Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu tishio la kuwa ‘tiketi ya kifo’ kwa watoto wenye utapiamlo na wadumavu Haiti

Mtoto akipimwa utapiamlo huko  Cité Soleil nchini Haiti.
UNICEF
Mtoto akipimwa utapiamlo huko Cité Soleil nchini Haiti.

Kipindupindu tishio la kuwa ‘tiketi ya kifo’ kwa watoto wenye utapiamlo na wadumavu Haiti

Afya

Nchini Haiti, serikali kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na wadau wamezindua mfumo wa kuchunguza watoto 40,000 wenye umri wa chini ya  miaka mitano ili kubaini iwapo wanakabiliwa na udumavu ili waweze kupatiwa huduma haraka iwezekavyo wakati huu ambapo mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini humo uko hatarini zaidi kusababisha vifo kwa watoto wenye utapiamlo uliokithiri na wadumavu.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo katika miji ya Port-au-Prince, Haiti na New York, Marekani inasema watoto watakaobainika watafikishwa katika vituo vinavyopata usaidizi wa UNICEF au vituo vya karibu vya afya ambako tayari huduma bora inapatiwa watoto 8,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambayo wamebainika kuwa wadumavu.

Udumavu ni pale mtoto anapokuwa umri wake hauendani na urefu na uzito.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti Bruno Maes amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema, hii leo tunapambana vita vikali dhidi ya utapiamlo na kipindupindu, vitisho viwili vinavyoweka maisha ya watoto hatarini. Wakati unakwenda kasi, kipindupindu kinasambaa kwa kasi na kuna uwezekano mlipuko wa kipindupindu ukashindwa kudhibitiwa.

Amesema janga nchini Haiti kwa kiasi kikubwa ni janga kwa watoto kwa kuwa mgonjwa mmoja wa kipindupindu kati ya watatu ni mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano. Kwa watoto ambao tayari ni dhaifu kutokana na ukosefu wa lishe bora, kuugua kipindupindu au athari zake ikiwemo kuhara na kutapika, ni karibu na hukumu ya kifo.

Ni kwa mantiki hiyo amesema watoto hao walio dhaifu kutokana na lihe duni lazima watambuliwe na wapatiwe matibabu haraka na hatua sahihi na za kina zichukuliwe ili kuzuia wagonjwa wapya wa kipindupindu miongoni mwa jamii.

Zaidi ya watoto milioni nusu kusini magharibi mwa Haiti wasio na makazi, maji ya kunywa na vifaa vya usafi wanazidi kuwa hatarini kupata magonjwa ya kupumua,  kuhara, kipindupindu na malaria.
MINUSTAH/Logan Abassi
Zaidi ya watoto milioni nusu kusini magharibi mwa Haiti wasio na makazi, maji ya kunywa na vifaa vya usafi wanazidi kuwa hatarini kupata magonjwa ya kupumua, kuhara, kipindupindu na malaria.

Hali halisi  ya Kipindupindu

Kipindupindu kiliripotiwa Haiti tarehe 2 mwezi huu wa Oktoba mwaka 2022 na tangu wakati hu kuna wagonjwa shukiwa 357 ambapo zaidi ya nusu ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 14. Watoto wenye umri kati ya mwaka mmoja hadi minne wako hatarini zaidi.

Katika mji wa Cité Soleil watoto 8,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wako hatarini kutokana na mchanganyiko wa udumavu na kipindupindu.

Msaada unaotolewa na UNICEF

UNICEF imepatia wadau vyakula ambavyo ni tayari kutumika, maziwa na vifaa vingine vya matibabu ya udumavu na vile vya kuwezesha mamlaka kutoa huduma za afya.

Shirika hilo pia linashirikiana na wahudumu wa afya wa jamii ili kuhamasisha utoaji wa lishe bora kwa watoto wachanga sambamba na kuelimisha jamii jinsi ya kuzuia kuenea kwa kipindupindu.

UNICEF ilishatangaza ombi la awali la dola milioni 22 ili kukabiliana na kipindupindu Haiti lakini hadi sasa mwitikio ni kidogo.