Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zetu za pamoja za kupambana na mabadiliko ya tabianchi lazima ziendelee - Uganda 

Jessica Alupo, Makamu wa Rais wa Uganda akiwa anahutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77
UN Photo/Loey Felipe
Jessica Alupo, Makamu wa Rais wa Uganda akiwa anahutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77

Juhudi zetu za pamoja za kupambana na mabadiliko ya tabianchi lazima ziendelee - Uganda 

Masuala ya UM

Mabadiliko ya tabia nchi bado ni moja ya changamoto kubwa ya wakati wetu, ndivyo Jessica Alupo, Makamu wa Rais wa Uganda akiwa anahutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 Alhamis jioni, jijini New York, Marekani, ndivyo alivyoanza kueleza kuhusu tatizo la mabadiliko ya tabianchi ambalo sasa ni tishio kwa ulimwengu kuliko wakati mwingine wowote.

Makama wa Rais huyo wa Uganda amesisitiza kwa kusema, “juhudi zetu za pamoja za kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni mchakato usioweza kutenduliwa ambao lazima uendelee. Hata hivyo, lazima tutambue kwamba licha ya kuchangia kiasi kidogo cha utoaji wa hewa chafuzi duniani, bara la Afrika kama vile maeneo mengi yanayoendelea duniani yanakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kiwango kisicho na uwiano.” 

Akitoa mfano kwa kutumia nchi yake, Uganda, “inaendelea kukumbwa na ukame wa muda mrefu, kuyeyuka kwa barafu kwenye mlima wake wa juu zaidi, Mlima Ruwenzori, mafuriko, mwelekeo wa mvua na maporomoko ya ardhi.” Amesema kiongozi huyo ambaye amemwakilisha Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni na akamnukuu akisema, “kama alivyosema Mheshimiwa Rais Museveni, tatizo la tabianchi pia ni matokeo ya kutowajibika na wakati mwingine vitendo vya uchoyo vya binadamu. Kadhalika, maendeleo duni yakiendelea, tusahau kuhifadhi mazingira.” 

Jessica Alupo akieleza namna ambavyo kuna ukosefu wa uwiano kati ya namna nchi zinavyochangia kwenye uchafuzi wa hali ya hewa na namna zinavyowajibika amesema, “inasikitisha na kinafiki kwamba baadhi ya maeneo na mataifa ambayo yalisimamia vibaya mazingira na kushiriki ipasavyo kwa ongezeko la joto duniani, yameanza kampeni kali ya kuzuia juhudi za nchi nyingine, kuendeleza kwa uwajibikaji na uendelevu sekta ya mafuta na gesi. Maoni yetu ni kwamba maendeleo yanapaswa kuwa rafiki kwa mazingira, shirikishi na kutoa manufaa kwa wote - yasimwache mtu nyuma.” 

Alshabaab na ADF 

Suala la ugaidi nalo lilikuwa sehemu ya hotuba ya Makamu wa Rais wa Uganda ambapo ameeleza kuwa Uganda itaendelea kuunga mkono na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kukabiliana na ugaidi duniani na kikanda. 

“Vikundi vya kigaidi kama vile Al-Shabaab na Allied Democratic Forces (ADF), vinaendelea kufanya vitendo vya kigaidi katika eneo letu. Kama jumuiya ya mataifa, ni lazima tuwe thabiti katika azimio letu la kuzuia na kupambana na ugaidi, katika aina na udhihirisho wake wote. Tunapaswa kutenda kwa uratibu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kukabiliana na tishio hili.” Amesema Jessica Alupo.  

Wakimbizi 

Kuhusu suala la wakimbizi, Uganda imeeleza kuwa imejitolea kushirikiana na nchi zinazozalisha wakimbizi, kanda na wadau wa kimataifa ili kushughulikia visababishi vya wakimbizi na kuiomba jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono, “juhudi zetu katika ukanda huu.” 

 Akionesha namna mzigo wa wakimbizi ulivyo mzito kwa nchi yake, amesema, "kwa sasa, tuna zaidi ya wakimbizi milioni 1.5 nchini. Idadi kubwa ya wakimbizi katika bara la Afrika na ya tatu kwa ukubwa duniani.” 

SDGs 

Uganda imeuambia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa  Serikali nchini humo imeingiza kikamilifu Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa na inafanya kazi pamoja na familia ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine.