Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi watoa maoni yao baada ya uamuzi wa Baraza Kuu la UN dhidi ya Urusi

Jengo lililoharibiwa katikati mwa Kharkiv, Ukraine.
© UNOCHA/Matteo Minasi
Jengo lililoharibiwa katikati mwa Kharkiv, Ukraine.

Viongozi watoa maoni yao baada ya uamuzi wa Baraza Kuu la UN dhidi ya Urusi

Amani na Usalama

Vita ya Ukraine ikiwa inaingia mwaka wake wa pili, wawakilishi mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wametoa maoni yao kufuatia uamuzi kwa njia ya kura uliofanywa na Kikao Maalumu cha  dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio jipya la kutaka amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine na kwamba Urusi bila masharti yoyote iondoe mara moja majeshi yake katika ardhi ya Ukraine. 

Umaalumu wa kikao hiki cha siku mbili kilichokamilika jana jijini, New York, Marekani ni kwa mujibu wa azimio lilipotishwa mwaka 1950 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba Baraza hilo linaweza kushughulikia masuala ya kimataiafa yanayohusu amani na usalama pale ambapo Baraza la Usalama linakuwa limeshindwa kufanya hivyo.

Kwa msingi huo kutokana na mara kwa mara Urusi kutumia kura ya turufu katika Baraza la Usalama kuzuia uamuzi wa kuibana,  ndipo kikao hiki cha Baraza Kuu kikaitishwa kwa siku mbili Jumatano na Alhamis katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ili nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wapige kura kuiambia Urusi iondoke Ukraine. 

Awali kabla ya azimio kupigiwa kura, Vassily Nebenzia Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa kufanya uamuzi kwa kuangalia tu yaliyotokea Februari 24 mwaka jana 2022 ni jaribio la makusudi la nchi za Magharibi kuficha sababu za kweli za mzozo huo. Hata hivyo matokeo ya kura yakaonesha kuwa walioinga mkono Urusi ni nchi 7 tu, 31 zikionesha kutokuwa upande wowote huku 141 zikiliunga mkono Azimio. Vita ikome, Urusi iondoke Ukraine. 

Dmytro Kuleba (mezani), Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa Ukraine.
UN Photo/Evan Schneider
Dmytro Kuleba (mezani), Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa Ukraine.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, mara tu baada ya kupitishwa kwa azimio… anasema “nchi yangu imeridhika na matokeo na ujumbe uko wazi; Haijalishi ni nini Urusi inajaribu na jinsi inavyojaribu kudhoofisha utaratibu wa kimataifa, inashindwa kila mara.” 

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa aliwasisitizia wajumbe akisema, “uchokozi ni kinyume cha sheria. Kumvamia jirani ni kinyume cha sheria. Kujimegea kipande cha nchi nyingine ni kinyume cha sheria.” 

Miongoni mwa nchi 32 ambazo zimepiga kura isiyoonesha kama zinaunga mkono azimio au la pamoja na Burundi, Msumbiji, Ethiopia, Congo, Zimbabwe, Afrika Kusini, China, India na Pakistan.  

Na zile ambazo zimeiunga mkono Urusi kwa kulipinga azimio hilo la kumaliza vita Ukraine ni Belarus, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Eritrea, Mali, Nicaragua, Urusi yenyewe na Syria.