Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya FAO kuhusu viazi lishe yaleta imani mpya ya lishe na kipato Kigoma 

Kikundi cha wanawake mkoani Kigoma nchini Tanzania wakiwa kwenye mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za vyakula kwa kutumia viazi lishe.
FAO Tanzania
Kikundi cha wanawake mkoani Kigoma nchini Tanzania wakiwa kwenye mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za vyakula kwa kutumia viazi lishe.

Mafunzo ya FAO kuhusu viazi lishe yaleta imani mpya ya lishe na kipato Kigoma 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuelekea mkutano wa ngazi ya juu wa viongozi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mifumo ya chakula, huko mkoani Kigoma nchini Tanzania Umoja wa Mataifa umedhihirisha jinsi uboreshaji wa mbegu za mazao na mafunzo kwa wakulima juu ya kilimo bora na matumizi bora ya mazao vinaweza kuimarisha siyo tu lishe bali pia kuongeza kipato.
 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitisha mkutano huo ili kujadili na kupitisha uamuzi kuhusu mifumo endelevu ya chakula. Hii ni kwa kutambua kuwa kuna mnyororo mzima kuanzia mbegu ya zao la chakula inapooteshwa shambani hadi inapomfikia mlaji mezani. Umoja wa Mataifa unataka hatua sahihi ili zao linapotoka shambani siyo tu liongezwe thamani bali pia limfikie mlaji katika njia bora zaidi na manufaa mapana zaidi ya kiafya na kiuchumi

Watoto mkoani Kigoma wakifurahia uji uliopikwa kwa kutumia viazi lishe.
FAO Tanzania

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula FAO kupitia mradi wa Pamoja wa Kigoma, KJP wamepatia wakulima mafunzo ya mapishi ya viazi lishe na hivyo kuongeza mnyororo wa thamani kwa zao hilo ambalo wengi wamezoea kula kwa kuvichemsha pekee.

Mafunzo yamefanyika katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma ambapo wakulima, wanafunzi, maafisa ugani wa kilimo na lishe kwa kushirikiana na watafiti toka kituo cha utafiti Tumbi Tabora kwa ufadhili wa FAO chini ya mradi wa KJP walijumuika pamoja ili kupata mafunzo juu ya mazao mbalimbali yatokanayo na viazi lishe ambavyo vimeanza kupata sifa mkoani Kigoma baada ya FAO kuanzisha uzalishaji wa mbegu za viazi hivyo kwa kushirikiana na Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Kanimbwa lililopo ndani ya mkoa huo.

Siku hiyo ya pekee ikilenga kutambua umuhimu wa lishe katika katika kaya ilitanguliwa na mafunzo ya kutambua umuhimu wa viazi lishe na mazao mbalimbali yatokanayo na viazi hivyo na kisha baadaye kwa vitendo wakulima hao walishiriki kutengeneza mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na uji, juisi, chapati, maandazi na chipsi.

Mahuno Mussa ambaye ni Mkulima wa Halmashauri hiyo aliishukuru FAO kwa kuwapatia mafunzo ya uzalishaji wa viazi lishe na baadaye leo hii mafunzo ya kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na viazi hivyo walivyovuna.

“Nimefurahia sana mafunzo haya”,  alisikika Bi Adrofina Yohana ambaye ni mkulima kiongozi na alikuwa mshiriki katika tukio hilo. “Nitaendelea kutengeneza bidhaa mbalimbali nilizojifunza leo kama vile tambi, uji na chipsi na nitaendelea kutoa mafunzo kwa wenzangu, kuzaiisha zaidi na kufanya biashara ya bidhaa zitokanazo na viazi lishe”, aliongeza Bi Adrofina.
Wanafunzi wa shule ya msingi Bogwe kwa furaha baada ya kuonja mazao ya viazi lishe walijibu wito wa Mwalimu wao alipowataka washangilie viazi lishe.

Mafunzo ya FAO mkoani Kigoma yamewezesha wanakikundi kutumia viazi lishe kutengeneza juisi, na kupika maandazi, chapati na kukaanga chipsi.
FAO Tanzania

Naye Therezia Elia Charles mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Bogwe alielezea kwa ufupi waliyojifunza siku hii ikiwa ni pamoja na faida za viazi lishe katika mwili ambayo ni chanzo cha Vitamin A ambayo husaidia macho kuona vema.

Kwa upande wake Rehema Eliachomu mwanafunzi wa shule hiyo ya bogwe akifurahia somo la mapishi yatokanayo na viazi lishe alitoa ombi lake kwa FAO iwapatie mbegu ili waweze kuzalisha viazi lishe.

Afisa Kiungo wa Mradi wa Pamoja wa Kigoma Bwana Aron Masalu alipata fursa ya kuelezea chimbuko la mbegu hii ya viazi lishe na mwitikio uliopo katika ngazi mbalimbali ndani na nje ya Halmashauri na kukiri kwamba kwa msimu ujao wa kilimo wakulima wengi wamejipanga kupokea mbegu na kuzalisha viazi lishe.