Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame umeniponza nusura niozwe kwa mzee: Carol

Watoto hawa wa shule katika shule ya msingi ya Naipa kaunti ya Turkana nchini Kenya. Wako hatarini kukumbwa na ndoa kwenye umri mdogo.
© UNICEF/UNI3Andrew Brown
Watoto hawa wa shule katika shule ya msingi ya Naipa kaunti ya Turkana nchini Kenya. Wako hatarini kukumbwa na ndoa kwenye umri mdogo.

Ukame umeniponza nusura niozwe kwa mzee: Carol

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema watoto wengi na hususan wa kike katika jamii zilizoathirika na ukame nchini Kenya ikiwemo Turkana wako katika hatari  hasa ya kuozwa mapema kwa sababu familia nyingi zinahaha kuweka mlo mezani na suluhu ya karibu wanayoiona ni kuoza binti zao mapema ili kujikimu. Sasa shirika hilo linashirikiana na mamlaka za huduma ya ulinzi kwa watoto katika maeneo yaliyoathirika ili kuwalinda dhidi ya ajira ndoa za utotoni. 

Carol , hilo si jina lake halisi ila amepewa sababu ya kulinda usalama wake, ana umri wa miaka 11 na anaishi katika Kaunti ya Turkana anasema mjomba wake aliamua kumuoza baada ya hali ya maisha kuzidi kuwa mbaya kutokana na ukame , kwani sasa hawana mbuzi tena, wala hawana chochote na matatizo yamekuwa mengi nyumbani. Lakini Caro mwenye ndoto za kusoma alikataa katakata akisema, “nilisema siwezi kukubali hata kama ni njaa basi wacha niake tu mi siwezi kukubali hicho kitu.”  

Hii ni changamoto inayozikabili familia nyingi hapa Turkana, kisa ni ukame wa muda mrefu uliowafanya kupoteza uwezo wa kujikimu kimaisha, mazao yamekauka, mifugo imekufa, fedha hakuna na msaada ni changamoto.

Kukosekana kwa fedha ya kulipia mtihani ndio kulimponza Carol na kisha, “Mama yangu niliporudishwa nyumbani kwenda kuleta hela ya kulipia mtihani alisema hana hela, hakunipa na hiyo likanifanya nikaacha shule. Na ndio ikafanya wanipe mzee anioe, mimi nikakataa nikasema huyo bwana siwezi kukubali.” 

Ameendelea kusema kuwa mwanaume huyo mzee alikuja kumchukua na pikipiki akaondoka naye na wakiwa njiani walisimama porini na mwanaume huyo akamnajisi. 

Mkurugenzi wa huduma ya ulinzi kwa watoto Turkana Julius Yator anasema “Kisa hicho kutoka Turkana South kiliripotiwa na jirani kwenye ofisi ya huduma kwa watoto ambayo ni ofisi yangu, na kuanzia hapo mchakato wa kukamata wahusika na kumuokoa mtoto ukaanza.” 

UNICEF inashirikiana na ofisi hiyo ili kuwalinda watoto walioathirika na ukame na walio hatarini kama Carol, na hadi sasa watoto 1,600 katika Kaunti hiyo wameshafikiwa na kuokolewa dhidi ya ajira na ndoa za utotoni. 

Mkuu wa UNICEF ofisi ya kanda ya Lodwar Laban Rotuno Kipsang anasema “kwa kawaida tunaporipoti kesi kama hizo binti huokolewa na anapewa malazi na ushauri nasaha. Ukanda wangu pia unafanya kazi kubwa ya kushirikisha jamii kupitia msaada wa UNICEF peke yetu na washirika wengine, na sasa hivi tuna kampeni inayosema baini na komesha , ili unapoona unazuia ni kama katika kesi hii mtu aliona na akaamua kuripoti na mtoto akaokolewa asiolewe.” 

Na Carol baada ya kuokolewa anasema anataka kurejea ndoto yake “Nataka kusaidiwa niendelee na shule.”