Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakikisheni afya ya akili kwa watu wote si ndoto:Guterres

Kazakhstan ametajwa kushika nafasi ya tatu miongoni mwa nchi za Asia ya Kati zenye viwango vikubwa vya vijana kujiua
© UNICEF/Anush Babajanyan/VII Photo
Kazakhstan ametajwa kushika nafasi ya tatu miongoni mwa nchi za Asia ya Kati zenye viwango vikubwa vya vijana kujiua

Hakikisheni afya ya akili kwa watu wote si ndoto:Guterres

Afya

Janga la COVID-19 limekuwa na athari kubwa kwa afya ya akili ulimwenguni kote, na lazima hatua zichukuliwe ili "kukomesha ukosefu wa usawa uliofichuliwa na janga hilo", pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya akili, inayoadhimishwa leo Jumapili Oktoba 10.

Katika ujumbe huo amekumbusha kwamba mamilioni ya watu wanakabiliwa na simanzi kwa sababu ya wanafamilia na marafiki waliopotea na janga la COVID-19 pia wengi wana wasiwasi juu ya usalama wa kazi, na wazee wakihofia kuweza kutengwa na upweke,  na hivyo amesisitiza kwamba "bila hatua za dhati, athari ya afya ya akili inaweza kudumu kwa muda mrefu kuliko janga lenyewe ”.

Watoto wametengwa na kufadhaika

Katika ujumbe wake kwa Siku hiyo, mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameangazia kwamba watoto na vijana "wanaweza kuhisi kutengwa na kufadhaika" na ametaka hatua zichukuliwe kushughulikia ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa huduma za afya ya akili.

Kulingana na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, karibu asilimia 20 ya watoto na vijana duniani wanasumbuliwa na afya ya akili, na kujiua ndio sababu ya pili ya vifo kati ya watoto wa miaka 15-29.

Wataalamu wa kisaikolojia wanawasadia mabinti wali katika mazingira hatarishi kaskazini mwa Ukraine wakati huu ambapo kuna vuzizi kutokana na janga la COVID-19 ambavyo vinawaathiri afya ya akili.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Wataalamu wa kisaikolojia wanawasadia mabinti wali katika mazingira hatarishi kaskazini mwa Ukraine wakati huu ambapo kuna vuzizi kutokana na janga la COVID-19 ambavyo vinawaathiri afya ya akili.

Mapema wiki, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, lilihimiza uwekezaji zaidi kwenye afya ya akili ya watoto.

Toleo la hivi karibuni la ripoti ya shirika hilo, ”Hali ya watoto duniani” limesema kuwa hata kabla ya mgogoro huo wa COVID-19, watoto na vijana tayari walikuwa wamebeba mzigo mkubwa wa tatizo la afya ya akili, na bila uwekezaji mkubwa katika kuwashughulikia hali itakuwa mbaya zaidi.

Miezi 18 iliyopita imekuwa migumu kwa watoto, amesema Henrietta Fore, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF.

Pengo la usawa katika upatikanaji wa matibabu

"Katika nchi zenye kipato cha juu, zaidi ya asilimia 75 ya watu walio na msongo wa mawazo wanaripoti kwamba hawapati huduma za kutosha, na katika nchi za kipato cha chini na cha kati, zaidi ya asilimia 75 ya watu walio na matatizo ya afya ya akili hawapati matibabu kabisa", aliendelea kusema Bwana. Guterres.

Akizungumzia uwekezaji mdogo kwa muda mrefu kama sababu kuu, na serikali kutumia wastani wa asilimia 2 tu ya bajeti zao za afya kwa afya ya akili, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema hii haikubaliki.

Hatua nzuri

Akisisitiza kwamba hatimaye kuna utambuzi kwamba "hakuwezi kuwa na afya bila afya ya akili", Guterres amesema nchi wanachama zimeidhinisha mpango wa utekelezaji wa afya ya akili uliosidhinishwa na WHO.

Mwaka 2019, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO lilizindua mpango maalum wa afya ya akili (2019-2023): Chanjo ya Afya ya akili kwa afya ya akili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na nafuu ya afya ya akili katika nchi 12 za kipaumbele, ikihudumia watu zaidi ya milioni 100.

Wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Afya duniani Mei 2021, serikali kutoka kote ulimwenguni zilitambua hitaji la kuongeza huduma bora za afya ya akili katika ngazi zote, na nchi zingine zimepata njia mpya za kutoa huduma ya afya ya akili kwa watu wao.

"Familia ya Umoja wa Mataifa, pamoja na washirika katika jamii ya kimataifa ya afya ya akili, wanaanzisha muongozo mpya na kutengeneza zana mpya za kuboresha afya ya akili", ameongeza Bwana Guterre.

Safari bado ndefu

Katibu Mkuu amehitimisha kuwa "hizi ni hatua nzuri, lakini tuna safari ndefu ya kwenda", akisistiza ahadi ya Umoja wa Mataifa kuwa ni muhimu "kufanya kazi kwa haraka na madhumuni ya kuhakikisha huduma bora za afya ya akili kwa watu wote, kila mahali"