Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda yaadhimisha miaka 60 ya kuwa mwanachama wa UN

Maadhimisho ya miaka 60 ya Rwanda kwenye UN.
UN RWANDA
Maadhimisho ya miaka 60 ya Rwanda kwenye UN.

Rwanda yaadhimisha miaka 60 ya kuwa mwanachama wa UN

Masuala ya UM

Serikali ya Rwanda na Umoja wa Mataifa wataadimisha miaka 60 ya Rwanda kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa chini ya maudhui “Ushirikiano kwa ajili ya mustakbali bora na wa pamoja kwa wote.”  Kutoka Kigali Rwanda Flora Nducha na maelezo zaidi

Hafla rasmi ya maadhimisho hayo itafanyika Jumatatu ya tarehe 24 Oktoba 2022 mjini Kigali.

Hafla hiyo itafuatiwa na zoezi la upandani miti ya matunda katika wilaya za Huye, Muzanze na mji mkuu Kigali Jumamosi ya tarehe 29 Oktoba wakati wa Umuganda ambao ni mradi wa shughuli za kijamii za uhifadhi wa mazingira zinazofanyika kila jumamosi ya mwisho wa mwezi. 

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Rwanda shughuli hizi ni fursa ya kutafakari kuhsu hadithi za mafanikio na yale ya kujifunza kutoka kwenye ushirikiano kati ya Rwanda na Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Rwanda Vincent Biruta amesema:

“Tunaupongeza Umoja wa Mataifa kwa uungaji mkono wake kwa nchi yetu na kwa kuendeleza juhudi na ushirikiano wa kimataifa. Rwanda inasalia kujizatiti kwenye ushirikiano wetu katika kushughulikia changamoto za pamoja katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, usawa wa kijinsia, ulinzi wa amani, ulinzi wa haki za wakimbizi, mabadiliko ya tabianchi, na mengine mengi. Dunia inahitaji ushirikiano thabiti na wenye ufanisi miongoni mwa nchi, na Rwanda itatekeleza jukumu lake daima."

Naye mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda Ozonnia Matthew Ojielo kwa upande wake amesema:

“Umoja wa Mataifa unatoa shukrani zake za dhati kwa serikali na watu wa Rwanda kwa uungaji wao mkono na kuendelea kujitolea kufanya kazi kwa karibu kwa manufaa ya watu wa nchi hii bila kumuacha mtu yeyote nyuma. Tunasisitiza dhamira ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na tunaahidi ushirikiano na msaada kwa njia zote ili kushughulikia malengo ya pamoja yanayozingatia mkataba wa Umoja wa Mataifa.”

Rwanda ni moja ya nchi wachangiaji wakubwa wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa wakiwa na zaidi ya askari na polisi 5,000 wanaohudumu katika nchi mbalimbali.

Rwanda pia ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zilitimiza malengo ya maendeleo ya Milenia na iko mbioni kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

Rwanda ilijiunga na Umoja wa Mataifa kama mwanachama tarehe 18 Septemba 1962, kufuatia kupitishwa kwenye Baraza la Usalama Azimio namba A_RES_1748(XVII) mwezi Julai mwaka huohuo.

Tangu wakati huo serikali ya Rwanda imekuwa ikishirikiana na Umoja wa Mataifa katika masuala mbalimbali ili kutimiza malengo ya maendeleo endelevu kuanzia masuala ya kilimo hadi ajira kwa vijana, na shughuli mbalimbali zimechangia katika mabadiliko ya Rwanda ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika miaka 60 iliyopita.