WFP yahitaji fedha zaidi kufanikisha operesheni zake Msumbiji

16 Aprili 2019

Mwezi mmoja tangu kimbunga Idai kipige Msumbiji na kusababisha maafa, shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema limeweza kufikisha msaada wa chakula kwa watu milioni mmoja huku likiendelea kupanua wigo wa msaada na kuwapatiwa wananchi misaada ya kujikwamua. 

WFP imesema inawapatia wahusika mgao wa siku 30 wa mchele pamoja na unga wa mahindi, maharagwe, vyakula vilivyoongezewa virutubisho pamoja na mafuta.

Karin Manente ni Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Msumbiji na anasema,

 (Sauti ya Karin Manente)

 “Sasa tumefanikiwa kuwafikia watu milioni moja , hayo ni mafanikio makubwa sana kwetu, na muhimu sana kwa watu wa Msumbiji ambao ndio waathirika wakubwa wa kimbunga IDAi. Sasa hivi unasikia mngurumo wa helikopta zetu zikiwapelekea watu ambao wapo katika maeneo yasiofikika kwa barabara.”

Tayari WFP imesambaza wataalamu wa lishe kwenye majimbo manne muhimu ambapo wanaanza kutoa matibabu dhidi ya utapiamlo na mpango ni kutibu takribani watoto na wanawake 100,000 katika kipindi cha miezi sita.

Hata hivyo msemaji huyo ameeleza ili mpango wao huo wa kupanua wigo wa huduma uweze kufanikiwa hadi mwezi Juni, wanahitaji dola milioni 130, huku akishukuru wahisani ambao tayari wamejitolea kufanikisha operesheni za awali nchini Msumbiji kufuatia kimbunga Idai.

Ili kufanikisha operesheni zake, WFP ilipeleka helikopta tatu za usafirishaji, ndege moja pamoja na magari mawili yanayotembea kwenye maji ambayo yana uwezo wa kubeba tani 1000 za mzigo kama vile chakula na kufikisha maeneo ambayo hayafikiki kwa barabara.

WFP inasema kwa kuzingatia kiwango kikubwa cha uharibifu,  mipango ya kuhakikisha Msumbiji inajikwamua itakuwa ni muhimu.

Ni kwa mantiki hiyo, shirika hilo linahaha kuhakikisha kuwa tathmini kubwa inayoongozwa na serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia inaanza wiki hii ili kupatia nchi hiyo mipango bora zaidi ya lishe, chakula na uhifadhi wa jamii.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter