Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 24 wanaishi na kisukari Afrika na idadi kufikia milioni 55 mwaka 2045:WHO

Afisa wa afya akifanya uchunguzi wa kisukari kwa mgonjwa barani Afrika.
WHO Africa
Afisa wa afya akifanya uchunguzi wa kisukari kwa mgonjwa barani Afrika.

Watu milioni 24 wanaishi na kisukari Afrika na idadi kufikia milioni 55 mwaka 2045:WHO

Afya

Wakati dunia ikiadhimisha hii leo siku ya kisukari duniani kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu ongezeko la mzigo wa ugonjwa huo na mikakati ya kuzuia na kudhibiti tishio lake, bara la Afrika linaonekana kuwa na changamoto kubwa ya ugonjwa huo kwa mujibu wa takwimu mpya za shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO.

Takwimu zilizotolewa leo na WHO kanda ya Afrika zinaonyesha kiwango cha changamoto ya ugonjwa wa kisukari Afrika ni kikubwa ambapo watu wazima milioni 24 hivi sasa wanaishi na ugonjwa wa kisukari na idadi inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 129% hadi kufikia watu million 55 ifikapo mwaka 2045.

Kupitia ujumbe ake wa siku hii Dkt. Matshidiso Moeti mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema “Mwaka jana ugonjwa wa kisukari ulikatili maisha ya watu 416,000 barani Afrika na ugonjwa huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo Afrika ifikapo mwaka 2030. La msingi zaidi ni kwamba kisukari ndio ugonjwaa pekee usio wa kuambukiza ambao hatari yake ya vifo vya mapema inaongezeka badala ya kupungua.”

Mkuu huyo wa WHO Afrika ameendelea kusema kwamba “Sababu kuu hatari zinazochangia ongezeko la ugonjwa huo Afrika ni pamoja na  historia ya familia, ongezeko la umri wa kuishi na sababu zingine zilizozoeleka kama uzito wa kupindukia na utipwatipwa, maisha ya kukaa bila mazoezi, lishe isiyofaa, uvutaji wa sigara na unywaji pombe kupita kiasi. Kwa bahati mbaya, sababu hizi za hatari zinazoweza kubadilishwa zinaongezeka katika nchi zote katika Kanda ya Afrika ya WHO.”

Dkt. Moeti amesema “Na changamoto kubwa katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ni ukweli kwamba zaidi ya mtu 1 kati ya kila watu 2 barani Afrika anayeishi na kisukari hajawahi kupimwa, hivyo kuongeza fursa za nyenzo za upimaji na dawa kama insulin, ni moja ya maeneo yanayopaswa kufanyiwa kazi haraka.”

kula vyakula vya afya kunapunguza kupata kwa aina ya 2 ya kisukari.
Photo: PAHO/WHO
kula vyakula vya afya kunapunguza kupata kwa aina ya 2 ya kisukari.

Bila hatua athari ni mbaya zaidi

WHO imeonya kwamba ukiachwa bila kudhibitiwa, na bila usimamizi na mabadiliko ya mwenendo wa maisha, ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha matatizo mengine mengi. 

Matatizo hayo ni pamoja na magonjwa ya mshtuko wa moyo, kiharusi, figo kushindwa kufanyakazi, kukatwa kwa viongo vya mwili kama miguu,  ulemavu wa kutoona, upofu, na uharibifu wa mishipa. 

Limeendelea kusema shirika hilo kuwa watu walio na ugonjwa wa kisukari pia wako katika hatari kubwa ya kupata dalili kali za COVID-19.

Ili kuharakisha hatua dhidi ya ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza, WHO iliandaa mkataba wa kisukari duniani ambao lengo lake ni “kupunguza athari mbaya za ugonjwa huo, na kuhakikisha kwamba kila mtu anayeishi na ugonjwa wa kisukari anapata matibabu na matunzo yaliyo sawa, ya kina, ya bei nafuu na yenye ubora.”

Afrika yahitaji mikakati ya kuudhibiti

Eric Omondi, muuguzi wa Kituo cha Usimamizi na Taarifa za Kisukari anakagua eneo lenye uvimbe kwenye mkono wa Maingi.
Eric Omondi, muuguzi wa Kituo cha Usimamizi na Taarifa za Kisukari anakagua eneo lenye uvimbe kwenye mkono wa Maingi.
Eric Omondi, muuguzi wa Kituo cha Usimamizi na Taarifa za Kisukari anakagua eneo lenye uvimbe kwenye mkono wa Maingi.

Dkt. Moeti amesisitiza kuwa “Leo, tunapoadhimisha siku ya kisukari duniani, ninataka kuchukua fursa hii kutoa wito kwa serikali za nchi wanachama kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa bidhaa muhimu, kama vile dawa za insulini, macshine za kuangalia kiwango cha sukaru glucometer na sindano zinazotumika kupimia au strips. Hii ni muhimu ili kuhakikisha fursa sawa kwa kila mtu anayeishi na ugonjwa wa kisukari, bila kujali ni wapi aliko katika bara hili.”

Pia amezihimiza serikali za Afrika kupitisha na kubinafsisha malengo ya kimataifa ya ugonjwa wa kisukari, kama sehemu ya mapendekezo ya kuimarisha na kufuatilia hatua za ugonjwa wa kisukari ndani ya programu zao za kitaifa za magonjwa yasiyo ya kuambukiza NCD.

Na kwa watu wote barani Afrika ujumbe wa Dkt. Moeti ni kwamba ni muhimu kula mlo unaofaa na kufanya mazoezi mara kwa mara, kuacha uvutaji sigara, kutokuwa na uzito wa kupindukia  na kudhibiti kiwango cha unywaji pombe kwani hatua hizo zitawalinda na kisukari aina ya 2 na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza NCD’s.

Nyiha anachunguza chupa ya insulini ambayo Maingi amekuwa akitumia, kuangalia kama kuna dalili za kuambukizwa. Baada ya kubaini tatizo la uhifadhi wa insulini, Nyiha anaeleza jinsi gani-hata bila friji-insulini inaweza kuwekwa katika hali ya ubaridi na s…
WHO
Nyiha anachunguza chupa ya insulini ambayo Maingi amekuwa akitumia, kuangalia kama kuna dalili za kuambukizwa. Baada ya kubaini tatizo la uhifadhi wa insulini, Nyiha anaeleza jinsi gani-hata bila friji-insulini inaweza kuwekwa katika hali ya ubaridi na safi.

Wito kwa wadau

Mwisho kabisa Dkt. Moeti amewataka wadau kushirikiana na serikali za Afrika kusongesha utekelezaji wa ajenda yaw Ho ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza PEN na PEN-Plus ili kuboresha fursa za matibabu na huduma kwa wagonjwa wa kisukari barani humo.

“Hebu sote tuungane na kutimiza sehemu ya wajibu wetu kuzuia madhila yasiyo ya lazima na kuokoa maisha ya watu.”

Siku ya kisukari duniani huadhimishwa kila mwaka Novemba 14 na maudhui yam waka huu kama yalivyokuwa yam waka jana na yatakavyokuwa mwakani ni “Fursa ya huduma za kisukari” yakisisitiza umuhimu wa kuzuia na juhudi za hatua dhidi ya kisukari.