waandishi wa habari kuhusu mkutano huo iliyotolewa na Ofisi ya Msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Bwana Griffiths akipongeza pande zote – ambazo pia zinaendesha Kituo cha Pamoja cha Uratibu kilichoko huko Istanbul – kwa kufikia kiwango hicho cha tani za ujazo milioni 30 za chakula kutoka Ukraine, na kusisitiza “umuhimu wa mpango huo kwa uhakika wa upatikanaji wa chakula duniani.” 

Mkuu huyo wa OCHA ametambua pia umuhimu wa mchango wa chakula na mbolea vinavyosafirishwa kutoka Urusi. 

Mapendekezo ya UN 

Mkutano huo pia ulijadili mapendekezo ya hivi karibuni ya kusongesha makubaliano hayo, mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa, kuhusu kuanza tena kutumika kwa bomba la kusafirisha ammonia kati ya Togliatti na Odesa, kuongezwa zaidi kwa muda kwa makubaliano hayo, na kuimarishwa kwa kituo cha pamoja cha uratibu, “kwa ajili ya kuweka utulivu kwenye usafirishaji nje wa bidhaa husika na masuala mengine yaliyoibuliwa na pande husika kwenye makubaliano hayo.” 

“Pande husika ziliwasilisha maoni yao na kukubali kujumuisha vipengele hivyo wakisonga mbele,” imesema taarifa hiyo. 

Bwana Griffiths amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa “utaendelea kufanya kazi kwa karibu na pande zote mbili kufanikisha mwendelezo na utekelezaji kamilifu wa mpango huo ili kupata hatimaye ahadi pana na ya pamoja katika kushughulikia ukosefu wa  uhakika wa chakula duniani. 

Nafaka kwa wanaohitaji zaidi 

Takwimu za hivi karibuni zaidi kuhusu mpango huo zinaonesha kuwa hadi Jumatatu ya tarehe 8 mwezi Mei 2023, takribani tani za ujazo 600,000 za nafaka zimesafirishwa kwa meli zilizokodishwa na shirika la Umoaj wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP kusaidia operesheni za kiutu huko Afghanistan, Ethiopia, Kenya, Somalia na Yemen. 

Mwaka jana, Ukraine ilichangia kwa WFP zaidi ya nusu ya mahitaji ya ngano duniani kote, sawa na mwaka 2021. 

Kadri mazungumzo yalivyoendelea kwa miezi michache iliyopita kuhusu kuongezwa muda kwa mpango huo – ambao  unapatia njia salama kwa vyombo vya majini kusafirisha shehena za bidhaa kutoka bandari za Ukraine, - mauzo ya nje yametwama kwa takribani asilimia 30, huku ukaguzi wa JCC ukipungua kwa wastani wa asilimia 2.9 kwa siku tangu mwezi Mei. 

Taarifa mpya zilizotolewa Jumatatu kutoka Ofisi ya Mratibu wa UN kuhusu mpango huo, zinasema wajumbe wa Umoja wa Mataifa na Uturuki wanafanya kazi kwa karibu na Ukraine na Urusi, kwa lengo la kufanikisha mienendo na ukaguzi wa meli zinazoingia na kutoka, “ndani ya mfumo wa mpango huo na kanuni zilizokubaliwa, huku mijadala kuhusu mustakabali wa makubaliano hayo ikiendelea.”