Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante FAO kwa ziara hii ya mafunzo Kagera- Wakulima Kakonko

Mbuzi hawa ni matokeo ya matumizi ya mbinu bora za ufugaji mbuzi zinazofuatwa na wanufaika wa mradi unaofadhiliwa na FAO Tanzania.
FAO Tanzania
Mbuzi hawa ni matokeo ya matumizi ya mbinu bora za ufugaji mbuzi zinazofuatwa na wanufaika wa mradi unaofadhiliwa na FAO Tanzania.

Asante FAO kwa ziara hii ya mafunzo Kagera- Wakulima Kakonko

Malengo ya Maendeleo Endelevu

•    Mradi wa kopa mbuzi lipa mbuzi wanufaisha wakulima wafugaji Kagera
•    Ufugaji wa kisasa wachukua nafasi ya ufugaji holela
•    Baada ya mafunzo wakulima wa Kakonko nao kupatiwa mbuzi bora
 
Wakulima kutoka mkoani Kigoma wakiwa kwenye ziara ya mafunzo ya kilimo bora na ufugaji mbuzi katika mkoa jirani wa Kagera nchini Tanzania, ziara iliyoandaliwa na FAO Tanzania.
FAO Tanzania
Wakulima kutoka mkoani Kigoma wakiwa kwenye ziara ya mafunzo ya kilimo bora na ufugaji mbuzi katika mkoa jirani wa Kagera nchini Tanzania, ziara iliyoandaliwa na FAO Tanzania.

Ziara ya mafunzo ya wakulima wafugaji wa mkoani Kigoma nchini Tanzania waliyoifanya mkoani Kagera chini ya ufadhili wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO imewapatia matumaini ya kuweza kuoanisha shughuli za ufugaji na kilimo kama njia mojawapo ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDG, hususan yale ya kutokomeza umaskini, njaa na mabadiliko ya tabianchi.

Safari ya mafunzo ilihusisha wakulima wafugaji 20 toka wilaya ya Kakonko wakiongozwa na maafisa ugani watatu na mshauri wa FAO. Safari hii ya Mafunzo ilifadhiliwa na FAO kupitia Mradi wa Pamoja wa Kigoma, KJP.

Wakiwa Kagera hususan wilayani Muleba wakulima walipata mafunzo ya kinadharia na kivitendo na walitembelea wakulima wafugaji.

Miongoni mwa waliotembelewa ni mkulima mfugaji Alexander ambaye ameanza ufugaji baada ya kuona mafanikio ya ufugaji unaofanywa na wanufaika wa mradi uliofadhiliwa na FAO mkoani Kagera, mradi ambao ulianza katika mfumo wa Kopa mbuzi lipa mbuzi.

Wakulima kutoka Kigoma walijifunza kutoka kwa wenzao wa Kagera ujenzi bora wa mazizi ya mbuzi ili kufanikisha ukusanyaji wa samadi kwa ajili ya kilimo.
FAO Tanzania
Wakulima kutoka Kigoma walijifunza kutoka kwa wenzao wa Kagera ujenzi bora wa mazizi ya mbuzi ili kufanikisha ukusanyaji wa samadi kwa ajili ya kilimo.

Kisha Bi.Ndyanabo ambaye ambaye ni mnufaika wa  mradi wa mfuko wa jamii Tanzania, TASAF na akawaeleza kuhusu faida ya maziwa anayokamua kutoka kwa mbuzi aliopata kupitia mradi huo, huku akisema maziwa ya mbuzi pamoja na kuuza anatumia na familia yake.

Mwingine ni Charles Ngaiza ambaye ni mnufaika wa mradi uliokuwa umefadhiliwa na FAO Mkoani Kagera na ambaye alianza katika mfumo wa Kopa mbuzi lipa mbuzi.

Hivi sasa Bwana Charles amenufaika na mradi wa  mbuzi kwa kuweza kuongezea sehemu ya mapato yatokanayo na ufugaji kwa kujenga nyumba ya kisasa na kujinunulia chombo cha usafiri.

“Nimeweza pia kupata ada ya kulipia watoto shuleni, lakini pia maziwa kwa matumizi ya familia na samadi kwa ajili ya kurutubisha shamba letu. Hebu tazama migomba hii ambayo ninatumia samadi ya mbuzi,” amesema Bwana Ngaiza.

Msaidizi wa Mkuu wa Chuo  cha Igabiro Sydney Stephen ambacho hutoa mafunzo kwa maafisa ugani wa kilimo na mifugo  akielezea faida za mifugo aina ya mbuzi amesema, “ mbali na maziwa na nyama, mifugo hutoa samadi ambayo hutumika katika kilimo cha bustani na kusababisha kupata mavuno mazuri kama vile mboga na matikiti maji.”

Akifurahia mafanikio ya safari ikiwa ni pamoja na kuleta mabadiliko toka kwenye ufugaji holela na kufuga kitaalamu, mwenyekiti wa Kikundi cha Wakulima Laurent Michael amesema wamejifunza ujenzi wa mabanda, ulishaji na ukamuaji. Na pia amefurahia  kujifunza uhusiano uliopo baina ya  mifugo na kilimo hususani bustani.

Wakulima kutoka mkoani Kigoma wakiwa kwenye ziara ya mafunzo ya kilimo bora na ufugaji mbuzi katika mkoa jirani wa Kagera nchini Tanzania, ziara iliyoandaliwa na FAO Tanzania.
FAO Tanzania
Wakulima kutoka mkoani Kigoma wakiwa kwenye ziara ya mafunzo ya kilimo bora na ufugaji mbuzi katika mkoa jirani wa Kagera nchini Tanzania, ziara iliyoandaliwa na FAO Tanzania.

Mtaalamu wa Mifugo toka wilaya ya Kakonko  Revelian Rushehela aliyeongozana na wakulima alikiri kwamba, safari hii ya mafunzo imekuja wakati muafaka na itakuwa ya manufaa makubwa kwa wafugaji wa Kakonko baada ya kuona kwa vitendo toka kwa wafugaji wenzao ambao tayari walishapatiwa mafunzo na FAO.

“Sasa wanasubiri kupatiwa mbuzi bora chini ya mradi wa KJP kwa ajili ya kuendeleza na kukuza kizazi cha asili cha mbuzi wa kienyeji ili kuwa na ufugaji wenye tija,” amesema Bwana Rushehela. Akitaja baadhi ya mafanikio waliyoyaona kuwa ni pamoja na faida za ufugaji wa ndani ikiwa ni pamoja na udhibiti wa magonjwa, na udhibiti wa upotevu wa samadi na wanyama wanakula na kushiba.