Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa KJP Kigoma nchini Tanzania wasaidia wakazi kuinua vipato: Asante UN

Huyu ni Kejelina Alfred mkazi wa Kigoma na mnufaika wa Mradi wa Pamoja wa Kigoma, KJP unaotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2017. Hivi sasa anamiliki nyumba yake kutokana na mradi wa kuku uliofadhiliwa na KJP.
FAO Tanzania
Huyu ni Kejelina Alfred mkazi wa Kigoma na mnufaika wa Mradi wa Pamoja wa Kigoma, KJP unaotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2017. Hivi sasa anamiliki nyumba yake kutokana na mradi wa kuku uliofadhiliwa na KJP.

Mradi wa KJP Kigoma nchini Tanzania wasaidia wakazi kuinua vipato: Asante UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania mashirika ya Umoja wa Mataifa kupitia Mradi wa Pamoja wa Kigoma KJP, yameendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa hususan namba 1 la kutokomeza umaskini kwa kushirikisha wananchi kwenye miradi ya kuwawezesha kuinua vipato vyao.

Mradi huo wa KJP ulioanza mwaka 2017 kwenye mkoa wa kaskazini-magharibi mwa Tanzania, Kigoma hivi karibuni ulifanikisha maonesho kwenye Halmashauri ya Mji wa Kasulu, maonesho yaliyoleta wanufaika wa miradi ya KJP kutoka wilaya za kasulu vijijini, Kakonko na Kibondo.

Tweet URL

Je wajua faida za kufuga kambale na sato kwenye bwawa moja?

Miongoni mwa wanufaika hao ni kijana Levis Rugayaza ambaye yeye ingawa ni mwanafunzi anashirikiana na baba yake kufuga samaki kufuatia mafunzo ya ufugaji bora kupitia mradi wa pamoja wa Kigoma.

Kijana Levis anasema “sisi tunafuga samaki kwa ajili ya kujipatia kipato lakini pia kuongeza aina mbalimbali za lishe katika kaya yetu ikiwemo protini.  Tunajipatia mboga mboga kama samaki

Katika maonesho hayo alikuwa na bwawa la mfano likiwa na samaki ambamo amechanganya kambale na sato akisema kambale wanasaidia kuchimba mashimo ambayo yatamsaidia sato kutaga mayai yake. Halikadhalika wakati wa kiangazi, maji yakipungua bwawani, sato atatumia mashimo hayo kujificha ili kukwepa joto linalotokana na jua.

Kijana huyu akawa na ujumbe kwa vijana hususan walio shuleni akisema, ujumbe wangu si kwa walio shuleni tu na hata wale wasio shuleni ya kwamba wajishughulishe na kazi mbalimbali kwa sababu kilimo ndio kinaweza kuwainua kama yeye ambavyo anashiriki ufugaji wa samaki ambao sasa unampatia kipato.

Ufugaji kuku umeniwezesha kujenga nyumba- Bi. Alfred

Mradi wa KJP pia umewezesha wanawake kushiriki kwenye  ufugaji kuku kwa kisasa na matokeo ya kuondokana na umaskini yako dhahiri kama anavyosimulia mnufaika aliyejitambulisha kwa jina la Kejelina Alfred.

“Nimekuja hapa kuwakilisha wafugaji wa kuku. Nimekuja na kuku na kwa manufaa niliyoyaona nimeweza kujenga nyumba kutokana na manufaa ya ufugaji wa kuku.”

Katika maonesho haya Bi. Alfred yuko na mabanda ya kisasa ya kufugia kuku yanayowezesha kufuga kuku wengi kwenye eneo dogo. Akafafanua chanzo cha mafanikio ya ujenzi wa nyumba akisema, “baada ya kupata mafunzo, tulipatiwa fedha tukanunua kuku, wakazaliana, na walipozaliana, FAO walituwezesha kupata mashine, japo ilichelewa kuanza kutumika. Lakini mwishowe tulifanikisha licha ya changamoto za umeme. Tuliwezesha kutotolesha vifaranga. Nilipopata shida niliuza kuku na changamoto niliyokuwa nayo ya ujenzi wa nyumba ikamalizika. Nyumba ilikamilika.”

Mnufaika huyu wa mradi wa KJP akaendelea kusema kuwa baada ya kumaliza ujenzi wa nyumba yake kutokana na ufugaji wa kuku, ameanza tena mzunguko mwingine wa ufugaji kuku.

“Hapa ndio nimeanza tena, tunataka tukusanye mayai na pia mchango wa kununua betri ya kuongezea kwenye mashine ili tuweke mayai kwa wingi tuone kama yatatotolewa.”

Ujumbe wake kwa wanawake wengine ni kwamba “kina mama wenzangu nawashauri wajifunze kufuga kuku, kwani hauhitaji mtaji mkubwa sana, ukinunua tu kuku mmoja ukamfuga baada ya muda wa miezi mitatu unashtukia mradi umeshapanuka.”

Wanufaika wa mradi wa Umoja wa Mataifa KJP mkoani Kigoma nchini Tanzania wanapatiwa stadi  na faida za kufuga kambale na sato kwenye bwawa moja kama njia ya kujipatia kipato na kutokomeza umaskini.
FAO Tanzania
Wanufaika wa mradi wa Umoja wa Mataifa KJP mkoani Kigoma nchini Tanzania wanapatiwa stadi na faida za kufuga kambale na sato kwenye bwawa moja kama njia ya kujipatia kipato na kutokomeza umaskini.

Umwagiliaji kwa manufaa ya kilimo na ufugaji

Kilimo bora na ufugaji bora vinataka pia uweko wa maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji mashamba halikadhalika kunywesha mifugo. Katika maonesho haya Abel Mpamba alileta mashine ya kuvuta maji ambayo hapa uwanjani pia inatumika kumwagilia mazao kama njia mojawapo ya kudhihirisha kile ifanyacho.

Bwana Mpamba anaeleza kuwa kwenye maonesho amewaletea wakulima na wafugaji pampu ya maji aina ya MoneyMaker ambayo ina uwezo wa kuvuta maji kutoka kwenye chanzo chochote cha maji iwe ni mto na kusafirisha kwenda kumwagilia shambani.

Amesema pampu hiyo ina uwezo wa kuvuta maji kutoka umbali wa mita 10 na kupeleka umbali wa mita 200.

Pampu hiyo ilikuweko kwenye maonesho ikitumiwa na wakulima ambapo Bwana Mpamba amesema katika kumwagilia ina uwezo wa kuvuta lita 60 kwa dakika moja.

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.