Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UN lapitisha azimio kusaidia Pakistani; Guterres asema janga leo Pakistani kesho kwa mwingine.

Maji ya mafuriko kwenye wilaya ya Umerkot jimboni Sindh nchini Pakistani
© UNICEF/Asad Zaidi
Maji ya mafuriko kwenye wilaya ya Umerkot jimboni Sindh nchini Pakistani

Baraza Kuu la UN lapitisha azimio kusaidia Pakistani; Guterres asema janga leo Pakistani kesho kwa mwingine.

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuonesha mshikamano na kufanikisha usaidizi kwa serikali na watu wa Pakistani ikiwemo misaada ya kibinadamu, ukarabati na ujenzi mpya sambamba na kuepusha majanga zaidi iwapo taifa hilo litakumbwa na janga kama la sasa.

Azimio hilo limepitishwa wakati wa mkutano ulioitishwa kuzingatia hali ya mafuriko katika taifa hilo la bara la Asia ambalo wakati huu theluthi moja ya taifa hilo imetwama kwenye maji kutokana na mafuriko makubwa yaliyokumba taifa hilo mwezi Juni mwaka huu.

Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hii leo in Pakistani na kesho inaweza kuwa nchi zetu na jamii zetu. Zahma ya tabianchi inabisha hodi kwenye mlango wa kila mtu hivi sasa.

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema ni wakati wa kuitikia wito wa wananchi wa Pakistani kwa kuwa “janga la kidunia lahitaji mshikamano na hatua za kidunia.”

Pakistani inalipa gharama ya janga isilosababisha

Bwana Guterres amesema Pakistani inapaswa kupatiwa usaidizi kukabiliana na madhara ya mafuriko hayo kwa sababu Pakistani inachangia asilimia 1 tu ya hewa chafuzi duniani, lakini inalipa gharama kubwa kutokana na mabadiliko  ya tabianchi yaliyosababishwa na binadamu.

Amerejelea ziara yake mwezi mmoja uliopita  nchini Pakistani ambako alishuhudia kwa macho yake machungu wanayopitia wananchi. Wengi wamepoteza kila kitu; nyumba zao, mifugo yao, mazao yao na mustakabali wao.

“Na bado majira ya baridi Kali yanakaribia Pakistan na kiza kinene zaidi kinanyemelea. Hali itakuwa mbayá zaidi,” amesema Katibu Mkuu.

Mtoto mwenye umri wa miaka 9 akiwa ametoka kuteka maji kutoka kisima cha kusukuma maji kwa mkono kilichofurika maji jimboni Sindh nchini Pakistani
© UNICEF/Asad Zaidi
Mtoto mwenye umri wa miaka 9 akiwa ametoka kuteka maji kutoka kisima cha kusukuma maji kwa mkono kilichofurika maji jimboni Sindh nchini Pakistani

Nini kifanyike sasa?

Katibu Mkuu amesema ingawa tayari Umoja wa Mataifa na wadau wameanza kupeleka usaidizi, fedha zaidi zinahitajika hivyo amesema, “tunashirikiana na serikali ya Pakistani kuitisha Mkutano wa Kimataifa wa kuchangisha fedha ili kuleta pamoja wadau katika ngazi ya juu zaidi kutoa msaada wa kina wa kusaidia juhudi za ujenzi na ukarabati.”

Guterres amesihi wahisani kuchangia akiongeza kuwa ombi lililorekebishwa la kusaidia Pakistani sasa ni dola milioni 816, ikiwa ni ongezeko la dola milioni 656 kutoka ombi la awali na kwamba zitahitajika kusaidia hadi mwezi Mei mwakani.

Janga la Pakistani ni jaribio kwa Baraza Kuu la UN

Kwa upande wake Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN, Csaba Kőrösi amesema mkutano wa leo ni jaribio la maudhui ya #UNGA77 ambayo ni Majawabu kupitia mshikamano, uendelevu na sayansi.”

Pakistani iko katikati ya janga la tabianchi, haya ni mafuriko mabaya zaidi kuwahi kukumba taifa hili katika historia yake ya karibuni.

Kisha akahoji, “Je tunaweza kukutana kwa mshikamano na wananchi wa Pakistani wakati huu wanapotuhitaji?”

Bwana Kőrösi amesema Pakistani imefika Baraza Kuu ikiwa na imani ya chombo hicho na napongeza uongozi wa nchi hiyo kwa kuwasilisha pendekezo ambalo linasaka majawabu kupitia mshikamano.

Hivyo Rais huyo wa Baraza Kuu akatamatisha akisema “hebu na tutumia sayansi na mshikamano ili tuweze kuimarisha uwezo wetu wa kushughulikia majanga. Nyakati ni ngumu, lakini nina imani tunaweza kujenga pamoja kwa ubora zaidi.”