Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1.2 zachangwa kwenye mkutano wa ufadhili Msumbiji

Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi akiwa na wanafunzi mara baada ya mkutano wa kimataifa wa wahisani kwa ajili ya nchi yake.
@UN Msumbiji
Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi akiwa na wanafunzi mara baada ya mkutano wa kimataifa wa wahisani kwa ajili ya nchi yake.

Dola bilioni 1.2 zachangwa kwenye mkutano wa ufadhili Msumbiji

Msaada wa Kibinadamu

Jumla ya dola bilioni 1.2 zimechangishwa mjini Beira katika mkutano wa kimataifa wa siku mbili wa ufadhili kwa ajili ya ujenzi mpya wa kijamii, uzalishaji na mioundombinu nchini Msumbiji baada ya taifa hilo kuathirika vibaya na vimbunga mapema mwaka huu.

Msumbiji inahitaji dola bilioni 3.2 kwa ajili ya kuyasaidia majimbo yaliyosambaratishwa vibaya na kimbunga Idai na Kenneth ya Sofala, Manica, Tete, Zambezia, Inhambane, Nampula na Cabo Delgado.

Katika mkutano huo wa kimataifa ulioandaliwa na serikali ya Msumbiji na kuwezeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP, Muungano wa Ulaya na Benko ya Dunia miongoni mwa waliochangia kiasi kikubwa cha fedha ni Muungano wa Ulaya ambao umetoa dola milioni 200, kati ya hizo dola milioni 100 zinatoka mfuko wa tume ya Muungano wa Ulaya na milioni 100 zingine kutoka Benki ya uwekezaji ya Ulaya.

Chumba kilichofanyika mkutano wa wahisani wa kimataifa mjini Beira Msumbiji kuchangisha fedha za ujenzi mpya
@UN Msumbiji
Chumba kilichofanyika mkutano wa wahisani wa kimataifa mjini Beira Msumbiji kuchangisha fedha za ujenzi mpya

Ujumbe wa Katubu Mkuu mkutanoni

Katika mkutano huo uliowaleta pamoja takribani washiriki 700 kutoka mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Msataifa Antonio Guterres uliosomwa kwa niaba yake umesema pamoja na mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF kutoa dola milioni 24 hapo awali na hata Umoja wa Mataifa kuzindua ombi la msaada wa kibinadamu la dola milioni 282 ambalo limefadhiliwa kidogo sana bado mamilioni ya watu Msumbiji wanahitaji msaada”tunakabiliwa na changamoto kubwa, mahitaji ya msingi ya watu hayafikiwi, hatari ya kulipika magonjwa iko dhahiri na athari kubwa za kutokuwepo na uhakika wa chakula ziko bayana kutokana na kupotea kwa mazao wakati wa vimbunga.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Guterres amewashukuru wote waliotoa changia na kurejelea wito wake wa ukarimu zaidi kutoka jumuiya ya kimataifa , akisema “Huu ni wakati wa kudhihirisha mshikamano wetu na nchi ambayo imeathirika na moja ya majanga makubwa na mabaya kabisa yahusianyo na hali ya hewa katika historia ya Afrika, majanga ambayo pia yanatuonya kuhusu kuchukua haraka hatua za kupambana na mabadiliko ya taifa nchi.”

Katibu Mkuu pia ameahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaongeza juhudi za kushughulikia athari za muda mfupi na za muda mrefu za majanga, na kwamba msaada wa dharua wa kibinadamu sasa utageuka polepole na kuwa wa ujenzi mpya na kusaidia juhudi za serikali za kuisongesh

a nchi hiyo katika masuala ya maendeleo.”Ujumbe wangu uko bayana Umoja wa Mataifa asilani hautoipa kisogo Msumbiji.”