Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanaojiua Afrika ni kubwa zaidi duniani; WHO yazindua kampeni kuzuia tatizo hilo

Wasafiri kwenye basi la mwendo kasi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.
UN-Habitat/Julius Mwelu
Wasafiri kwenye basi la mwendo kasi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Idadi ya wanaojiua Afrika ni kubwa zaidi duniani; WHO yazindua kampeni kuzuia tatizo hilo

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa ulimwenguni WHO leo limezindua kampeni mpya ili kuchagiza uelewa na kuchukua hatua kwa ajili ya kuzuia kujiua barani Afrika ambako kuna kviwango vikubwa vya vifo vitokanavyo na kujiua.

Kwa mujibu wa takiwimu za shirika hilo zilizotolewa mjini Brazaville, nchini Congo,  karibu watu 11 katika kila watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa kujiua Afrika kikiwa ni kiwango kikubwa zaidi ya kiwango cha wastani cha kimataifa ambacho ni watu 9 kwa kila watu 100,000.

WHO inasema “Hali hii inatokana kwa kiasi kikubwa kwa kutochukuliwa hatua za kushughulikia na kuzuia sababu za hatari ikiwemo hali ya matatizo ya afya ya akili ambayo kwa sasa inaathiri watu milioni 116 likiwa ni ongezeko kubwa kutoka watu milioni 53 mwaka 1990.”

Kuhusu kampeni hiyo

Kampeni hiyo kupitia mitandao ya kijamii, iliyozinduliwa kabla ya siku ya afya ya akili duniani, inalenga kufikia watu milioni 10 kote kanda ya Afrika ili kuhamasisha umma na kuhamasisha uungwaji mkono wa serikali na watunga sera kwa ajili ya kuongeza umakini na ufadhili wa programu za afya ya akili, pamoja na juhudi za kuzuia watu kujiua.

Juhudi hizo ni pamoja na kuwawezesha wahudumu wa afya kusaidia zaidi wale wanaokabiliana na fikra za kujiua, kuwaelimisha watu ambao wanaweza kupata fikra hizo juu ya wapi pa kupata usaidizi pamoja na kuhamasisha umma jinsi ya kutambua na kusaidia wale wanaohitaji msaada na kusaidia kukabiliana na unyanyapaa unaohusishwa na afya ya akili na kujiua, kifafa, matatizo ya afya ya akili na matumizi mabaya ya pombe na madawa ya kulevya.

Hali halisi ya kujiua barani Afrika

Taarifa hiyo ya WHO imesema “Kanda ya Afrika ni maskani ya nchi 6 kati ya 10 zilizo na viwango vya juu vya watu kujiua ulimwenguni. “ Na njia zinatotumika zaidi kujiua katika kanda hiyo ni kujinyonga, kunywa sumu na kwa kiasi kidogo kujitosa majini na kuzama, kutumia bunduki, kujirusha kutoka ghiorofani au kumeza madawa kuzidi kiwango. Uchunguzi unaonesha kuwa barani Afrika kwa kila mtu anayefanikiwa kujiua, kuna takriban watu wengine 20 waliojaribu kujiua."

Dkt. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema "Kujiua ni tatizo kubwa la afya ya umma na kila kifo cha kujiua ni janga. Kwa bahati mbaya, hatua za kuzuia kujiua ni mara chache sana kuwa kipaumbele katika programu za afya za kitaifa. Uwekezaji mkubwa lazima ufanywe ili kukabiliana na mzigo unaoongezeka kwa Afrika wa magonjwa sugu na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile matatizo ya akili ambayo yanaweza kuchangia kujiua."

Kwa mujibu wa WHO matatizo ya afya ya akili huchangia hadi asilimia 11% ya sababu za hatari zinazohusiana na kujiua. Siku ya afya ya akili duniani mwaka huu inaadhimishwa chini ya kaulimbiu "Fanya afya ya akili na ustawi kwa wote kuwa kipaumbele cha Kimataifa" ili kuvutia umuhimu wa huduma za afya ya akili na haja ya upatikanaji bora wa huduma za afya. Barani Afrika, uwekezaji duni unaofanywa na serikali ndio changamoto kuu ya utoaji wa huduma za afya ya akili. Kwa wastani serikali hutenga chini ya senti 50 za Marekani kwa kila mtu kwa ajili ya afya ya akili.

“Ingawa ni uboreshaji kutoka senti 10 za Marekani mwaka 2017, bado iko chini ya dola 2 zilizopendekezwa kwa kila mtu kwa nchi zenye kipato cha chini. Zaidi ya hayo, huduma ya afya ya akili kwa ujumla hazijajumuishwa katika mipango ya kitaifa ya bima ya afya.” 

Uwekezaji duni

Kutokana na uwekezaji mdogo katika huduma za afya ya akili, kanda ya Afrika ina daktari mmoja wa magonjwa wa akili kwa kila wakazi 500,000, ambayo ni mara 100 chini ya mapendekezo ya WHO.

Zaidi ya hayo, wahudumu wa afya ya akili wako wengi katika maeneo ya mijini, huku vituo vya afya vya msingi na vya jamii vikiwa na vichache sana kama vipo.

WHO inaunga mkono nchi kuongeza huduma za afya ya akili katika eneo hilo.

Wahudumu wa afya ya msingi nchini Zimbabwe wanapewa mafunzo chini ya mpango wa WHO ili kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za afya ya akili.

Nchini Kenya, Uganda na Zimbabwe mpango wa kuendeleza kesi za uwekezaji nchini kwa ajili ya huduma za afya ya akili umehitimishwa na mchakato unaendelea ili kukusanya rasilimali.

Shirika la WHO pia linaunga mkono Cabo Verde na Cote d'Ivoire kufanya uchanganuzi wa hali ya kitaifa ya kujiua kama hatua ya kwanza ya kubuni hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hilo.

Mwezi Agosti 2022, mawaziri wa afya wa Afrika waliokusanyika kwa kikao cha 72 cha Kamati ya kanda ya WHO ya Afrika ambao ni mkutano mkuu wa afya wa kanda waliidhinisha mkakati mpya wa kuimarisha huduma ya afya ya akili na kuweka malengo ya 2030 yakitaka nchi zote kuwa na sera au sheria kuhusu afya ya akili, asilimia 60 ya nchi zinazotekeleza sera hiyo, asilimia 95 ya nchi zinazofuatilia na kutoa taarifa kuhusu viashirio muhimu vya afya ya akili na asilimia 80 ya nchi zina bajeti ya huduma za afya ya akili.