Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UN linaitaka Urusi kubatilisha jaribio la kunyakua maeneo manne ya Ukraine

Mtazamo wa ndani ya Baraza Kuu wakati wa kikao cha 11 cha dharura kuhusu Ukraine
UN Video
Mtazamo wa ndani ya Baraza Kuu wakati wa kikao cha 11 cha dharura kuhusu Ukraine

Baraza Kuu la UN linaitaka Urusi kubatilisha jaribio la kunyakua maeneo manne ya Ukraine

Amani na Usalama

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio siku ya Jumatano linaloitaka Urusi kubatilisha "jaribio lake la kutaka kunyakua kiharamu maeneo manne ya Ukraine kufuatia kinachojulikana kama kura za maoni za kinyume cha sheria".

Maandishi ya azimio hilo yenye kichwa "Uadilifu wa eneo la Ukraine: utetezi wa kanuni zilizowekwa katika mkataba wa Umoja wa Mataifa", ilipitishwa kwa kura 143 za ndio kwa, 5 dhidi  ya azimio hilo na wanachama 35 walijizuia kupigia kura azimio ambalo sio la lazima.

Baraza Kuu limefanya mjadala kuhusu rasimu ya azimio hilo baada ya Urusi kutumia kura yake ya turufu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu jaribio lake la kutaka kutwaa mamlaka hiyo.

Mjadala huo ulianza Jumatatu, huku Rais wa Baraza Kuu Csaba Kőrösi akitoa wito wa "kupatikana suluhu ya kisiasa kwa kuzingatia mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa".

Katika utangulizi, azimio hilo linabainisha kuwa maamuzi yaliyochukuliwa na Shirikisho la Urusi mwezi Februari  tarehe 21 na Septemba 29, 2022 kuhusu hali ya mikoa ya Ukraine ya Donetsk, Kherson, Luhansk na Zaporizhia "Ni ukiukaji wa uadilifu wa eneo na uhuru wa Ukraine. " na kukiuka kanuni za mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Taswira ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Katibu Mkuu António Guterres alipohutubia ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa UNGA77
UN /Cia Pak

Kura haramu ya maoni

Baraza Kuu pia limebainisha kwa wasiwasi kwamba "kinachojulikana kama kura za maoni haramu zilifanyika katika mikoa hii kutoka tarehe 23 hadi 27 Septemba 2022 katika jaribio la kubadilisha mipaka inayotambulika kimataifa ya Ukraine" na inazingatia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa mwezi Septemba tarehe 29, 2022, ambapo Umoja huo ulikumbusha kwamba unyakuzi wowote wa eneo la nchi na serikali nyingine kutokana na matumizi au tishio la matumizi ya nguvu ni ukiukaji wa kanuni zilizowekwa na mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Katika muktadha huu, Baraza Kuu "Linalaani shirikisho la Urusi kwa maandalizi ya kile kinachoitwa kura ya maoni haramu katika mikoa iliyo ndani ya mipaka inayotambulika kimataifa ya Ukraine na jaribio la kunyakua kwa njia haramu mikoa ya Kiukreni ya Luhansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhya iliyofuata".

Jengo lililoharibiwa vibaya Ukraine
© UNICEF/Anton Kulakowskiy

Hakuna uhalali chini ya sheria ya kimataifa

Azimio hilo linasema kwamba "Vitendo haramu vya shirikisho la Urusi kuhusu kile kinachoitwa kura ya maoni haramu iliyofanyika kuanzia Septemba 23 hadi 27, 2022 katika sehemu za mikoa ya Kiukreni ya Donetsk, Kherson, Luhansk na Zaporizhia ambayo ni au inapatikana kwenye sehemu iliyo chini ya udhibiti wa kijeshi wa muda wa shirikisho la Urusi na jaribio la baadaye la kunyakua maeneo haya haina uhalali chini ya sheria za kimataifa na haiwezi kutumika kama msingi wa mabadiliko yoyote katika hali ya mikoa hii ya Ukraine".

Baraza Kuu "linatoa wito kwa mataifa yote, mashirika ya kimataifa na mashirika maalum ya Umoja wa Mataifa kutotambua marekebisho yoyote ya shirikisho la Urusi ya hadhi ya mikoa yote au sehemu ya Ukraine ya Donetsk, Kherson, Luhansk na Zaporizhia na kujiepusha na kitendo chochote au mgusano unaoweza kutafsiriwa kama kukiri uhalali wa mabadiliko hayo”.

Baraza kuu linataka Shirikisho la Urusi "Mara moja na bila masharti kubatilisha maamuzi iliyochukua Februari 21 na Septemba 29, 2022 kuhusu hali ya maeneo fulani ya mikoa ya Ukraine ya Donetsk, Kherson, Luhansk na Zaporizhia na kwamba mara moja, iondoe vikosi vyake vyote vya kijeshi bila masharti katika eneo la Ukraine ndani ya mipaka ya nchi inayotambulika kimataifa".