Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO imetuondoa wanawake kwenye utegemezi- Mkulima kigoma

Wanakikundi wa Umoja  ni nguvu  na Mshikamano  A  Kata ya Katanga wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, wakichambua maharage aina ya Jesca yenye virutubisho asilia vya madini ya chuma, kutoka shamba darasa lao lililofanikishwa na mafunzo ya mradi wa pamoja wa
FAO Tanzania
Wanakikundi wa Umoja ni nguvu na Mshikamano A Kata ya Katanga wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, wakichambua maharage aina ya Jesca yenye virutubisho asilia vya madini ya chuma, kutoka shamba darasa lao lililofanikishwa na mafunzo ya mradi wa pamoja wa Kigoma wa UN kupitia FAO.

FAO imetuondoa wanawake kwenye utegemezi- Mkulima kigoma

Wanawake

Nchini Tanzania hususan mkoani Kigoma, mafunzo ya kilimo hifadhi yanayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO nchini humo yamejengea uwezo wanawake na sasa wana uwezo sio tu wa kukidhi mahitaji yao bali pia kulipa gharama za pembejeo za kilimo.

Mafunzo hayo yanayoendana na kupatia wakulima stadi za kisasa za kilimo, matumizi ya mbegu za kisasa zinazohimili mabadiliko ya tabianchi pamoja na matumizi ya samadi yamejengea uwezo wakulima kama vile Grace Jackson Ntaziha, mkazi wa kijiji cha Kitahana, kilicho kata ya Kitahana, wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Mkulima huyu mnufaika wa mafunzo ya FAO akiwa anapura mahindi aliyovuna anatanabaisha kuwa mavuno ya mwaka huu wa 2022 ni bora kuliko ya mwaka jana kwa sababu ya mbegu ya Njano Uyole waliyopatiwa na FAO.

Bi. Ntaziha anakiri kuwa mbegu ya Njano Uyole imekuwa nzuri kuliko mbegu aina ya Yamungu ambayo haikuwafaa. “Wakulima kupitia chama cha ushirika cha Kitahana, tumepata bahati ya kulima eka 40 na kila mkulima ana uhakika wa kupata fedha ya kulipa deni la pembejeo na kubakia na masalia ya fedha anayoweza kujikimu na pia kusomesha watoto.”

Wanawake tuondokane na fikra za utegemezi kwa wanaume

Wakati huu ambapo dunia inaelekea kuadhimisha siku ya wanawake duniani tarehe 8 mwezi huu wa Machi ujumbe ukiwa Usawa wa kijinsia kwa mustakabli bora, Bi. Ntaziha anapaza sauti kwa wanawake ili waondokane na utegemezi na kuwa imara kiuchumi.

“Ushauri wake ni kwamba wanawake wenzangu wajiunge na vikundi ili wapate mbinu bora za kilimo cha kisasa ili hatimaye waondokane na kero za kila siku za kuwa na fikra za utegemezi kwa akina baba. Ukijiunga na vikundi vya ushirika na vile vya kilimo lazima utapata fedha za kujikimu kwa mahitaij mbalimbali,” amefafanua Bi. Ntaziha.

Maharage ya Njano Uyole ni zaidi ya uwezeshaji kiuchumi

Wakulima akiwemo Bi. Ntaziha pamoja na kuuza maharage kupata fedha, pia wanatumia kwenye mlo ambapo kwa mujibu wa FAO maharage haya yana virutubisho vyenye faida mwilini kuanzia kwa watoto hadi wajawazito kwa sababu yana protini.

Halikadhalika kwa upande wa udongo yanarutubisha udongo na pia yanakomaa mapema, na kuvumilia magonjwa.

Mafunzo haya ya kilimo hifadhi yanatolewa na FAO chini ya mradi wa pamoja wa Kigoma, KJP unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo FAO.

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.