Ingawa hakuna kisa chochote cha kipindupindu mwaka huu Haiti vita haijaisha:UNICEF

14 Februari 2020

Mwaka 2020 umeanza vyema kisiwani Haiti kwa kutokuwa na kisa chochote kipya cha kipindupindu baada ya maelfu ya watu kupoteza maisha kwa miaka 9 iliyopita na ugonjwa huo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika moja ya vituo vya matibabu ya kipindupindu na kuhara mjini Port au Prince nchini Haiti vitanda vimesalia vitupu kwa sababu hakuna wagonjwa.

ikiwa ni dalili njema ya vita dhidi ya kipindupindu ugonjwa ambao UNICEF inasema kwa miaka 9 mfululizo umekatili maisha ya maelfu ya watu.

Na leo ni takribani mwaka mmoja hakujakuwa na kisa chochote kipya cha kipindupindu kilichoripotiwa na kuthibitishwa Haiti kama anavyofafanua mkurugenzi wa UNICEF wa operesheni za dharura Manuel Fontain

(SAUTI YA MANUEL FONTAIN)

“Tunaadhimisha mwaka wa kwanza wa kutokuwa na kisa chochote cha kipindupindu kilichothibitishwa hapa Haiti. Tumekuwa na kipindupindu kwa miaka 10, tumekuwa na karibu visa 800 vilivyoripotiwa  na vifo takribani 10,000 na huenda vingi zaidi. Na sasa hatuasikia kisa kilichothibitishwa kwa mwaka mzima hii ni muhimu sana”

UNICEFna washirika wamepeleka tiumu katika maeneo yote yaliyoathirika  na jumla ya watu 660,00 walielimishwa kuhusu hulka ya kulinda afya zao na usafi ili kuzuia ugonjwa huo mwaka 2019. Hata hivyo UNICEF inasisitiza kwamba vita havijaisha

(SAUTI YA MANUEL FONTAIN )

“Sio wakati wa kubweteka bado tuna kazi kubvwa kuhusu masuala ya maji, bado tuna kibarua kuhusu masuala ya usafi. Tunahitaji kuhakikisha tunaendelea kufanya kazi hii katika jamii ambazo zimehamasishwa na kujifunza jinsi ya kusafisha maji, kunawa mikono, kuweka mazingira yao safi na tunahitaji kufanya hivyo."

Amesisitiza kuwa sasa ni wakati wa kuongeza juhudi kudumisha mafanikio yaliyopatikana baada ya miaka 10 ya mahangaiko.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud