Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko ya Pakistani yanapima uwezo wetu wa hatua kwa tabianchi - Guterres

Malaria na magonjwa mengine yanaongezeka baada ya mafuriko katika jimbo la Sindh, Pakistan.
© UNICEF/Saiyna Bashir
Malaria na magonjwa mengine yanaongezeka baada ya mafuriko katika jimbo la Sindh, Pakistan.

Mafuriko ya Pakistani yanapima uwezo wetu wa hatua kwa tabianchi - Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Mwaka mmoja tangu mafuriko makubwa yakumbe Pakistan, bado usaidizi unasuasua na hii leo viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa wamekutana kwenye kikao maalum na kutoa ahadi za usaidizi zaidi wakati taifa hilo la Asia likiendelea na mchakato mgumu wa kujijenga upya.

Viongozi hao wamesisitiza pia umuhimu kwa kupunguza utoaji wa hewa chafuzi na kuimarisha kule iliko na kuanzisha kule ambako haiku, mifumo ya kutoa mapema tahadhari ya majanga ili kulinda mataifa yote duniani kwani kila uchao nchi zinakuwa hatarini kukumbwa na hali za hewa za kupindukia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye mkutano huo jijini New York, Marekani amesema vile ambavyo jamii ya kimataifa inachukua hatua kwa harakati za Pakistani kujikwamua ni jaribio la jinsi ya kupata haki kwa tabianchi.

Muathirika pacha

“Pakistani inahitaji na ina haki ya kupata msaada mkubwa kutoka kwa jamii ya kimataifa,” amesema Guterres.

Hii ni kwa kuzingatia kuwa licha ya kuchangia chini ya asilimia moja kwenye hewa chafuzi duniani, wananchi wa Pakistani wanakabiliwa na hatari mara 15 zaidi ya kufariki dunia kutokana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

“Pakistani ni muathirika pacha, wa madhara ya tabianchi na kupitwa kwa wakati kwa mfumo wa kimataifa wa fedha duniani ambao unazuia nchi za kipato cha kati kushindwa kupata rasilimali zinazohitajika sana kuwekeza katika miradi ya kuhimili na kujijengea mnepo,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Janga halikuwa la kawaida

Mafuriko hayo yaliyochochewa na mvua za monsuni yalitwamisha theluthi moja ya ardhi ya Pakistani, yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,7000, zaidi ya nyumba milioni mbili zilibomoka, halikdhalika miundombinu muhimu iliharibiwa. Watu milioni 33 waliathiriwa na mafuriko hayo, na nusu yao ni watoto.

Punde tu baada ya janga hilo, serikali ya Pakistani, ikiungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilizindua mpango wa kuchukua hatua na usaidizi, ikiomba dola milioni 816 kusaidia watu milioni 9.5 walioathiriwa zaidi. Ombi hilo hdi sasa limefadhiliwa kwa asilimia 69 pekee.

Hata leo hii,, hatua za usaidizi zinaendelea ambapo Umoja wa Mataifa na wadau wanasaidia maeneo yaliyokumbwa na mafuriko. Mashirika kama vile lile la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP linasaidia pia jamii kujijenga upya kiuchumi.

Kauli ya Rais wa UNGA78

Dennis Francis, Rais wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alisihi nchi wanachama na mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa kuendeleza kasi yao ya kusaidia juhudi za Pakistani za kujikwamua ya kujijenga upya.

Kwa mujibu wa shirika la  Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, takribani watu milioni nane, nusu yao wakiwa ni watoto, bado wanaishi kwenye maeneo yenye mafuriko bila huduma ya maji safi na salama, watoto milioni 3.5 hawako shuleni, na takribani watoto milioni 1.5 wanahitaji misaada ya huduma za lishe.

“Hali inayokumba watu wengi kwenye maeneo yaliyokabiliwa na mafuriko ni mbaya, na inatokea wakati tayari kuna matatizo mengine,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell akihutubia mkutano huo.

“Lakini changamoto hizi si kwamba haziwezi kukabiliwa, tuna fursa ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya kwa watoto wa Pakistani.”

Kauli ya OCHA

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, Joyce Msuya amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa kilichotokea Pakistani ni kiashiria kuwa hatua hazipaswi kuchelewa kuchukuliwa.

Amekumbusha kuwa kiwango cha athari kutokana na mafuriko hayo ni dhahiri kuwa msaada zaidi unahitajika kuwezesha jamii kujikwamua na kujijengea mnepo.

"Kwa msaada wa taasisi za kitaifa yakiwemo mashirika yanayoongozwa na wanawake, bila kusahau jamii ya kimataifa, zaidi ya watu milioni 6 wameshapokea aina ya msaada wa kibinadamu," amesema Bi. Msuya.

Hodi mlangoni haiitikiwi

Bwana Guterres amesisitiza kuwa onyo la janga la tabianchi linabisha hodi katika mlango wa kila mtu, na kuongeza kuwa “hodi inapigwa kuanzia Pembe ya Afrika hadi Canada. Uchafuzi utokanao na hewa ya ukaa unaongeza joto kwenye sayari, unaua watu na kuharibu jamii na uchumi.”