Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Sudan asema deni la nje linairudisha nyuma nchi yake kufikia maendeleo

Abdel-Fattah Al-Burhan Abdelrahman Al-Burhan, Rais wa Baraza Kuu la Mpito la Sudan, akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu.
UN Photo/Cia Pak
Abdel-Fattah Al-Burhan Abdelrahman Al-Burhan, Rais wa Baraza Kuu la Mpito la Sudan, akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu.

Rais wa Sudan asema deni la nje linairudisha nyuma nchi yake kufikia maendeleo

Masuala ya UM

Deni la nje ni kikwazo kikubwa kinachozuia ukuaji wa kiuchumi na kijamii nchini Sudan na pia linazuia kutimiza malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs amesema leo Rais wa serikali ya mpito wa Sudan Abdel-Fattah AlBurhan Abdelrahman Al-Burhan wakati akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu kikao cha 77 jijini New York Marekani.

“Naamini unafahamu kwamba Sudan inatakiwa kunufaika na msamaha wa madeni kwa nchi masikini duniani kama ilivyokubaliwa na wadau wetu wa kimataifa katika mkutano wa Paris mwaka 2020 na kisha mkutano wa Berlin mwaka 2021 lakini bado hatujaanza kunufaika japo Sudan imejiwekea sheria ya kulipa madeni yake ya nje.”

Pamoja na kukabiliwa na mzigo huo wa deni ameeleza Sudan inaendelea kutumia mbinu zote kuhakikisha wanatekeleza Malengo ya Maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs kwakuwa inaamini kwenye matokeo chanya wanayoletwa na utekelezaji wake ifikapo mwaa 2030.

“Serikali yetu imepitisha hati ya kupunguza umasikini kuanzia mwaka 2021-2023 na mwezi Julai mwaka jana 2021 Sudan iliwasilisha kwa hiyari ripoti yake kuhusiana na utelezaji watu wa SDG kwakuwa tunaamini katika mpango huu wa kupunguza umasikini.”

Amesema nchi yake pamoja na kuendelea na utekelezaji wa kupunguza umasikini bado wanahitaji msaada kutoka nchi wahisani na wadau mbalimbali.

Akizungumzia masuala ya uchumi amesema mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za chakula na nishati kutaweza kupatiwa suluhu iwapo kutakuwa na ushirikiano wa kimataifa na kusihi Umoja wa Mataifa na Mashirika yake kusaidia katika uanzishaji wa Taasisi ya utafiti ya kilimo nchini humo .

“Tunataka Sudan iweze kuwahakikishia chakula wananchi wake na kusaidia wananchi walio katika ukanda wetu ndio maana tunataka msaada ili kuweza kufanikisha. Msaada tunaotaka ni kubadilishana uzoefu na kujengewa uwezo katika taasisi yetu ya utafiti wa kilimo.”

 

Wakimbizi

Sudan ni moja ya nchi zilizohifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani kwa miaka mingi na wamekuwa wakishirikiana nao licha ya hali mbaya ya kiusalama na kiuchumi inayoikabili nchi hiyo na ndio maana ameomba usaidizi wa kimataifa katika kusaidia wakimbizi

“ Tumefungua milango yetu kwa miaka mingi kwa zaidi ya wakimbizi milioni nne lakini athari za Mabadiliko ya tabianchi zinazidi kuongezeka, ukame na mafuriko vinazidi kuongezeka huko msaada wa rasilimali ukizidi kupungua ndio maana tunaitisha usaidizi wa pamoja tushirikiane katika kutoa msaada kwa wakimbizi .”

Rais huyo pia amezungumzia ushiriki wao katika kusaka amani katika nchi jirani ya Sudan kusini, Somalia, DRC na inaendelea na kushirikiana na nchi nyingine zilizopo pembe ya Afrika na hata zile zilizopo Magharibi katika kusaidia wananchi kuweza kupata haki zao.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha silaha ndogo ndogo zinatokomezwa ili kuhakikisha amani katika ukanda huo na hi inatokana na kupambania rasilimali kama maji, malisho ya mifugo na madini na hii imesababisha silahi hizi kusambaa zaidi kwahiyo inahitajika udhibiti wa silaha hizo.

Mageuzi katika Baraza la Usalama

Rais AlBurhan amesema Sudan inaunga mkono msimamo wa Afrika kuhusu Mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi yake imeshiriki kikamilifu.

“Tumeshiriki katika mchakato usio rasmi wa mazungumzo kati ya serikali na serikali kuhusu mageuzi ya Baraza la usalama, Baraza la usalama lazima lifanyiwe mageuzi na hii lazima liwe mageuzi makubwa na lijumuishe marekebisho ya utendaji kazi wa Baraza hilo ili kushughulikia mazoea mabaya ya sasa.” Amesisitiza Rais huyo na kutolea mfano matumizi ya maneno ya upande mmoja kutumika na wenye kalamu kwa baadhi ya nchi bila kujumuisha pande zote zinazohusika kwenye suala husika.

Amehitimisha hotuba yake kwa kutoa shukran za dhati kwa wadau wote waliosimama na nchi yao wakati wakipia kipindi kigumu na kutoa wito kwa wadau wote na Umoja wa Mataifa kuendelea kuonesha ushirikiano zaidi kwa nchi yake  ya Sudan.