Skip to main content

Baraza lapitisha azimio moja kuhusu ubinadamu Ukraine huku lingine likitupiliwa mbali

Misaada ya kibinadamu ikiwasili eneo la Sumy nchini Ukraine tarehe 18 Machi 2022
© UN/Ukraine
Misaada ya kibinadamu ikiwasili eneo la Sumy nchini Ukraine tarehe 18 Machi 2022

Baraza lapitisha azimio moja kuhusu ubinadamu Ukraine huku lingine likitupiliwa mbali

Msaada wa Kibinadamu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio hii leo limepitisha kuhusu madhara ya kibinadamu yatokanayo na uvamizi dhidi ya Ukraine ambapo azimio hilo linatilia mkazo misingi ya utu, kutoegemea upande wowote na uhuru katika kutoa misaada ya kibinadamu.
 

Azimio hilo namba A/ES11/L.2 lililowasilishwa na Ukraine limepigiwa kura ya Ndio na nchi 140 huku 5 ikiwemo Urusi zikipinga na 38 ikiwemo Tanzania hazikupiga kura katika kikao hicho cha 9 cha mkutano wa 11 wa dharura wa Baraza hilo Kuu la Umoja wa Mataifa.

Likiwa na vipengele 14, azimio hilo pamoja na mambo mengine linasisitiza umuhimu wa utekelezaji wa azimio namba A/ES-11/1 la tarehe 2 mwezi Machi mwaka huu wa 2022 likipatiwa jina Uvamizi dhidi ya Ukraine.

Matokeo ya kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu azimio la ubinadamu Ukraine.
UN WebTV
Matokeo ya kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu azimio la ubinadamu Ukraine.

Azimio linataka pia sitisho la chuki za Urusi dhidi ya Ukraine hususan mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia huku ikitaka raia, wakiwemo wahudumu wa kibinadamu, waandishi wa habari na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi wakiwemo wanawake na watoto walindwe kwa ukamilifu.

Baraza pia kupitia azimio hilo limemtaka Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu awasilishe ripoti ya hali nchini Ukraine na hatua za kibinadamu kwa mujibu wa azimio namba A/ES-11/2 na limemuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aendele kupatia ripoti mara kwa mara chombo hicho kuhusu utekelezaji wa azimio hili la leo.

Masuala mengine ni nchi wanachama kuendelea kuchangia ombi la kimataifa la kusaidia Ukraine.

Vuta nikuvute Barazani

Mbele ya Baraza, wajumbe walikuwa wamepatiwa maazimio mawili, A/ES-11/L.2 likiwasilishwa na Marekani na washirika wake na  A/ES-11/L2 likiwasilishwa na Afrika Kusini.

Mara baada ya Mwenyekiti wa kikao kutangaza hatua ya kupigia kura maazimio hayo kwa mujibu wa yalivyowasilishwa barazani, wajumbe walipigia kura azimio namba A/ES-11/L.2 lililowasilishwa na Marekani na washirika wake ambapo lilipitishwa kwa kura 140 huku 5 zikipinga na 38 hazikupiga kura.

Mkazi huyu wa mji wa bandari wa Mariupol nchini Ukraine akitazama bila kuamini jinsi nyumba yake ilivyosambaratishwa kwa mabomu, kusini-mashariki mwa taifa hilo.
© UNICEF/Evgeniy Maloletka
Mkazi huyu wa mji wa bandari wa Mariupol nchini Ukraine akitazama bila kuamini jinsi nyumba yake ilivyosambaratishwa kwa mabomu, kusini-mashariki mwa taifa hilo.

Kisha Mwakilishi wa kudumu wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Sergiy Kyslytsya akaomba fursa ya kuzungumza na kutaka azimio la pili namba A/ES-11/L.3 lisizingatiwe kwenye Baraza, akimaanisha lisipigiwe kura.

Mwenyekiti aliwasilisha hoja na kisha kutaka wajumbe wapiga kura kuamua iwapo lizingatiwe au la.

Matokeo ya kura ni kwamba wajumbe 67 walipiga kura ya Hapana ya kwamba litupiliwe mbali ilihali 50 ikiwemo Urusi wakitaka lizingatiwe huku nchi 36 hazikupiga kura kabisa.

Mwenyekiti akatangaza matokeo yakionesha kuwa azimio hilo limetupiliwa mbali.

Maoni ya wajumbe

Wajumbe walipatiwa fursa ya kuzungumza kuhusu uamuzi wa kura yao ambapo Rwanda ilisema imeunga mkono kwa kutambua umuhimu wa usaidizi wa kibinadamu kwa wananchi wa Ukraine.

“Hata hivyo lazima tutambua kuwa Urusi na Ukraine ndio wameshikilia ufunguo na kufuli ya mzozo huo kwa hiyo wao ndio wa kumaliza mzozo huu,” alisema mjumbe kutoka Rwanda.

Malaysia kwa upande wake ilisema haikupiga kura kuonesha msimamo wowote kwa sababu inahoji “kwa nini waandishi wa maazimio hayo mawili hawakuketi pamoja na kuandika nyara moja?. Hii inaonesha ni kwa jinsi gani hatuko kitu kimoja kusaidia wale walio kwenye janga.”

“Sisi tumeamua kutopigia kabisa kura azimio lililopitishwa,” alisema mjumbe wa Laos, “kwa sababu azimio la kibinadamu linapaswa kuungwa na wajumbe wote na halipaswi kuwa na misingi ya kisiasa.”

Hata hivyo Laos imesema inapongeza hatua za mashauriano zinazoendelea kati ya pande kinzani ambazo ni Ukraine na Urusi ikisema suluhu pekee ni kwa njia ya mazungumzo.

Kikao kimeahirishwa huku azimio likitaka Rais wa Baraza Kuu aitishe kuhusu mada ya Ukraine kadri ambavyo ataona inafaa.