Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Benki ya Dunia Msumbiji waleta nuru kwa familia zilizokata tamaa 

Wanachama wa kikundi cha Nathelaca, wanufaika wa mradi wa Benki ya Dunia wa Usimamizi wa  Ardhi wakipanda miti kwenye shamba lao la kijamii.
Benki ya Dunia
Wanachama wa kikundi cha Nathelaca, wanufaika wa mradi wa Benki ya Dunia wa Usimamizi wa Ardhi wakipanda miti kwenye shamba lao la kijamii.

Mradi wa Benki ya Dunia Msumbiji waleta nuru kwa familia zilizokata tamaa 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Msumbiji, Benki ya Dunia inatekeleza mradi wa usimamizi bora wa ardhi, ILM,  unaolenga siyo tu kupanda miti na kulinda mmomoyoko bali pia kujenga usawa wa kijinsia, mradi ambao tayari umeanza kuzaa matunda huko jimboni Zambezia. 

Benki ya Dunia inasema Msumbiji ni moja ya nchi chache za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo bado zina maeneo yaliyofunikwa na misitu. Misitu ya asili inafunika asilimia 43 ya taifa hilo na kuchangia katika bayonuai na manufaa ya kiuchumi na kijamii, miongoni mwa machache. 

Hata hivyo ukataji holela wa misitu na mmomonyoko wa ardhi vinatishia bayonuai na mbili za wakazi wa vijijini kujipatia kipato. 

Mradi wa huo wa Benki ya Dunia unaanza kuwa jawabu ya vitendo hivyo vinavyotishia uwepo wa misitu na mbinu za kujipatia kipato. 

Victoria Duerte, Rais wa Kikundi cha Nathelaca nchini Msumbiji ambacho kimenufaika na mradi wa usimamizi wa ardhi unaotekelezwa na Benki ya Dunia.
Benki ya Dunia
Victoria Duerte, Rais wa Kikundi cha Nathelaca nchini Msumbiji ambacho kimenufaika na mradi wa usimamizi wa ardhi unaotekelezwa na Benki ya Dunia.

Mradi waenda kujibu hofu ya ‘majuto mjukuu’ 

Sasa mradi unatekelezwa jimboni Zambezia na video ya Benki ya Dunia inafuatilia wanufaika na miongoni mwao ni wakazi wa Alto Molocue  jimboni Zambezia ambako Victoria Duarte akiwa anatembea shambani anasema ni vigumu kupata kuni, ni vigumu kujenga nyumba! Eneo hili ni mchanga mtupu kwa sababu ya miti yote tuyliyokata! 

Ni sawa na kusema majuto ni mjukuu kwa mwanamke huyu wa kijijini ambaye anasimulia hali ilivyokuwa. Lakini Benki ya dunia ikaja na mradi wa kuwaondoa kwenye mawazo ya siyo tu kupata nishati bali pia kuweza kujipatia kipato. 

Bi. Duarte ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha kupanda miti cha Nathelaca anasema tulitakiwa kupanda miti ili udongo uweze kusalia na unyevunyevu. Video inawaonesha akiwa shambani na wanawake wengine huku wakipanda mitin a kuweka mbolea.  

Mradi wawezesha upandaji miti kibiashara 

Mradi huo wa Uwekezaji kwenye misitu unawawezesha kupanda miti ya kibiashara na wakati huo huo kurutubisha ardhi. 

Bi. Duarte anasema, “kwanza tulipanda miti kwenye eneo hili la majaribio, na kisha kila mmoja akaenda kupanda kwenye eneo lake. Na tulisaidiana kupanda kwenye kila shamba la mwanakikundi hadi tulipomaliza. Kwa ujumla tukijumlisha tumepnda miti katika jumla ya ekari 33. ” 

Shughuli za upandaji miti kutoka shamba moja hadi lingine inafanyika kwa furaha kila mwanachama akiwa amebeba mche huku wakiimba! 

Faida sasa ni dhahiri kwa wakazi wa Zambezia 

Bi Duarte anasema,“sasa hivi tuko kwenye maeneo. Tuko jumla ya wanachama 19 tukiwa na mashamba ya mikaratusi. Hadi leo hii tuna mipango ya kuweka akiba, miradi ya kilimo na ya upandaji miti.” 

Sasa wako shambani wanawake kwa wanaume wakiwa na kiongozi akiwaelekeza jinsi ya kupanda miti na anasema,“lazima tutunze miti yetu. Kwa ajili ya matumizi yetu nyumbani, kwa ajili ya kuuza na pia tuweze kuweka akiba na kutimiza ndoto zetu. Kila mmoja ana kitabu ambamo anaandika ndoto zake. Lengo ni kuona kuwa kile ulichoandika napaswa kufanikisha, na je nitafanikisha vipi? Kupitia miti yetu, mashamba yetu ambamo tunapanda mahindi, ufuta, maharagwe ya soya, badala ya kutumia tu fedha.” 

Mradi huu pia unajumuisha kipengele cha jinsia, GALS ambamo familia zinafundishwa jinsi ya kubaini vikwazo vya maendeleo na kusonga pamoja kwa ajili ya kujipatia kipato.  

Sasa Bi. Duarte yuko darasani anafundisha wanawake kwa wanaume juu ya masuala ya jinsia akiwahoji, nyumbani kati ya mwanamke na mwanaume nani anafanya kazi zaidi? 

Anawaambinadhani kuna kazi ambazo mwanamke anaweza kufanya akisaidiwa na mwanaume! 

Mwanachama wa kikundi cha Nathelaca nchini Msumbiji kilichonufaika na mradi wa Benki ya Dunia wa  usimamizi wa ardhi akipanda mti.
Benki ya Dunia
Mwanachama wa kikundi cha Nathelaca nchini Msumbiji kilichonufaika na mradi wa Benki ya Dunia wa usimamizi wa ardhi akipanda mti.

Kipengele cha jinsia na uwekezaji kwenye misitu ni ‘Zinduna na Ambari’ 

Kipengele cha jinsia na uwekezaji kwenye misitu kwa pamoja vimo kwenye mradi wa usimamizi wa ardhi, ILM, unaotekelezwa na Benki ya Dunia. Afrika Olojoba, Meneja wa mradi huo kutoka Benki ya Dunia anafafanua zaidi. 

Bwana Olojoba anasema, “ILM inatambua suala la jinsia kuwa ni suala mtambuka la miradi yote. Na kwa sababu hiyo, tunajumuisha suala la jinsia kwenye operesheni zetu zote. Suala hilo ni muhimu sana kwa kuzingatia tofauti ya umiliki wa mali. Hivyo ILM inawajumuisha wanawake katika  kuamua kipi ni kizuri kwao na kwa vipi wanaweza kusimamia rasilimali pamoja. Na  umuhimu hapa si kwamba inawezesha wanawake pekee, bali inaweka rasilimali mezani na kuwapatia fursa za ajira.” 

Kwa mujibu wa Benmi ya Dunia, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Msumbiji wanategemea maliasili, lakini maliasili hizo zinamomonyolewa. Kwa hiyo mradi wa ILM unashughulikia uharibifu huu wa ardhi, umaskini wa vijijini, haki za vijijini na usimamizi wa ardhi.” 

Anatamatisha akisema,  “na hapa ndio tunashirikiana kwa uthabiti na serikali na tuko hapa kusaidia programu ya serikali ya Maendeleo endelevu.” 

Sasa mambo ni mazuri na kikundi cha Nathelaca kinachoongozwa na Bi. Duarte,  hakikati tena miti bali kinapanda miti!