Utu na maendeleo vyakutanishwa Coranne na kuleta ustawi kwa wakimbizi na wenyeji
Utu na maendeleo vyakutanishwa Coranne na kuleta ustawi kwa wakimbizi na wenyeji
Charlotte Fatuma na Neema Cenga ni wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na sasa wanaishi ukimbizini nchini Msumbiji katika jimbo la Nampula. Kwa sasa Charlotte ni mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, akiendesha biashara ya duka kwenye makazi ya wakimbizi ya Coranne huku Neema naye akijitahidi kulea na kusomesha watoto wake.
Wanawake wote hawa wawili ni wanufaika wa mradi wa kusambaza umeme unaofanikishwa kwa ubia kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB na serikali ya Msumbiji Mradi unalenga kusambaza umeme kwa wakimbizi wa ndani walioko kambini na wakati huo huo kunufaisha pia wenyeji. Hapa ni sawa na kuua ndege wawili kwa jiwe moja.
Charlote alikimbia DRC miaka 7iliyopita kutokana na ghasia na sasa hapa ni mjasiriamali mwenye duka lenye nishati ya umeme na anasema, “ninapouza bidhaa zenye thamani ya Meticais 1,000 ninanunua umeme wa thamani hiyo hiyo ya elfu moja na ninautunza, kwa sababu ninaumia sana pale ambapo ninashindwa kuuza bidhaa zangu kwa sababu hakuna umeme.”
Meticais 1000 ni sawa na dola 16 za kimarekani.
UNHCR na wadau wa maendeleo na kiutu wameleta neema Coranne
Kwenye video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Charlotte anaonekana akipanga vinywaji ndani ya jokofu, na UNHCR inasema alikimbia DRC miaka 7 iliyopita kutokana na ghasia nchini mwake.
Sasa kwenye duka lake hili anauzia wenyeji na wakimbizi vinywaji baridi na bidhaa nyingine za nyumbani ili aweze kuhudumia familia yake.
Charlotte anasema duka lake lilipounganishwa kwenye umeme wa gridi ya taifa, mambo mengi yalibadilika akifafanua, “Iwapo hutawasha umeme, kila kitu ni giza. Wateja hawawezi kuingia hapa kununua bidhaa iwapo huna umeme.”
Katika kambi hii ya wakimbizi wa ndani ya Coranne, milingoti ya umeme imesambaa huku na kule, na hii ni matokeo ya kazi ya UNHCR kwa ushirikiano wa serikali ya Msumbiji na wadau wake wa maendeleo ya kusambaza huduma ya umeme kwenye eneo hili la Msumbiji.
Irene Omondi ni afisa wa UNHCR hapa kambini na anasema,“kambi ya wakimbizi ya ndani ya Coranne ni mfano mzuri ambako unashuhudia matokeo ya ushirikiano wa kazi za usaidizi wa kibinadamu na maendeleo. Kambi hii ina manufaa ya usambazaji wa huduma za umeme kama uonavyo, ambapo nyumba zimeunganishwa na huduma ya umeme.”
Mabadiliko ya tabianchi na mizozo bado ni mwiba kwa Msumbiji
UNHCR inasema Msumbiji ni sawa na miongoni mwa dharura zisizoonekana. Mzozo wa mapigano na mashambulizi unaoendelea kaskazini mwa nchi hiyo pamoja na madhara ya mabadiliko ya tabianchi vimefurusha zaidi ya watu milioni moja kutoka kwenye makazi yao. Pamoja na hayo taifa hilo ni nyumbani kwa wakimbizi 29,000.
Kimbunga Gombe kilipopiga taifa hilo mwezi Machi mwaka huu wengi waliathirika, miongoni mwao Neema Cenga anayesema, “mimi nilikuwa nyumbani upepo ulipopiga, paa likaanguka, sasa nikakimbilia kwa majirani. Walinipatia sehemu ya kuishi na watoto wangu kwanza.”
Huduma hii ya umeme imebisha hodi hata hapa kwa Bi. Cenga, na imekuwa neema kubwa kama ilivyo jina lake ya kwamba, “mimi nitaachaje kufurahi? Kwa sababu ile ya kununuanunua mafuta ya taa imeisha. Inanisaidia sana. NAfurahi kwa sababu wale wadogo ikifika usiku wakati wa kulala walikuwa wanaogopa kuingia ndani kwa sababu kuna giza.”
Jimbo la Nampula limeweka msimamo wake
Hivi sasa serikali ya Msumbiji inahaha kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma kwenye huduma hii ya umeme.
Alberto Amando ni afisa kutoka taasisi ya udhibiti wa majanga nchini Msumbiji na “jimbo la Nampula liko hatarini zaidi kukumbwa na hali mbayá za hewa kwa kuwa lina ukanda mrefu wa pwani. UNHCR inajitahidi kusaidia wanufaika, hasa ujumuishaji wa wakimbizi wa ndani. Jimbo la Nampula limeweka wazi, unaposaidia wakimbizi wa ndani, basi na wenyeji wanaowapatia uhisani, nao wasisahaulike. HAtua hii inaleta matokeo.”
Na kwa Neema umeme sasa si manufaa kwa duka tu bali hata kwa elimu ya mtoto wake akisema, “mtoto wangu mdogo anapotaka kufanya kazi zake za shuleni nyumbani, umeme uko, hakuna shida!”