Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita vya Ukraine: Mkuu wa UN awasili kwa mazungumzo Moscow kama mjumbe wa amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na wajumbe wake wakati wa mkutano na waziri wa mambo ya nje  Sergey Lavrov, Moscow, Urusi
UN Russia/Yuri Kochin
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na wajumbe wake wakati wa mkutano na waziri wa mambo ya nje Sergey Lavrov, Moscow, Urusi

Vita vya Ukraine: Mkuu wa UN awasili kwa mazungumzo Moscow kama mjumbe wa amani

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza haja ya "kuweka hai maadili ya ushirikiano wa kimataifa" huku vita vya Ukraine vikiendelea na athari zake kote duniani.

Akizungumza mjini Moscow leo Jumanne, ametoa mapendekezo ambayo yataweka mazingira ya kuruhusu raia kuondoka kwa usalama na utoaji wa misaada ya kibinadamu inayohitajika sana, katika miji ya Donbas na Mariupol.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amekuwa katika mji mkuu wa Urusi kwa mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Sergey Lavrov na pia atapokelewa na Rais Vladimir Putin.

Majadiliano bayana

Bwana. Guterres amewaambia waandishi wa habari kwamba “alikuwa na majadiliano ya wazi kabisa na bwana Lavrov na ni bayana kwamba kuna misimamo miwili tofauti kuhusu kile kinachotokea Ukraine."

Urusi imesema inaendesha "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine, wakati kwa Umoja wa Mataifa, uvamizi wa Februari 24 ni ukiukaji wa uadilifu wa haki ya ardhi ya nchi na unakwenda kinyume na mkataba wa Umoja wa Mataifa.

"Lakini ni imani yangu kubwa kwamba kadiri tutakavyomaliza vita hivi mapema, itakuwa bora kwa watu wa Ukraine, kwa watu wa shirikisho la Urusi, na wale walio mbali zaidi," amesema Guterres.

Akisisitiza jukumu lake kama "mjumbe wa amani", Katibu Mkuu amekariri kwamba Umoja wa Mataifa umetoa wito mara kwa mara wa kusitisha mapigano ili kuwalinda raia, pamoja na mazungumzo ya kisiasa kuelekea suluhu, ambayo hadi sasa hayajazaa matunda.

Akizungumzia vita vikali vinavyoendelea katika eneo la Donbas Mashariki mwa Ukraine, amesema kuwa raia wengi wanauawa, na mamia kwa maelfu wamenaswa katika mzozo huo, akiongeza kuwa ripoti za mara kwa mara za ukiukaji wa haki za binadamu, pamoja na uwezekano wa uhalifu wa kivita vitahitaji uchunguzi huru kwa ajili ya uwajibikaji unastahili

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa mkutano na waziri wa mambo ya nje Sergey Lavrov, Moscow, Urusi.
UN Russia/Yuri Kochin
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa mkutano na waziri wa mambo ya nje Sergey Lavrov, Moscow, Urusi.

Njia za kupitisha misaada ya kibinadamu

"Tunahitaji haraka njia za kupitisha misaada ya kibinadamu ambazo ni salama na zinazofaa na zinazoheshimiwa na wote ili kuwaondoa raia na kuweza kutoa msaada unaohitajika."

Katibu Mkuu amependekeza kuanzishwa kwa kikundi cha mawasiliano ya kibinadamu kinachojumuisha Urusi, Ukraine na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya "kutafuta fursa za kufunguliwa kwa upenyo salama, pamoja na usitishaji wa uhasama wa ndani, na kuhakikisha kuwa zinaufanisi. "

Akizungumzia mgogoro ndani ya mgogoro huko Mariupol, ambapo maelfu wanahitaji sana msaada wa kuokoa maisha, na kwa wengi, uokoaji, amesisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kuhamasisha kikamilifu rasilimali zake za kibinadamu na vifaa ili kusaidia kuokoa maisha.

Bwana Guterres amependekeza kuwa Umoja wa Mataifa, Kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu, na vikosi vya Ukraine na Urusi, kuratibu kazi ya kuwezesha uokoaji salama wa raia wanaotaka kuondoka Mariupol ikiwa ni Pamoja na ndani ya kiwanda cha chuma cha Azovstal na katika jiji lenyewe, na katika mwelekeo wowote wanaochagua na kufikisha misaada ya kibinadamu.

Mshtuko kwa ulimwengu

Akizungumzia athari kubwa za vita hivyo, Katibu Mkuu ameeleza baadhi ya mawimbi ya mshtuko wa vita hivyo yanayosikika kote ulimwenguni, kama vile kuongezeka kwa kasi kwa gharama za chakula na nishati, hali ambayo inaathiri mamilioni ya watu walio hatarini kote duniani.

"Hii inakuja wakati bado kuna mshtuko wa janga linaloendelea la COVID-19 na ufikiaji usio sawa wa rasilimali za kujikwamua, ambazo zinaadhibu nchi zinazoendelea kote ulimwenguni."

Kwa hivyo, amesema “kuanzishwa haraka kwa amani itakuwa bora zaidi kwa ajili ya Ukraine, Urusi, na kwa ulimwengu wote," amesema.

Ameongeza kuwa "Na ni muhimu sana, hata katika wakati huu wa ugumu, kuweka hai maadili ya umoja wa kimataifa.”

Katibu Mkuu amesisitiza haja ya kuwa na ulimwengu ambao ni wa mitazambo mbalimbali na unaotii mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, na ambao unatambua usawa kamili kati ya mataifa, kwa matumaini kwamba ubinadamu utaungana tena kushughulikia changamoto zinazofanana kama vile mabadiliko ya tabianchi na ambayo vita pekee tunayopaswa kuwa nayo itakuwa vita ya wale wanaoweka sayari hatarini.

Katibu Mkuu atakuwa Ukraine siku ya Alhamisi ambapo atakuwa na mkutano wa kikazi na waziri wa mambo ya nje Dmytro Kuleba, na atapokelewa na Rais Volodymyr Zelenskyy.