Vijana shikeni usukani, tunawategemea katika kutimiza SDGs:Guterres

12 Aprili 2019

Vijana kote duniani wametakiwa kushika hatamu za kusongesha mbele ajenda ya maendeleo endelevu SDGs kwa sababu sauti zao ni muhimu na uwezo wanao.

Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterrres wakati wa ufunguzi wa jukwaa la vijana la mfano wa Umoja wa Mataifa (Model UN) lililoanza kwenye makao makuu mjini New York Marekani. Guterres amesema mara nyingi vijana huachwa nyuma lakini sasa watapewa kipaumbele kwani mchango wao utakifaa kizazi cha sasa na kijacho.

Ameongeza kuwa “kote duniani kuna mifano halisi ya nini kinachofanywa na vijana kuleta mabadiliko duniani, kuanzia masuala ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na hata kitamaduni.”

Amesisitiza kuwa jukwaa la mfano wa Umoja wa Mataifa ni fursa nzuri kwa vijana washiriki wawe ni kutoka vyuo vikuu, au shule za sekondari ni njia ya kujifunza kuhusu dunia, Umoja wa Mataifa na jinsi ushirikiano wa kimataifa unavyofanya kazi hasa katika masuala muhimu yanayoigusa dunia ikiwemo kwa vijana.

“Mnakutana katika wakati ambao tunakabiliwa na changamoto lukuki. Mabadiliko ya tabia nchi yanakwenda kasi kuliko juhudi zetu za kuyashughulikia, chuki inaongezeka, umasikini na umasikini na vita vianaendelea kuongeza madhila, wanawake na wasichana wanaenendelea kukabiliwa na ubaguzi na vijana wengi wanakosa ajira na elimu wanayohitaji ili kutimiza ndoto zao.”

Vijana wakiwezeshwa kupata uwezo wa kutumia kompyuta katika kituo cha UN-Habitat Kigali,Rwanda.
© UN-Habitat /Julius Mwelu
Vijana wakiwezeshwa kupata uwezo wa kutumia kompyuta katika kituo cha UN-Habitat Kigali,Rwanda.

Guterres amesema wakati huohuo kuna mpango ambao unatuongoza ambao ni ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu SDGs, lakini changamoto ni kuchukua usukani. “Ili kufikia malengo 17 ya maenmdeleo endelevu tunahitaji uhamasishaji ambao unakwenda mbele zaidi ya serikali, na hapo ndipo mnapokuja, kwani sauti ya vijana ni muhimu sana. Mara nyingi tunasikia watu wakizungumza kuhusu nini tunachotaka kufanya kwa vijana, Mimi napenda kufikiria kuhusu nini tunaweza kufanya na vijana.”

Ameongeza kuwa “Si juu ya kizazi changu kuelezea será za vijana bali kizazi chenu kufanyakazi pamoja na kizazi changu kuhakikisha kwamba será hizo zinakwenda sanjari na mahitaji na matarajio yenu.”

Amewalezeka vijana hao kwamba katika kusonga mbele “tunataka kuhakikisha kwamba malengo ya maendeleo endelevu SDGs yanakuwa sehemu kubwa ya mazungumzo yenu.”

Kundi la wanafunzi wanakihudhuria vikao vya Model UN kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
Picha na UN/DPI
Kundi la wanafunzi wanakihudhuria vikao vya Model UN kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa

Amewaambia kwamba kwenye Umoja wa Mataifa inafahamika kuwa vijana mara nyingi wanahisi wanaachwa nyuma katika mchakato wa kufanya maamuzi yanayowaathiri na kwamba wanapozungumza hawasikilizwi, sasa amewaahidi “hivyo kuanzia leo hii tunaahidi kuwaonyesha jinsi gani mnaweza kushiriki kwenye kampeni za Umoja wa Mataifa na kufanya kazi nasi. Tunawategemea kufikisha ujumbe wa mlichojifunza kwa zaidi ya klabu zenu za mfano wa Umoja wa Mataifa, tunawataka kuwahamasisha zaidi ya maelfu ya vijana walioandamana mwezi uliopita kwa ajili ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, tunawataka mkifanye kizazi changu kiwajibike na pengine muwe na ujasiri zaidi ya kizazi changu. Kwani ninauhakika kwamba mkihusishwa hakuna mtakachoshindwa kufanya”

Duniani kote kuna zaidi ya vijana 400,000 wanaoshiriki katika mfano wa Umoja wa Mataifa kila mwaka na idadi hiyo imeelezewa luongezeka.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter